Ifakara. Serikali imeendelea kuhimiza wakulima kujiunga na mfumo wa stakabadhi ghalani kama njia ya kuwasaidia kupata masoko ya uhakika na bei nzuri za mazao yao.
Mbali na hilo, pia kudhibiti unyonyaji unaofanywa na madalali wasiokuwa rasmi katika mnyororo wa thamani wa mazao.
Kauli hiyo imetolewa katika kikao maalumu kilichoandaliwa kwa lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa wakulima wa mazao mbalimbali.
Kikao hicho kiliendeshwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghalani ya Wizara ya Viwanda na Biashara, wawakilishi wa benki mbalimbali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, pamoja na wataalamu wa sekta ya kilimo kutoka Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Asangye Bangu amesema kuwa mfumo huo umeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima, hususan wa mazao ya biashara kama ufuta na kokoa, kupata bei nzuri na ya ushindani inayolingana na hali ya soko.
Bangu amesisitiza kuwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, wakulima watauza mazao yao kwa njia ya uwazi zaidi, hali itakayowezesha kuongeza kipato na kujikwamua kiuchumi.
“Mfumo wa stakabadhi za ghalani upo kuhakikisha wakulima wananufaika kwa kuuza mazao yao kwa bei nzuri sokoni.
“Mkoa wa Morogoro umekuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa mfumo huu, hasa hapa Ifakara ambapo wakulima wameanza kuona faida ya kuwa sehemu ya mfumo huu rasmi,” amesema Bangu.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero, Abraham Mwaikwila amesisitiza kuwa elimu zaidi inahitajika kwa wakulima kuhusu mfumo huu ili waweze kuuelewa vyema namna ya kuuutumia.
“Ni muhimu kuondoa dhana potofu kuhusu mfumo huu na kuwaelimisha wakulima jinsi unavyofanya kazi kwa uwazi. Mfumo huu siyo tu unawasaidia kuuza kwa bei nzuri, bali pia ni njia ya kuwaondoa madalali wasio rasmi waliokuwa wakiwanyonya kwa bei ya chini,” amesema.
“Tunataka kuona mkulima analima kwa tija na kuuza mazao yake kwa njia rasmi, salama na yenye faida,” amesema Mwaikwila.
Mmoja wa wakulima waliohudhuria kikao hicho, Gilbert Lipecha amesema kuwa kabla ya mfumo huo kuwepo, walikuwa wakinyonywa na madalali waliokuwa wakitumia vipimo visivyo rasmi kama ndoo na sado na kuweka bei ya mazao kwa mapenzi yao.
“Kabla ya mfumo huu, tulikuwa tunalazimika kuuza kwa bei wanayotaka madalali. Mara nyingi walikuwa wakipima kwa ndoo au sado badala ya mizani rasmi, na hata gunia moja la kilo 100 ilikuwa inafikia hadi kilo 120. Hii ilitufanya tupate hasara kubwa,” amesema Lipecha.
Wakulima wameiomba Serikali na wadau wengine kuongeza juhudi za uelimishaji kwa jamii ili wakulima wengi zaidi wauelewe mfumo huo na kuutumia kwa manufaa yao.