Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kuwa licha ya hali ya uchumi duniani kuendelea kuyumba, Tanzania imeonyesha uimara kwa kuendelea kukuza uchumi wake kwa kasi na ustahimilivu wa hali ya juu.
Akitoa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2025/2026 bungeni jijini Dodoma leo, Alhamisi Juni 12, 2025, Profesa Mkumbo alisema mafanikio hayo yanatokana na usimamizi makini wa sera pamoja na mshikamano wa Watanzania katika kujenga uchumi wa Taifa.
“Nihitimishe kwa kulihakikishia Bunge lako tukufu kuwa hali ya uchumi wa nchi yetu kwa sasa ni himilivu, ukiwa na mwelekeo chanya na ukuaji endelevu. Kuimarika kwa uchumi kunatokana na usimamizi makini wa sera za uchumi jumla, pamoja na ushiriki wa wananchi wote katika ujenzi wa Taifa. Ninawashukuru na kuwapongeza Watanzania wote kwa mshikamano huu wa kizalendo,” amesema Profesa Mkumbo.
Profesa Mkumbo amebainisha kuwa licha ya changamoto za kiuchumi duniani, Tanzania imeendelea kuvutia wawekezaji na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta mbalimbali zikiwemo miundombinu, nishati, kilimo na afya -hatua ambazo zimechangia ustawi wa uchumi wa Taifa.
Profesa Mkumbo amesema Pato la Taifa linatarajiwa kuendelea kupanda hadi asilimia 6.0 mwaka 2025 na kufikia asilimia 6.1 mwaka 2026, akisisitiza kuwa msingi wa mafanikio haya ni utekelezaji thabiti wa sera bora za uchumi na ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya Taifa.
“Katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka 2024, Pato Halisi la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 5.6 ikilinganishwa na asilimia 5.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2023,”amesema Profesa Mkumbo
Ameeleza kuwa ukuaji huo umetokana na juhudi endelevu za Serikali katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji, nishati, maji, afya, na elimu; pamoja na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na biashara.
Profesa Mkumbo amesema wananchi wengi nchini wameonyesha kuridhishwa na utendaji wa Serikali,
“Tathmini ya kitafiti inaonyesha kuwa wananchi walio wengi katika nchi yetu wanaridhishwa na utendaji wa Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo,” amesema Profesa Mkumbo
Akitolea mfano matokeo ya utafiti wa Afrobarometer uliofanyika kati ya Juni na Julai 2024, Profesa Mkumbo amesema: “Utafiti umeonyesha kuwa asilimia 71 ya wananchi wote waliohojiwa walisema wanaridhishwa sana na utendaji wa Serikali, huku asilimia 70 wakisema nchi ipo katika mwelekeo sahihi.”