Dar es Salaam. Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema katika mwaka 2025/2026, Serikali inatarajia kutenga Sh19.47 trilioni sawa na asilimia 34.1 ya bajeti Kuu kwa ajili ya kugharamia programu na miradi ya maendeleo.
Fedha hiyo ni ongezeko kutoka Sh15.95 trilioni sawa na asilimia 31.7 ya bajeti kuu ya Serikali ya Sh50.29 iliyotumika mwaka 2024/25.
Hayo ameyasema leo wakati akiwasilisha bungeni Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/26 ikiwa ni maandalizi kuelekea bajeti kuu ya Serikali itakayosomwa jioni ya leo.
Profesa Mkumbo amesema katika kiwango kilichopangwa kutumika, Sh13.32 trilioni ni fedha za ndani na Sh6.15 trilioni ni fedha za nje kutoka vyanzo mbalimbali.
“Pia Serikali inalenga kuongeza zaidi ushiriki na mchango wa sekta binafsi katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia njia bunifu na mbadala za kugharamia miradi ikiwemo njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP),” amesema Profesa Mkumbo.
Akizungumzia vipaumbele vinavyopendekezwa katika mpango huu amesema vimezingatia malengo tarajiwa na matokeo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Katika kuhakikisha ufanisi wakati wa utekelezaji, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itaweka mkazo katika maeneo ya miradi ya kielelezo yenye manufaa na matokeo makubwa na kujielekeza katika vipaumbele ikiwemo kuchochea uchumi shindani na shirikishi.
“Eneo hili litajikita katika kutekeleza miradi na programu za maendeleo zinazolenga kuongeza uwezo wa nchi kikanda na kimataifa, kuimarisha utulivu na uendelevu wa viashiria vya uchumi jumla, kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara na kuendeleza miundombinu ya usafiri na usafirishaji, Tehama na nishati,” amesema Profesa Mkumbo.
Amesema ili kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji huduma serikali itajielekeza katika programu na miradi ya maendeleo inayolenga kuimarisha uzalishaji viwandani. Kukuza Uwekezaji na Biashara.
Programu na miradi itakayotekelezwa katika eneo hili itajielekeza katika kuimarisha mifumo ya kitaasisi, sera na sheria za kodi ili kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji.
Pia, wamelenga kuchochea maendeleo ya watu na ili kufanikisha hilo, programu na miradi ya maendeleo itakayotekelezwa katika eneo hili itajielekeza katika kuimarisha usimamizi na uendeshaji, mifumo na miundombinu ya elimu, afya, maji na mazingira.
Pia, itaongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini na maeneo ya kimkakati, kukuza ujuzi kwa vijana na kutoa mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa wahitimu wa elimu ya juu.
“Pia tutaendeleza rasilimali watu na katika eneo hilo litajumuisha programu na mikakati inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasilimali watu nchini, kuanzia ngazi za elimu ya awali hadi elimu ya juu ili kuwawezesha vijana kujiajiri,” amesema Profesa Mkumbo na kuongeza.
“Eneo hili linajumuisha hatua za kuboresha viwango vya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujuzi adimu ambavyo ni muhimu katika kuongeza tija na ushindani wa wananchi katika kutumia rasilimali zilizopo nchini ili kuleta maendeleo.