Mzee adaiwa kujinyonga kisa mbuzi

Arusha. Mkazi wa Kijiji cha Nambere, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Joseph Melau ambaye anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 60 na 65, inadaiwa amefariki dunia kwa kujinyonga ndani ya nyumba yake.

Tukio hilo linadaiwa kusababishwa na msongo wa mawazo uliotokana na kudhulumiwa mbuzi wake wawili.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, Melau alinunua mbuzi hao wawili kutoka kwa kaka yake na kuwaweka kwa muda katika banda lake la mifugo (la kaka yake), akisubiri kukamilisha ujenzi wa banda lake binafsi nyumbani kwake.

Hata hivyo, siku aliyokwenda kuwachukua mbuzi hao, alinyimwa jambo ambalo linadaiwa kumsababishia msongo mkubwa wa mawazo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Juni 11, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi cha kifo hicho.

“Upelelezi bado unaendelea kuhusu mazingira ya tukio hili. Tutatoa taarifa kamili mara uchunguzi utakapokamilika,” amesema Kamanda Masejo.

Kwa upande wake, mtoto wa marehemu, Wilson Joseph amesema baba yake alirudi nyumbani siku ya Ijumaa (Juni 6, 2025) akiwa na hasira, akieleza kuwa amepigwa na ndugu zake na kunyimwa mbuzi aliowanunua wiki iliyopita.

“Sikujua alinunua lini hao mbuzi, lakini siku hiyo alirudi akiwa na machungu sana. Aniambia wazi kuwa atajinyonga. Nilijaribu kumtuliza akanielewa, tukaachana kila mmoja akaenda kulala,” amesema Wilson.

Ameongeza kuwa Jumatatu, baba yake alirudi akiwa amelewa na akazungumza kwa msisitizo kuwa angekunywa sumu. “Nilijaribu kumsihi tena asifanye hivyo, lakini aliendelea kurudia kauli hiyo hadi alipolala usingizi,” amesimulia mtoto huyo.

Wilson amedai siku iliyofuata, alimuomba jirani aje azungumze na baba yake ili kumkanya kutokana na kauli zake za kujiua, kisha akaondoka kuelekea kazini.

Hata hivyo, alipokuwa kazini mchana alijaribu kumpigia simu baba yake lakini hakupokea. Hali hiyo ilimpa wasiwasi na kuamua kurejea nyumbani saa tisa alasiri.

“Nilipofika nyumbani nilikuta watu wamekusanyika. Nilipoingia ndani, nilikuta mwili wa baba yangu ukining’inia kwenye kamba ya neti, tayari akiwa amekufa,” ameeleza kwa masikitiko.

Naye jirani wa marehemu ambaye pia ni balozi wa nyumba kumi, Lucas Kabaha amesema tukio hilo linaaminika kusababishwa na msongo wa mawazo baada ya mzee huyo kudai kudhulumiwa mbuzi wake.

“Siku ya tukio Juni 10, 2025, jioni, nilipigiwa simu na majirani kuwa mzee Melau amejinyonga. Nilipofika nilikuta mwili wake ukiwa umening’inia. Nilimpigia simu mwenyekiti ambaye aliwasiliana na polisi ambao waliuchukua mwili kwenda kuuhifadhi,” amesema Kabaha.

Amesema huenda marehemu alifikia hatua hiyo kutokana na ukosefu wa mtu wa karibu wa kuzungumza naye mara kwa mara, hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa akiishi peke yake baada ya mkewe kuondoka na kijana wake kila siku huwa anashinda kazini.

Related Posts