Ahmedabad. Mwaka 2025 umeendelea kuwa wa majanga kwa sekta ya usafirishaji wa anga duniani baada ya ndege ya Shirika la Ndege la Air India yenye abiria na wahudumu 242 kuanguka eneo la makazi la Meghani Nagar nchini India.
Ndege hiyo aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyokuwa safarini kutoka Ahmedabad India kuelekea jijini London nchini Uingereza ilianguka jana Alhamisi Juni 12, 2025 Saa 7: 38 mchana na kuua watu 241 huku mmoja akinusurika kwa mujibu wa Al-Jazeera.
Katika abiria waliokuwamo ndani ya ndege hiyo, ni Vishwash Kumar Ramesh ambaye ni raia wa Uingereza mwenye asili ya India aliyetoka akiwa hai.
Daktari anayemhudumia katika Hospitali ya Ahmedbad nchini humo, Dk Dhaval Gameti amesema abiria huyo ana majeraha makubwa maeneo mbalimbali ya mwili wake.
“Ana majeraha mengi maeneo mengi ya mwili wake,” Dk Gameti amelieleza Shirika la Habari la Associated Press.
Vishwashkumar Ramesh alikuwa amekaa kwenye ‘siti’ namba 11A wakati ndege hiyo aina ya Boeing 787-8 inapata ajali.
Kwa mujibu wa Hindustan Times, manusura wa ajali hiyo akizungumza hospitalini alipolazwa akipatiwa matibabu amewaeleza kuwa baada ya kupata fahamu ameshuhudia miili ikiwa imetapakaa ndani ya ndege hiyo.

Manusura huyo amesema baada ya kuona hali ile alijivuta na kutokea mlango wa dharura ulioko nyuma ya ndege hiyo.
“Nilipopata fahamu nilikuwa nimezungukwa na miili ya watu, niliogopa sana. Nikajivuta kutoka eneo lile kulikuwa na vipande vya mabaki ya ndege kila mahali kuna mtu akanivuta mkono hadi kwenye Ambulance iliyonileta hospitalini,” amesema Ramesh.
Ndege hiyo ilikuwa na abiria 230 na wahudumu 12, wakiwamo Rubani Mkuu, Sumit Sabharwal na Rubani Msaidizi, Clive Kunder. Miongoni mwao, 169 ni raia wa India, 53 wa Uingereza, mmoja wa Canada na 7 wa Ureno.
Kwa mujibu wa Kamashna wa Polisi eneo la Ahmedabad, Gyanender Singh Malik athari za ajali hiyo huenda zikaongezeka kwa kuwa, ndege hiyo ya abiria kabla ya kulipuka iligonga kwenye jengo ambalo ni ‘Hosteli’ ya Chuo cha Afya cha Serikali maarufu kama ‘B. J Medical College’ nchini humo.
“Miongoni mwa watu ambao pia wamefariki kutokana na ajali hii ni wakazi wa eneo ilipoangukia. Bado tunafanya uchunguzi na kubaini waliofariki na kuathiriwa,” amesema Malik.
Waziri wa Anga wa India, Kinjarapu Ram Mohan Naidu amesema uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo, umeshaanza na kuahidi kuanika majibu ya chanzo cha ajali hiyo.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amesema amepokea taarifa ya ajali hiyo kwa mshtuko mkubwa.
“Kuna janga limetokea Ahmedabad, limetuhuzunisha na kutuumiza. Machozi yetu yanabubujikwa pamoja na familia za walioathiriwa na ajali ya ndege hii,” ameandika Modi kupitia akaunti yake ya mtandao wa X(Twitter).

Mbali na Modi, Rais wa Russia Vladimir Putin naye ameandika kuwa: “Natoa salamu za pole kwa Rais wa India Droupadi Murmu na Waziri Mkuu Narendra Modi, tunaomboleza pamoja kufuatia ajali ya hiyo ndege”
“Nitoe pole kwa familia za waliofariki katika ajali hiyo na niwatakie majeruhi kupona kwa haraka,” ameandika.
(Imeandaliwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari)