:::::::
Kila Mtanzania anadaiwa takribani Sh. 1,668,176.80 kulingana na deni la Taifa ambalo limefikia Sh. trilioni 107.7, Machi 2025, kutoka Sh. trilioni 91.7 Machi mwaka jana.
Hii ni kwa sababu idadi ya Watanzania imeongezeka hadi 64,241,822 mwaka 2024 kulinganishwa na watu 61,718,700 mwaka 2023.
Akiwasilisha leo bungeni Juni 12, 2025 taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2025/26, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema fedha zilizokopwa zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
“Ongezeko la deni lilitokana na serikali kuendelea kupokea mikopo mipya kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, ukiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji,” amefafanua. Kuhusu idadi ya watu, Waziri Mkumbo amesema Tanzania Bara inakadiriwa kuwa na watu 64,241,822 mwaka 2024 kulinganishwa na watu 61,718,700 mwaka 2023.
Wakati deni likiwa hivyo, Prof. Mkumbo amesema Pato la Taifa kwa Mtu lilikuwa wastani wa Sh. milioni 3.2 mwaka 2024 kulinganishwa na wastani wa Sh. milioni 3.05 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 4.8. “Kiasi hicho ni sawa na Dola za Marekani 1,227.4 kwa mtu mwaka 2024 kulinganishwa na dola za Marekani 1,276.8 kwa mtu mwaka 2023,” alisema.
Cc Nipashe