TCAA NA WOMEN IN AVIATION WAUNGANA NA SMALL HANDS BIG CHANGE KUPANDA MITI KWA AJILI YA MAZINGIRA

Katika kuhitimisha Wiki ya Mazingira, taasisi ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kwa kushirikiana na Women in Aviation, imeungana na shirika lisilo la kiserikali la Small Hands Big Change katika zoezi la upandaji miti lililofanyika leo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza katika tukio hilo, kwa niaba ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Maria Memba alisema kuwa taasisi hiyo imedhamiria kuunga mkono jitihada za mtoto mdogo anayeongoza Small Hands Big Change, ambaye licha ya umri wake mdogo ameonyesha dhamira ya kweli katika kuhifadhi mazingira.

“Leo tupo hapa kuunga mkono juhudi za mtoto wetu mdogo ambaye amekuja na wazo la kupendeza, la kusaidia mazingira kupitia upandaji wa miti. Kama mnavyojua, tumemaliza Wiki ya Mazingira, hivyo tukasema nasi kama taasisi, hatuwezi kubaki nyuma. Tumeingia katika makubaliano (MoU) na Small Hands Big Change ili tushirikiane kwa karibu zaidi katika juhudi hizi,” alisema Maria.

Aliongeza kuwa mazingira hayawezi kutenganishwa na sekta ya usafiri wa anga kwani ndege zinachangia kwa kiasi fulani katika uchafuzi wa mazingira. Kupitia mpango huu wa kupanda miti kila mwaka, mamlaka inalenga kufidia athari hizo na kuendeleza mazingira bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Upandaji miti ni zoezi endelevu, na tumekuwa tukilishiriki kila mwaka. Tunawaalika taasisi zingine pamoja na watu binafsi nao waunge mkono jitihada hizi. Tufanye kwa ajili ya leo na kwa ajili ya kizazi kijacho. Tushirikiane kuifanya Tanzania kuwa ya kijani zaidi,” alihimiza.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Women in Aviation alieleza kuwa wanawake katika sekta ya anga wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya, hasa kwa kushiriki katika shughuli za kijamii na kimazingira.

Tukio hilo lilihitimishwa kwa zoezi la upandaji miti na kuwahamasisha vijana na watoto kushiriki kikamilifu katika kuhifadhi mazingira. Mgeni rasmi alitoa pongezi za dhati kwa mtoto huyo mdogo kwa kuonesha mfano wa kuigwa na kuahidi kuendelea kushirikiana naye katika shughuli zijazo.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Maria Memba akipanda mti katika eneo la Mamlaka ya Usafiri wa Anga ili kuunga za kulinda na kuhifadhi mazingira  kupitia shirika lisilo la kiserikali la Small Hands Big Change

Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Small Hands Big Change Akoth Okeyo akipanda mti katika eneo la mamlaka ya Usafiri wa Anga

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Maria Memba akizungumza kuhusu Mamlaka hiyo ilivyodhamiria kuunga mkono jitihada za mtoto mdogo anayeongoza Small Hands Big Change ili kuweza kutunza na kuhifadhi mazingira.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Maria Memba akisikiliza risala iliyokuwa inasomwa na Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Small Hands Big Change Akoth Okeyo wakati wa zoezi la kupanda mti katika eneo la mamlaka ya Usafiri wa Anga

Mkaguzi Mwandamizi wa Huduma za hali ya hewa na Mazingira wa mamlaka hiyo John Mfungo akipanda mti 

Baadhi ya wanafunzi na walimu kutoka shule mbalimbali za msingi wakipanda miti katika eneo la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)

Related Posts