Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Zanzibar inajipanga kuendelea kujenga miundombinu ya viwanja vya ndege ili kuifanya kuwa kituo bora cha utoaji wa huduma za usafiri wa anga Afrika na duniani.
Dk Mwinyi ameyasema hayo leo Juni 12, 2025 alipofungua mkutano wa Huduma za Usafiri wa Anga pamoja na Utalii Afrika (AviaDev) ambao una washiriki zaidi ya 50, ukizikutanisha nchi 50 na mashirika 48 ya ndege kutoka mataifa hayo.
Amesema kwamba upanuzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume na ujenzi wa uwanja wa ndege mpya wa Pemba ni miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali kuimarisha huduma za usafiri wa anga nchini.
“Hatua hii itaifungua Zanzibar kikanda na kimataifa kwa mashirika zaidi ya ndege kuja nchini, na hivyo kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea pamoja na kutangaza utalii wa Zanzibar,” amesema Dk Mwinyi
Amesema huduma za usafiri wa anga ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa sekta ya utalii inayochangia asilimia 30 ya pato la Taifa na kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar, huku Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi na mashirika ya ndege ya kikanda na kimataifa ili kuongeza ufanisi na usalama katika viwanja vya ndege.
Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha huduma katika viwanja vya ndege, ikiwemo kushirikiana na sekta binafsi kupitia sera ya PPP, mashirika ya ndege ya kikanda na kimataifa.
Sambamba na hilo pia inafanya jitihada kusimamia ipasavyo kanuni na miongozo ya huduma za usafiri wa anga na hali ya usalama wa nchi hatua inayochangia kuongezeka kwa mashirika ya ndege yanayotoa huduma nchini.
Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohammed amesema mkutano huo umedhihirisha uwezo wa Zanzibar kufanyika mikutano mikubwa ya kimataifa hasa katika kukuza sekta ya utali.
Amefafanua kuwa dunia inaona kwamba Zanzibar ipo tayari kukuza usafiri wa anga unaofikia malengo la kimataifa.
“Sisi tunajivunia kwamba sekta ya anga imefikia hatua nzuri kwani huduma zetu zimeimarika hasa katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume, lakini pia tuzo mbalimbali tulizozipata kutokana na mafanikio hayo,” amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga amesema hatua hiyo italeta mageuzi makubwa katika sekta ya utalii ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ngege Zanzibar (AAKIA), Seif Abdalla Juma, alisema lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wa sekta ya anga na utalii katika kuboresha huduma za sekta hizo na kukuza sekta ya utalii kwa bara la Afrika.
Amesema tukio hilo limeanza kwa msisimko mkubwa, kuonyesha dira mpya ya maendeleo katika sekta ya usafiri wa anga barani Afrika.
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Peter Ulanga amesema Zanzibar ni eneo zuri la utalii na sekta hiyo inaendeshwa na sekta ya anga hivyo wataendelea kuangalia fursa za kuleta watalii na wageni Zanzibar.
Amesema watatumia fursa ya kuzungumza na wadau ili kupanua wigo wa kufika nchi mbalimbali ambapo hadi sasa Air Tanzania inafika vituo 13 nje ya nchi, 14 ndani ya nchi na wanatarajia kuongeza safari zake kwa kisiwa cha Pemba hivi karibuni.
Baadhi ya washiriki akiwemo Charles Murithi kutoka Shirika la Ndege la Premier Airlines la nchini Kenya, amesema lengo la kushiriki mkutano huo ni kuendelea kutafuta njia kuwezesha ndege zao kufika Zanzibar kwa ajili ya kusafirisha wageni.
Naye Emmanuel Ekpenyong kutoka Puma Energy Tanzania, amesema mkutano huo ni chanzo cha kuongezeka kwa fursa mbalimbali za ajira, sambamba na kukuza utalii ndani ya kisiwa cha Zanzibar