MV New Mwanza yafanya jaribio kupima mitambo ndani ya Ziwa Victoria

Mwanza.  Meli ya MV New Mwanza imefanyiwa majaribio ya mitambo ndani ya Ziwa Victoria kwa mwendo wa saa mbili kisha kurejea Bandari ya Mwanza Kusini inakojengwa.

Taarifa iliyotolewa Juni 10, 2025 na Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), inaeleza kuwa, majaribio yaliyofanyika ni pamoja na jaribio la mwendo kwa spidi tofauti, kushusha nanga, uzani wa kuelea pamoja na utulivu wa mitambo kwa ujumla.

“Meli ya MV New Mwanza leo (jana) Juni 10, 2025 wataalamu wameendelea kufanya majaribio ya mitambo yake kwa kuitembeza ziwani kwa mwendo wa saa mbili kwenda umbali mrefu na kurejea katika Bandari ya Mwanza Kusini,” inaeleza taarifa ya Tashico iliyochapishwa katika mtandao wa Instagram.

Jaribio hilo ambalo ni la pili, limefanyika ikiwa ni miezi michache imepita tangu kampuni hiyo ipokee kontena tisa zenye samani za viti ambazo tayari zimefungwa ndani ya meli hiyo.

Mafundi wakiangalia mitambo wakati wa majaribio ya meli ya Mv Mwanza yaliyofanyika kwa saa mbili jana Juni 10, 2025.

Jaribio la kwanza lilifanyika Machi 26, 2024, meli hiyo ilifanya safari ya kwanza ya majaribio ya kiufundi katika Ziwa Victoria ili kubaini utendaji kazi wa mitambo iliyosimikwa ndani yake.

Majaribio hayo yalianza kwa kuhusisha wataalamu 60 kutoka ndani na nje ya nchi wakiwamo makandarasi, wafanyakazi wa meli wakiongozwa na nahodha wao, wahandisi wa meli, wasambazaji wa vifaa na mitambo iliyosimikwa kwenye meli hiyo kutoka Marekani, China, Ujerumani na Korea.

Meli hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2020 na mkandarasi wa Kampuni ya Gas Entec Ship-Building Engineering ya Korea kwa gharama ya Sh124 bilioni, ilitakiwa kukamilika baada ya miezi 24, sasa umefikia asilimia 98.

Meli hiyo inayotajwa kuwa kubwa zaidi kuliko zote katika Ziwa Victoria, itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari 20 na malori matatu, ikiwa na ghorofa nne, uzito wa tani 3, 500, urefu wa mita 92.6 na upana wa mita 17.

Itafanya safari zake kati ya Bandari za Mwanza, Kemondo, Bukoba, Portbail nchini Uganda na Kisumu nchini Kenya.

Meli ya MV New Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ itakuwa na madaraja tofauti kwa ajili ya abiria kulingana na mahitaji na uwezo wao kiuchumi.

Ndani ya meli hiyo, kutakuwa na daraja la hadhi ya juu (VVIP) lenye uwezo wa kuhudumia abiria wawili, daraja la watu mashuhuri (VIP) litakalobeba abiria wanne, daraja la kwanza litakalohudumia abiria 60 na daraja la biashara llitakalobeba abiria 100.

Madaraja mengine ni la pili litakalotumiwa na abiria 200 na daraja la uchumi litakalobeba abiria 836.

Muonekano wa ndani wa meli ya Mv Mwanza baada ya kuwekewa viti.

Mkazi wa jijini Mwanza, Baraka Mussa amesema ujenzi wa meli hiyo utakapokamilika na kuanza safari, utawanufaisha wafanyabiashara wa  mikoa ya kanda ya ziwa kwenda nchi za Kenya na Uganda, lakini pia kutachochea shughuli za kiuchumi mkoani Mwanza.

Sophia Kija, ameiambia Mwananchi kuwa kati ya mambo ambayo Serikali imeamua kuwawezesha wakazi wa kanda ya ziwa ni na usafiri wa majini na barabara.

“Hii meli ikianza kazi, hofu ya changamoto ya usafiri itaisha, tutakuwa na uhakika wa kusafiri ndani na nje ya Tanzania na hata kusafirisha biashara zetu kwenda mfano Uganda na Kenya kutokea hapa Mwanza,” amesema Kija.

Related Posts