Unguja. Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa mwaka wa fedha 2025/26 imependekeza kuongeza viwango vya ushuru katika bidhaa mbalimbali, zikiwamo dizeli, petroli, pombe kali, mvinyo na shisha, hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh38.27 bilioni.
Bajeti hiyo pia imejumuisha ongezeko la mishahara kwa madiwani na masheha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha masilahi ya viongozi wa ngazi za msingi na kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hotuba ya Bajeti ya SMZ imewasilishwa leo, Alhamisi Juni 12, 2025, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha na Mipango), Dk Saada Mkuya Salum huku akiomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha jumla ya Sh6.9 trilioni kwa ajili ya mwaka wa fedha 2025/26.
Maombi hayo yamelenga kuongeza mapato ya ndani, kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti matumizi ya shisha na vileo vingine vyenye madhara, kuwalinda vijana dhidi ya athari za ulevi na kuimarisha viwanda vya ndani na kukuza ajira kwa wananchi.
Dk Mkuya amesema SMZ imetenga Sh3.2 bilioni kwa ajili ya kuongeza mishahara ya madiwani na masheha.
Amesema pia, Serikali inapendekeza marekebisho ya kodi kwa bidhaa mbalimbali ili kuongeza mapato na kuimarisha sekta za uzalishaji na afya.
Dk Mkuya amesema Serikali itapunguza kodi za leseni za barabara kwa dizeli na petroli kwa kuongeza tozo kutoka Sh38 hadi Sh100 kwa kila lita moja ya mafuta, pamoja na kuongeza tozo ya kuendeleza barabara kutoka Sh100 hadi Sh200 kwa kila lita.
“Hatua hizi zinatarajiwa kuleta mapato ya Sh35.75 bilioni, yatakayowekezwa katika kuboresha miundombinu ya barabara nchini,” amesema.
Pia, Dk Mkuya amesema kwamba ushuru wa bidhaa kwa vinywaji vikali na mvinyo utapandishwa kutoka Sh4,386 hadi Sh6,000 kwa lita moja, hatua inayolenga kuongeza mapato ya Sh1.25 bilioni kwa ajili ya kuimarisha Mfuko wa Afya.
Kuhusu shisha, licha ya ushuru wa asilimia 120 ulioanzishwa mwaka 2024/25, matumizi yameendelea kuongezeka, hasa miongoni mwa vijana.
Amesema Serikali inapendekeza ushuru wa Sh28,232 kwa kila kilo moja ya ladha ya shisha ili kupunguza matumizi na kulinda afya za wananchi na inatarajia kukusanya Sh1.27 bilioni zitakazotumika katika Mfuko wa Afya.
Pia, ili kuimarisha uzalishaji viwandani, Serikali imependekeza kupandisha ushuru kutoka Sh300 hadi Sh1,000 kwa kila kilo moja ya kuku na samaki wanaoingizwa Zanzibar.
“Hatua hii inalenga kuendeleza viwanda vya ndani, kuimarisha ushindani wa sokoni, na kuongeza ajira kwa wananchi. Mabadiliko haya yanatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh7.25 bilioni,” amesema.
Makusanyo na Deni la Taifa
Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali ilipanga kukusanya Sh5.182 trilioni kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje, hadi kufikia Machi 31, 2025, Sh2.204 trilioni zilikamilika kukusanywa.
Dk Mkuya amesema deni linalodhaminiwa na SMZ limefikia Sh1.334 trilioni hadi Machi 2025.
Kati ya deni hilo, la ndani linakadiriwa kuwa Sh1.319 trilioni, linalojumuisha asilimia 99 ya jumla ya deni, wakati la nje likiwa ni Sh15.20 bilioni, sawa na asilimia moja ya deni lote.
Aidha, deni hilo limeongezeka kwa Sh400.6 bilioni ikilinganishwa na deni lililoripotiwa Machi 2024, lililokuwa Sh934 bilioni.
Dk Mkuya ameeleza kuwa, kati ya deni la ndani, Sh557.5 bilioni linalotokana na hati fungani za muda mrefu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huku Sh761.9 bilioni likitokana na mikopo kutoka taasisi za kifedha mbalimbali.
“Kwa upande wa mwenendo wa makusanyo ya mapato, Serikali inatarajia kukusanya Sh4.057 trilioni ifikapo Juni 2025, sawa na asilimia 78 ya makadirio ya jumla ya Sh5.182 trilioni kwa mwaka mzima wa fedha,” amesema Dk Mkuya.