Dar es Salaam. Serikali imepunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu ‘energy drink’, huku ikitoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia tano katika aisikrimu (lambalamba) na soseji zinazozalishwa nchini.
Ushuru wa bidhaa ya vinywaji hivyo vinavyozalishwa ndani ya nchi, imepungua kutoka Sh561 kwa kila lita hadi Sh134.2 kwa kila lita.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Juni 12, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni Mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/2026.
Dk Mwigulu amesema lengo la hatua hiyo ni kuweka unafuu kwa wazalishaji wa ndani wanaozaliwa vinywaji hivyo (energy drink), kuongeza ushindani na kuchochea uwekezaji nchini.
Hata hivyo, amesema hatua hiyo inatarajia kupunguza mapato ya Serikali kwa Sh1.7 bilioni.
Amesema Serikali inapendekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia tano kwenye aisikrimu zinazotengezwa nchini kwa kutumia kakao au malighafi nyingine, na asilimia 10 kwa zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.
“Bidhaa hizo zinatambulika kwa HS Code 2105.00.00. Lengo la hatua hii ni kupunguza athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya bidhaa hizi, kuongeza mapato ya Serikali na kulinda wazalishaji wa ndani. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh119 bilioni,” amesema.
Waziri amesema Serikali inapendekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia tano kwa soseji na bidhaa zingine zinazofanana na hizo zinazozalishwa nchini na asilimia 10 kwa zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.
Amesema bidhaa hizo zinatambulika kwa HS Code 1601.00.00 na lengo la hatua hiyo ni kuongeza mapato ya Serikali, kuvutia uwekezaji nchini na kulinda wazalishaji wa ndani.
Dk Mwigulu amesema hatua hiyo inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh2.4 bilioni.