Mamlaka nchini India zimeilieleza Shirika la Habari la Associated Press kuwa hakuna aliyenusurika kwenye ajali ya ndege ya Shirika la Ndege la Air India iliyoanguka eneo la makazi la Meghani Nagar nchini India ikiwa safarini kuelekea jijini London nchini Uingereza, huku viongozi mbalimbali duniani wakituma salamu za rambirambi.
Ndege hiyo iliyokuwa na jumla ya abiria na wahudumu 242 imeanguka saa 7:38 mchana leo Alhamisi Juni 12, 2025, dakika chache baada ya kuruka kutoka Uwanja wa Ndege Ahmedabad nchini India.
Shirika la Habari la Associated Press limeripoti kuwa mamlaka nchini humo zimeithibitishia kuwa hakuna abiria wala mhudumu aliyekuwemo ndani ya ndege hiyo aliyetoka akiwa hai.
Kamishna wa Polisi eneo la Ahmedabad, Gyanender Singh Malik akizungumza na Associated Press amesema; “Hadi inaonekana wazi kuwa hakuna aliyenusurika.”
Mbali na hilo, Malik amesema athari za ajali hiyo huenda zikaongezeka kwani ndege hiyo ya abiria kabla ya kulipuka iligonga kwenye jengo ambalo ni ‘Hosteli’ ya Chuo cha Afya cha Serikali maarufu kama ‘B. J Medical College’ nchini humo.
“Miongoni mwa watu ambao pia wamefariki kutokana na ajali hii ni wakazi wa eneo ilipoangukia. Bado tunafanya uchunguzi na kubaini waliofariki na kuathiriwa,” amesema Malik.
Ndege hiyo ya Air India aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, ilikuwa na abiria 230 na wahudumu 12, wakiwemo Rubani Mkuu, Sumit Sabharwal na Rubani Msaidizi, Clive Kunder.
Iliyopaa kutoka uwanja wa Ahmedabad Saa 7:38 mchana ilikuwa na jumla ya watu 242 ndani. Miongoni mwao, 169 ni raia wa India, 53 wa Uingereza, mmoja wa Canada na 7 wa Ureno.
Kulingana na Kituo cha Udhibiti wa Polisi, ndege hiyo ya Air India yenye nambari ya safari AI 171 ilikuwa ikielekea London nchini Uingereza.
“Mnamo Juni 12, 2025, ndege ya Air India B787 yenye usajili VT-ANB, ikiwa katika safari ya AI-171 kutoka Ahmedabad kwenda Gatwick (London), ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka Ahmedabad,” imesema taarifa ya mamlaka hiyo.
Tayari Kampuni ya Boeing imetoa taarifa kwa Umma ikisema iko tayari kutoa msaada wowote kwa waathiriwa na familia zao kadri itakavyohitajika.
“Kampuni yetu iko pamoja inaomboleza na walioathirika na ajali hii. Imetuumiza sana,” imesema taarifa ya kampuni.
Tayari viongozi mbalimbali wametuma salamu za pole kwa waathiriwa wa ajali hiyo. Miongoni mwao ni Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ambaye ameeleza kupokea taarifa ya ajali hiyo kwa mshtuko mkubwa.
“Kuna janga limetokea Ahmedabad, limetuhuzunisha na kutuumiza. Machozi yetu yanabubujikwa pamoja na familia za walioathiriwa na ajali ya ndege hii,’ ameandika Modi kupitia akaunti yake ya mtandao wa X.
Mbali na Modi, Rais wa Russia Vladimir Putin naye ameandika kuwa; “Natoa salamu za pole kwa Rais wa India Droupadi Murmu na Waziri Mkuu Narendra Modi, tunaomboleza pamoja kufuatia ajali ya hiyo ndege”
“Nitoe pole kwa familia za waliofariki katika ajali hiyo na niwatakie majeruhi kupona kwa haraka,” ameandika.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi wa Ureno, Emidio Sousa amethibitisha raia wake saba kuwemo ndani ya ndege hiyo huku akisema tayari orodha ya watu hao imeshawasilishwa nchini humo.
“Wengi wao wanaonekana kuwa walikuwa na uraia pacha ila ni raia wa Ureno bado tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu,” amesema Sousa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amesema bado anaendelea kupokea taarifa kutoka India kuhusiana na ajali hiyo. Mfalme Charles naye anaendelea kupatiwa mwenendo wa taarifa za tukio hilo.
“Nitoe pole kwa familia ambazo zimepoteza wapendwa wao kwenye ajali hii,” amesema Starmer,
Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi.