‘Bwana harusi’ aliyeiba gari, apigwa faini ya Sh500,000

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu ‘Bwana harusi’ Vincent Masawe (36) kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi sita baada ya kupatikana na hatia katika shtaka moja la wizi wa gari aina ya Toyota Ractis, lenye thamani ya Sh15 milioni.

Pia, Mahakama hiyo imemuhukumu mshtakiwa huyo kutokufanya kosa lolote la jinai kwa kipindi cha miezi 12 kuanzia leo Alhamisi Juni 12, 2025.

Vilevile, Mahakama hiyo imetoa amri kuwa gari hiyo aliyoiba Vicent, arejeshewe mwenye gari ambaye ni Sylvester Masawe.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo amefanikiwa kulipa faini hiyo, hivyo kukwepa kifungo cha miezi sita jela.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Alhamisi Juni 12, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, baada ya mshtakiwa kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi.

Masawe alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni wizi wa gari aina ya Toyota Ractis lenye thamani ya Sh15 milioni ambalo aliazimwa kwa ajili ya kulitumia katika sherehe ya harusi yake na kujipatia fedha taslimu Sh3milioni kwa njia ya udanganyifu.

Lakini baada ya kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ya kukiri makosa na kuomba kupunguziwa adhabu, mshtakiwa huyo alifutiwa shtaka moja la kujipatia Sh3 milioni na kubaki na shtaka la wizi wa gari ambalo ndio alilotiwa hatiani na Mahakama hiyo.

Itakumbukwa Mei 19, 2025 Serikali iliieleza Mahakama hiyo mshtakiwa amemuandikia barua DPP akiomba kukiri mashtaka yake na kuomba kupunguziwa adhabu.

Baada ya barua hiyo kupokelewa ofisi ya DPP, Serikali iliomba Mahakama iwapangie tarehe kwa ajili ya majadiliano.

Baada ya kukamilika kwa majadiliano hayo, Mahakama ilipewa taarifa na leo, mkataba wa majadiliano ulisomwa mahakamani.

Awali, wakili wa Serikali, Aron Titus ameileza Mahakama kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya uamuzi baada mshtakiwa amefanya majadiliano ya kukiri mashtaka yake.

Wakili Titus baada ya kutoa taarifa hiyo, hakimu Nyaki alisema mshtakiwa ametiwa hatiani katika shtaka la wizi wa gari na kwa kuwa alifanya majadiliano ya kuimaliza kesi, Mahakama inamuhukumu kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi sita.

“Kwenye majadiliano ya kuimaliza kesi, Mahakama inatoa adhabu kwa mshtakiwa huyu kutokufanya kosa la jinai kwa kipindi cha miezi 12  na kwenye kosa ulilotiwa hatiani, mahakama hii inakuhukumu kulipa faini ya Sh500,000 na ukishindwa utatumikia kifungo cha miezi sita jela” amesema Hakimu Nyaki na kuongeza;

“Na pia Mahakama hii inatoa amri, gari aina ya Toyota Ractis irejeshwe kwa mwenye gari,” amesema Hakimu.

Katika kesi ya msingi, Vicent alikuwa anakabiliwa na kesi ya jinai yenye mashtaka mawili.

Massawe anadaiwa kutenda makosa hayo Novemba 15, 2025 kinyume na vifungu  namba 258 na 273(b) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kwa mara ya kwanza Massawe alifikishwa mahakamani Desemba 24, 2024 na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Katika shtaka la kwanza la wizi wa kuaminika, Masawe anadaiwa kuwa akiwa wakala, tarehe hiyo  Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, aliiba gari aina ya Toyota Ractis.

Gari hilo lenye thamani ya Sh15 milioni, kwa mujibu wa upande wa mashtaka ni mali ya Silvester Masawe.

Anadaiwa aliazimwa gari hilo na Silvester kwa lengo la kulitumia katika sherehe ya harusi yake lakini baada ya hapo, hakurudisha gari kama ambavyo walikubaliana.

Katika shtaka la pili la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, anadaiwa kuwa tarehe hiyohiyo ya tukio Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, kwa lengo la kuiba na kutapeli, alijipatia fedha taslimu Sh3 milioni kutoka kwa Silvester.

Anadaiwa kuwa alijipatia fedha hizo kwa kuahidi kuwa atamrudisha fedha hizo baadaye, wakati akijua kuwa ni uongo na hakuweza kurudisha fedha hizo hadi alipokamatwa.

Kabla ya kukamatwa na kisha kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka hayo, Massawe mkazi wa Ungindoni, Kigamboni jijini Dar es salaam alidaiwa kupotea.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, Massawe ambaye alikuwa fungate baada ya kufungua ndoa, alitoa taarifa kwa marafiki zake kuwa alikuwa Mbezi na kwamba alikuwa anafuatiliwa na gari ambalo alikuwa halijui.

Tangu siku hiyo, hakuonekana wala kupatikana kwenye simu zake.

Hata hivyo, Desemba 17, 2024 Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitoa taarifa za kukamatwa kwake.

Kamanda Muliro alisema kuwa Massawe alikamatwa Desemba 15, 2024, akiwa kwa mganga wa kienyeji, Pemba na  alikuwa na tuhuma za wizi wa kuaminiwa na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.

Related Posts