Dar es Salaam. Ni nani amewaua wanandoa Antony Ngaboli (46) na Anna Amiri (39)? Hili ni swali linaloulizwa na kila mmoja aliyefika nyumbani kwa wawili hao eneo la Tabata Bonyokwa GK, wilayani Ilala jijini Dar es Salaam kujua chanzo cha kifo chao.
Tukio hilo limetokea usiku wa kumkia leo Alhamisi, Juni 12, 2025 baada ya miili yao kukutwa chumbani kwao ikiwa na majeraha sehemu mbalimbali.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Jumanne Muliro amesema miili ya wanandoa hao imekutwa ndani ya chumba chao cha kulala huku ikiwa na majeraha.

Amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kujua chanzo cha vifo hivyo.
Mwananchi imefika yalipo makazi ya Anthony aliyejulikana pia kama Ally na Anna aliyekuwa na jina la Amiri ambao wote inaelezwa walibadilisha dini kutoka uislamu na kuwa Wakrito ili kujua kinachoendelea na chanzo cha vifo hivyo.
Polisi walikuwapo kuanzia asubuhi wakiendelea na upelelezi kwa kuzungumza na wanafamilia wakiwamo watoto.
Miili yao ikiwa iliondolewa na kupelekwa hospitalini ikisubiri taratibu za uchunguzi na mazishi.
Nyuso za majonzi zikitawala kwa kila mmoja aliyefika eneo hilo, michirizi ya damu ikionekana kutoka ndani.

“Hivi hawa waliowaua hawa watu ni kina nani hasa, kwa nini wametekeleza hili, kweli unawaua wenzako kinyama kiasi hiki,” alisikika mmoja wa waombolezaji akizungumza na wenzake.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Maliya Tabu amesema saa mbili asubuhi alipokea simu kutoka kwa wananchi wakimuarifu kutokea kwa tukio hilo la mauji ya wanandoa.
“Nimepata taarifa ya mauaji haya muda wa saa mbili asubuhi na nikatoa taarifa polisi; ndani ya muda mfupi walifika kufanya uchunguzi na baadaye kuiondoa miili ya marehemu kwa ajili ya hatua nyingine, miili tuliikuta chumbani ikiwa imejeruhiwa,” amesema Tabu.

Jirani na mjumbe wa eneo hilo, Aisha David amesema ni tukio lililowahuzunisha na kutaka mamlaka husika kuchukua hatua.
“Tuna maswali mengi tunajiuliza kuhusu tukio hili, tunaomba uchunguzi wa kina ufanyike na wahusika wachukuliwe hatua,” amesema Aisha
Akisimulia namna alivyobaini kutokea kwa tukio hilo, msaidizi wa kazi za ndani wa familia hiyo, Mariam Said amesema waligundua kutokea kwa tukio hilo baada ya mtoto wa marehemu kugonga kwa muda mrefu chumba cha wazazi wake asubuhi akihitaji nauli ya kwenda ‘tuisheni’ (kwenye masomo ya ziada) bila ya mafanikio.
Amesema baadaye akiwa anafanya usafi nje ya dirisha la wanandoa hao aliona hali iliyomtia shaka baada ya kuona dirisha la wanandoa hao limevunjwa kidogo huku pazia likiwa na madoa mithili ya damu.
“Nilikimbia kumueleza mtoto wao mkubwa ambaye alikimbia kwa haraka kuingia chumbani kwao na kukuta miili yao ikiwa imejeruhiwa,” amesema Mariam.
Amesema baada ya kuwapigia baadhi ya ndugu waliwashauri kutoa taarifa kwa majirani waliowasaidia kutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa.
Mariam amesema awali kabla ya tukio hilo kutokea majira ya saa mbili usiku (jana) wanandoa hao walirudi nyumbani na baada ya kula chakula usiku waliingia ndani kupumzika.

“Baada ya hapo hatukusikia makelele wala kiashiria chochote kibaya hadi asubuhi tulipoiona miili ya dada na kaka ikiwa imejeruhiwa,” amesema Mariam huku akibubujikwa na machozi.
Kilango aliyejitambulisha kwa jina moja, ni mdogo wa marehemu (Antony Ngaboli) amesema alipigiwa simu saa mbili asubuhi na kupewa taarifa kuwa kaka na shemeji yake wameuawa.
“Nilipofika niliona mwili wa shemeji ukiwa umejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili na kaka ukiwa umejeruhiwa maeneo ya moyo,” amesimulia.

Akiwazungumzia marehemu mkazi wa eneo hilo, Ester Jonas amesema walikuwa watu wapole, wacha Mungu waliopenda ushirikiano na majirani.
“Hata shughuli zote za jumuiya tulikuwa tunazifanyia hapa nyumbani kwao, tutawakumbuka namna walivyokuwa na upendo na kila mtu,” amesema Ester.