Upelelezi kesi ya kuporomoka jengo Kariakoo, haujakamilika

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili watu sita wakiwemo wamiliki wa jengo lililoporomoka mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, umedai kuwa bado unaendelea na uchunguzi.

Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Alhamisi Juni 12, 2025, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa kutajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ambao wote ni wafanyabiashara na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni Leondela Mdete(49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam(61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour(38) mkazi wa Ilala.

Wengine ni Soster Nziku (55) mkazi wa Mbezi Beach, Aloyce Sangawe(59) mkazi wa Sinza na Stephen Nziku(28) mkazi wa Mbezi beach.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya 31 ya kuua bila kukusudia katika kesi ya mauaji iliyopo mahakamani  hapo.

Roida ameieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geodfrey Mhini, kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

“Mheshimiwa hakimu, washtakiwa wote wapo mbele ya Mahakama yako na kesi yao imeitwa leo kwa ajili ya kutajwa, lakini upelelezi wake bado unaendelea, hivyo tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema.

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 10, 2025 itakapo tajwa na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha  vifo vya watu 31.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022

Related Posts