Kigoma. Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye ametoa rai kwa jamii kuachana na mila na desturi zinazochochea ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu na wasiojiweza.
Kwa mujibu wa Andengenye vitendo hivyo vinakiuka misingi ya utu na vinadhoofisha ustaarabu wa jamii.
Amesisitiza kuwa jamii iliyostaarabika hujengwa kwa misingi ya heshima, usawa na mshikamano, hivyo ni muhimu kuendelea kutoa elimu ya maadili ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuheshimiana na kushirikiana bila kujali tofauti zao.
Andengenye ametoa kauli hiyo leo Juni 11, 2025 katika Makazi ya Wazee Kibirizi, aliposhiriki shughuli za usafi na kugawa zawadi mbalimbali.
Tukio hilo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Uelewa kuhusu Watu Wenye Ualbino, ambayo kitaifa yatafanyika Ijumaa, Juni 13, 2025, mkoani Kigoma.
“Tunatoa wito kwa watu wote kuendelea kuyakumbuka makundi maalumu wakiwemo wazee, kwa upande wa ndugu zetu wenye ualbino tuendelee kupiga vita mila, desturi na tamaduni potofu dhidi yao na tutafanya hivyo kama sisi wenyewe tutakuwa na uelewa mzuri katika kujenga nchi yenye ustaarabu kwa wote,” amesema.
Amesema maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Community Centre, Kigoma, ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Maadhimisho hayo yatasindikizwa na kaulimbiu isemayo: “Kushiriki katika uchaguzi ni haki kuchagua na kuchaguliwa, linda haki za watu wenye ualbino.”
Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Godson Mollel ametoa wito kwa jamii na wadau kuwasaidia wazee wanaoishi katika Kituo cha Kibirizi bila ubaguzi, akisema maisha ya kila binadamu hutegemea mipango ya Mungu.
“Wazee hawa hawako hapa kwa bahati mbaya. Ni mpango wa Mungu kujidhihirisha kupitia maisha yao. Tuwaenzi na tuwatunze kwa kuwa sisi pia tunaelekea uzeeni. Maandiko yanasema kila aliyezaliwa na mwanamke, siku zake si nyingi na zimejaa taabu,” amesema.
Akizungumzia dhana potofu kuhusu watu wenye ualbino, Mollel amekemea matumizi ya jina ‘watu wenye ulemavu wa ngozi’, akisisitiza kuwa wanapaswa kutambulika kama ‘watu wenye ualbino’.
“Kuna wanaodhani hatufai kuwa viongozi, wengine wanatuita watu wenye ulemavu wa ngozi. Ieleweke kuwa ualbino ni hali kama nyingine ya kibinadamu, na baadhi yetu pia tuna ulemavu wa viungo, lakini si wote. Tunapaswa kutambuliwa kwa heshima kama watu wenye ualbino,” amesema.
Kwa upande wake Katibu wa Makazi ya Wazee Kibirizi, Veronica Ramadhan ameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma kwa wazee, zikiwemo mavazi, chakula na za afya zinazojumuisha kupatiwa daktari maalumu anayewahudumia moja kwa moja tofauti na awali.
Hata hivyo, ameomba Serikali kwa kushirikiana na wadau kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio, akieleza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakikatiza katika eneo hilo na kuiba mali za wazee.