Sheikh Ponda: Ni umuhimu viongozi wa dini kushiriki siasa

Dar es Salaam. Sheikh Issa Ponda ni mmoja wa viongozi wa dini ya Kiislamu maarufu nchini ambaye kwa nyakati tofauti, amekuwa akiingia matatani na kufunguliwa kesi tofauti, ambazo mara kadhaa amekuwa akizishinda na kuachiwa huru.

Yeye na wenzake 49 waliwapandishwa kizimbani Oktoba 18, 2012 ikiwa ni mara yake ya kwanza, na kusomewa mashtaka manne kwa pamoja, huku yeye akikabiliwa na shtaka lingine la kula njama.

Katika kesi hiyo walishtakiwa kwa kuingia kwa jinai katika eneo la ardhi, kulikalia kwa nguvu na wizi wa vifaa vya ujenzi, mali ya kampuni ya Agritanza, vyenye thamani ya Sh59.6 milioni.

Katika hukumu ya kesi hiyo, Mahakama ilimhukumu Sheikh Ponda kifungo cha nje kwa kosa moja la kuingia kwa nguvu katika eneo hilo la ardhi isiyo yake huku wengine wote wakiachiwa huru na Mahakama.

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania na kada wa ACT-Wazalendo, Sheikh Ponda Issa Ponda akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa Mwananchi.

Si hilo tu, yapo matukio mengine na katika mojawapo aliwahi kupigwa risasi ya bega katika harakati zake mkoani Morogoro.

Mwananchi limefanya mahojiano na Sheikh Ponda, katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, ambaye licha ya kuwa kiongozi wa dini, Juni 5, 2025 alijiunga na ACT Wazalendo.

Katika mahojiano hayo, Sheikh Ponda amezungumzia masuala tofauti ikiwamo kuchanganya dini na siasa, tetesi za kugombea ubunge katika moja ya majimbo Dar es Salaam pamoja na sababu za kukichagua ACT Wazalendo kuwa chama chake.

Wakati akijiunga na chama hicho, kumekuwa na mjadala mpana kuhusu kuchanganya dini na siasa, baadhi ya wadau wanajielekeza kwenye athari zake huku wengine wakifafanua faida zake kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Akizungumzia hilo, Sheikh Ponda anasema sheria za Tanzania hazizuii kiongozi wa dini kushiriki siasa, hivyo anaweza kushiriki siasa kama mwanachama na akabaki kuwa kiongozi wa dini katika jamii anayoishi.

 “Kwanza, mimi ni kiongozi wa dini na hata kama nimejiunga kwenye chama cha siasa, sitoki kwenye dini. Nitaendelea kuwa kiongozi wa dini na nitaishi kwenye maadili yangu, sitabadilika kuwa kitu tofauti.

“Hii ni kwa mujibu wa sheria. Sheria za Tanzania hazikatazi kiongozi wa dini kushiriki siasa kwa sababu kiongozi wa dini anashiriki siasa kwa sheria zilizopo. Hakuna kiongozi wa dini anaingia pale, anasema yeye anashiriki siasa kwa sababu ya injili, ni kwa sababu ya sheria na Katiba ya nchi,” anasema.

Anasema ni muhimu viongozi wa dini kushiriki siasa na kuingia kwenye vyombo vya uamuzi kwa sababu wao wana sifa ambazo wanasiasa wengine hawana, sifa ya uadilifu na ukweli katika kusimamia mali za umma.

Katibu wa Idara ya Itikadi, Mawasiliano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Salim Biman (kulia) akimtambulisha kada mpya wa chama hicho, Sheikh Issa Ponda aliyepokewa katika makao makuu ya chama hicho Magomeni jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi Juni 5, 2025. Picha na Sunday George

Sheikh Ponda anasema leo ukiangalia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), huwezi kuamini watu waliopewa dhamana wametumia vibaya fedha za umma, jambo ambalo viongozi wa dini hawawezi kufanya.

“Watu wanaosema viongozi wa dini wasishiriki siasa, hawajui historia ya Tanzania. Fikra ya ukombozi au uhuru wa Tanzania ilitoka kwa viongozi wa dini, ukiangalia kwenye ile kamati ndogo ya TAA, alikuwepo Mufti Hassan bin Amir wa Tanganyika.

“(Mufti Amir) aliwashajihisha watu kuingia kwenye chama cha TAA. Pia, Zanzibar, chama kilicholeta uhuru cha ZNP, kiongozi wake alikuwa ni Ali Muhsin Al-Barwani, yule alikuwa sheikh na ametafsiri vitabu vingi vya dini ikiwemo Quran Tukufu,” anasema Ponda.

Anasema hao ambao hawataki viongozi wa dini kushiriki siasa, wanataka wawe watazamaji tu, hawajui historia ya Tanzania, na viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika siasa za nchi yoyote na hakujawahi kuwa na tatizo katika jambo hilo.

“Hiyo dhamira siyo nzuri. Sisi, kwenye dini ya Uislamu hakuna hiyo kitu, kwamba dini na siasa ni vitu viwili tofauti, hapana,” anasisitiza.

Sheikh Ponda anahusisha hilo na tukio la Juni 2, 2025 la kufungiwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, akisema si sahihi kufungia nyumba ya ibada kwa kuwa inawanyima watu haki yao ya kuabudu.

Sheikh Ponda anasema; “Hili ni jambo baya sana, haliungwi mkono na mtu yeyote mwenye nidhamu. Huwezi kufunga nyumba ya ibada, wala haiingii akilini, unafungaje nyumba ya ibada? Ile ni haki kubwa ya watu kuabudu, ni haki ya kikatiba, kama kuna mtu amekosea, afikishwe mbele ya chombo cha kutenda haki ambacho ni Mahakama.”

Sheikh Ponda anabainisha kwamba ameamua kujiunga na chama cha siasa kwa lengo la kuongeza nguvu za kisheria, ili kuwa na uwanja mpana wa kisheria katika kufanya kazi za umma.

Anasema ameamua kujiunga na ACT Wazalendo kwa sababu ni chama makini na mahiri licha ya uchanga wake na amebaini kwamba umakini huo unatokana na watu waliomo mle ndani ambao ni wakongwe katika siasa za mageuzi.

Kiongozi huyo wa dini anatolea mfano viongozi kama Juma Duni Haji, kuwa ni mtu mwenye uzoefu mkubwa katika siasa za mageuzi. Pia, amemtaja Othman Masoud Othman kama mtu mwenye msimamo usioyumba na uzoefu wa kutosha.

“Kuna watu kama Othman Masoud Othman, wana mvuto mkubwa sana. Ukiangalia ule wasifu wake, unaona ni mtu ambaye ungependa ushirikiane naye katika kufanya hizi kazi kwa sababu ni mtu mweledi, mkweli na jasiri,” anasema Sheikh Ponda.

Kingine kinachomvutia, anasema chama hicho tayari kinashiriki katika kuunda Serikali upande wa Zanzibar.

Hata hivyo, anasema hamaanishi kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) inafanya vizuri huko Zanzibar, bali ni hatua nzuri ya matumaini.

Baada ya kujiunga na ACT Wazalendo, Sheikh Ponda alianza kuhusishwa na mbio za ubunge katika moja ya majimbo ya Dar es Salaam, hususan jimbo la Kigamboni, hata hivyo anasema hajapokea ushauri wowote kuhusu hilo, hivyo hawezi kusema chochote kwa sasa.

“Mimi sijasema, lakini pia hao wanaonitaja, hii habari ndiyo kwanza naisikia kwako, sijui wao wameipata wapi. Nilichokifanya mimi ni kwamba nimejitokeza kuchukua kadi, kwa hiyo niko wazi, kwamba sasa ninaweza kushiriki siasa katika ngazi tofauti tofauti.

“Sijapata ushauri, kwa hiyo siwezi kusema chochote kwa sababu sijashauriwa, hajatokea mtu kuja kuniambia fanya hiki, fanya hiki. Mimi nia yangu ni kushiriki siasa kwa kuwa nina haki za kisheria,” anaeleza kiongozi huyo wa dini.

Sheikh Ponda anasema hali ya kisiasa nchini haivutii kwa sababu ule utamaduni wa kuzungumza uliokuwepo huko nyuma, haupo tena, badala yake taifa limekwenda kwenye siasa za ubabe.

Anasema kinachoendelea sasa, kuna mvutano kuhusu namna uchaguzi utakavyoendeshwa na baadhi ya watu wameamua uchaguzi usifanyike. Anasema katika hili, kuna umuhimu wa kuzungumzia suala hilo.

“Mazungumzo watu hawachoki, huwezi kusema umechoka kuzungumza au hutaki kuzungumza. Mazungumzo siku zote yanatengeneza mambo, mpaka mfike mahala muone ni nani hataki kutengeneza mambo.

“Kwa hiyo, naiona hali si nzuri kwa sababu ya kutoka kwenye ule utamaduni wa busara, utamaduni wa kuzungumza, ambao kila mara tumezoea kuutumia,” anasema.

Sheikh Ponda anatoa wito kwa Watanzania kushiriki uchaguzi mkuu ujao kwa kuwajengea watu uwezo wa kutambua haki zao za msingi na kuzisimamia.

“Kwa mfano, unakwenda kupiga kura, halafu mtu anakuzuia usilinde kura yako, huyu ni mtu anayekunyima haki yako ya msingi. Anakwambia kakae mita ngapi, kwa nini? Kura nimepiga hapa, iko hapa kura yangu, wewe unaniambia nikakae porini huko, hapa analinda nani?” anahoji.

Anasisitiza Watanzania washiriki kwenye uchaguzi na kulinda haki zao na wasiruhusu wengine kuchezea haki zao.

Anasema Watanzania wajenge utamaduni wa kusimamia haki zao popote bila kuvunja sheria.

Related Posts