Njombe. Jeshi la polisi mkoani Njombe limemkamata Yuston Mwangalilwe (22) mkazi wa kijiji cha Ilembula ambaye alitoroka baada ya kufanya tukio la mauaji ya Andrew Kayombo lililotokea Aprili 2 mwaka huu huko wilayani Wanging’ombe.
Katika kipindi Mei mwaka huu jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 217 wakiwa na vielelezo mbalimbali ikiwemo pikipiki moja, televisheni 8, radio 6, spika 2, magodoro 8,kompyuta 1, simu mbalimbali 9, visimbusi na sukari kilo 40.
Hayo yamebainishwa leo Juni 13, 2025 na kamanda wa polisi mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakatika akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya jeshi hilo lililopo mkoani hapa.
Amesema mtuhumiwa huyo alimuita marehemu kwa njia ya simu mwezi Aprili mwaka huu na kumuua kwa kazi ambayo alipewa ili kufanya hivyo ambapo watuhumia wa awali wa tukio hilo walishafikishwa mahakamani.
“Tukikamilisha upelelezi wa shauri hili mtuhumiwa huyu naye atafikishwa mahakamani,” amesema Banga.
Amesema jeshi hilo pia linamshikilia Fisha Mzumala (31) mkulima wa nchi jirani ya Malawi kwa kosa la kuwepo nchini na kufanya biashara ya uvuvi wa samaki katika ziwa la Nyasa bila ya kuwa na kibali na kuwa amekabidhiwa idara ya uhamiaji kwa hatua zingine.
Amesema upande wa usalama barabarani jumla ya madereva 5,125 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali na waliotozwa faini ni 5,119, waliofungiwa leseni ni watatu na waliopewa onyo ni watatu.
Amesema katika kipindi cha mwezi Mei jeshi hilo limefanikiwa kuwafikisha watuhumiwa watano katika mahakama baada ya kupatikana na hatia na vifungo mbalimbali ikiwemo kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na mwingine kifungo cha maisha kwa kosa ubakaji.
Baadhi ya wananchi mkoani Njombe akiwemo Magreth Abely ameomba serikali kuongeza adhabu kwa madereva ambao wanakutwa na makosa ya barabarani ili kupunguza ajali ambazo zinajitokeza kutokana na makosa ya uzembe.
“Hivi karibuni tumesikia ajali zinavyoua watu tena idadi kubwa lakini ukiangalia makosa mengi yana sababishwa na uzembe wa madereva hivyo naona adhabu haitoshi inabidi kuongeza,” amesema Abely.