Bajeti Afrika Mashariki zaongezeka zikilenga maeneo tofauti

Dar es Salaam. Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika Mashariki jana waliwasilisha bajeti za Serikali zao kwa mwaka wa fedha 2025/2026, huku baadhi ya nchi hizo zikikabiliwa na mazingira magumu ya kiuchumi pamoja na mizozo ya kisiasa.

Mawaziri waliowasilisha bajeti hizo Juni 12, 2025 ni Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda ambazo zinazonesha tofauti katika vipaumbele na zikiweka mkazo kwenye vyanzo vipya vya mapato.

Nchi nyingine wanachama kama vile Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Somalia, bado hazijasoma bajeti.

Mwenendo wa bajeti hizo unaonyesha kuongezeka mwaka hadi mwaka, huku Kenya ikiongoza kwa ukubwa wa bajeti kuliko nchi nyingine, ikifuatiwa na Tanzania, Uganda na Rwanda.

Waziri wa Fedha wa Kenya, John Mbadi amewasilisha bajeti ya Dola 33.03 bilioni za Marekani (Sh85.382 trilioni) kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikiweka mkazo zaidi katika hatua za kuongeza mapato ya Serikali.

Serikali ya Kenya inakadiria kukusanya Dola 25.63 bilioni (Sh66.1 trilioni) katika makusanyo ya kawaida huku Dola 7.06 bilioni (Sh18.2 trilioni) zikipatikana kupitia mikopo ya ndani na nje ya nchi.

Wakati mpango wa bajeti ukiwasilishwa bungeni, polisi waliwatawanya waandamanaji katikati ya Jiji la Nairobi kwa kutumia gesi ya kutoa machozi wakati wa maandamano kufuatia kifo tata cha mwalimu na mwanablogu, Albert Ojwang.

Maandamano hayo yaligeuka vurugu baada ya baadhi ya waandamanaji kuchoma magari mawili eneo la Aga Khan, karibu na jengo la Uchumi House na kuharibu mali kadhaa, jambo lililosababisha biashara zilizo karibu kufungwa.

Bajeti ya Tanzania ya mwaka 2025/2026, iliyowasilishwa na Serikali ni ya Sh56.49 trilioni (Dola 21.6 trilioni). Bajeti hii inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani ya Sh40.47 trilioni, misaada Sh1.07 trilioni na mikopo ya Sh14.95 trilioni.

Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri wa fedha, Mwigulu Nchemba alisema kati ya mapato ya ndani yanayotarajiwa, mapato ya kodi ni Sh32.31 trilioni, mapato yasiyo ya kodi ni Sh6.48 trilioni na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Sh1.68 trilioni.

Pia, alisema mikopo inajumuisha Sh6.27 trilioni kutoka vyanzo vya ndani na Sh8.68 trilioni kutoka vyanzo vya nje.

Makadirio ya matumizi ya Serikali ya Sh56.49 trilioni kwa mwaka 2025/26 yanajumuisha: stahiki za watumishi na michango ya pensheni (Serikali Kuu) Sh9.17 trilioni; ununuzi wa bidhaa na huduma Sh5.58 trilioni; malipo ya riba za mikopo Sh6.49 trilioni; na ruzuku kwa taasisi za Serikali, mashirika ya umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa Sh22.17 trilioni.

Pia, Serikali inatarajia kutumia Sh7.72 trilioni kugharamia malipo ya mtaji kwa deni la ndani na nje.

Waziri wa Fedha wa Uganda, Matia Kasaija aliwasilisha bajeti ikiwa imeongezeka kwa asilimia 0.3 kutoka Ush72.1 trilioni katika mwaka wa fedha 2024/25 hadi Ush72.3 trilioni (Dola 20.1 bilioni).

Ongezeko hilo linatokana na msaada wa bajeti ulioongezeka kwa kiasi kidogo, kutoka Ush1.39 trilioni hadi Ush2.08 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 50, pamoja na mikopo ya ndani inayotarajiwa kuongezeka kutoka Ush8.97 trilioni hadi Ush11.38 trilioni,  ongezeko la asilimia 26.9.

Vipaumbele vya bajeti hiyo ya Uganda ni uwekezaji katika shughuli za mafuta na gesi na miradi ya miundombinu kama vile matengenezo ya barabara na madaraja, ukarabati wa reli ya njia ya kawaida (meter gauge railway), ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), pamoja na usafiri wa majini.

Nchini Rwanda, Waziri wa Fedha Yusuf Murangwa aliomba bajeti ya Dola 4.9 bilioni (Sh12.8 trilioni) kwa mwaka wa fedha 2025/26, unaoanza Julai.

Serikali ya Rwanda inatarajia kutumia kiasi cha ziada cha dola 840 milioni (Sh2.19 trilioni) — sawa na ongezeko la asilimia 21 — katika bajeti ya mwaka 2025/26 ya dola 4.9 bilioni, ikilinganishwa na bajeti ya sasa ya 2024/25 ya dola 4.06 bilioni.

Maeneo ya kipaumbele ni pamoja na ujenzi wa uwanja mpya wa ndege huko Bugesera, pamoja na sekta za kilimo, elimu, afya, makazi na uboreshaji wa upatikanaji wa umeme.

Serikali inatarajia kukusanya Dola 2.87 bilioni (Sh10.4 trilioni) kutokana na mapato ya ndani, ambayo ni sawa na asilimia 58 ya bajeti nzima.

Bajeti za mataifa mengine

Wakati hali ya bajeti ya Afrika ikiwa hivyo, bajeti za mataifa mengine barani Afrika, kwa mwaka 2025/26, zinaakisi dhamira ya ukuaji wa uchumi, upanuzi wa miundombinu na maendeleo ya kijamii.

Ugawaji wa bajeti za 2025 unaonyesha uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu, huduma za kijamii na mabadiliko ya kiuchumi kote barani.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), yafuatayo ni mataifa 10 barani Afrika yenye bajeti kubwa kwa mwaka huu.

Kwanza, Afrika Kusini, ikiwa na bajeti ta dola 141.4 bilioni. Nchi hiyo inaongoza kwa bajeti kubwa barani Afrika kwa mwaka 2025, ikiwa na ugawaji wa kuvutia wa dola 141.4 bilioni. Bajeti ya nchi hiyo inaipa kipaumbele miundombinu, huduma za kijamii, na maendeleo ya kiuchumi.

Algeria inafuata kwa karibu ikitenga bajeti ya dola bilioni 126, ikionyesha uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati na ulinzi.

Misri inashika nafasi ya tatu kwa dola 91 bilioni, ikielekeza fedha kwenye elimu, afya na miundombinu ya umma.

Morocco pia inaonekana wazi katika orodha hii, ikiwa na bajeti ya kitaifa ya dola 73 bilioni.

Angola inashika nafasi ya tano na bajeti ya dola 37.847 bilioni, hasa ikichangiwa na mapato yake ya mafuta.

Nigeria, taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, lina bajeti ya dola 36.7 bilioni, likilenga kubadilisha uchumi na miundombinu.

Kenya inafuata na bajeti ya dola 32.65 bilioni, ikipa kipaumbele elimu, afya, na ukuaji wa uchumi. Kama ilivyoelezwa, bajeti hii inazidi kwa mbali bajeti za majirani zake wa Afrika Mashariki, Uganda na Tanzania.

Libya, licha ya changamoto za kisiasa, inaendelea kudumisha bajeti ya dola 26 bilioni.

Ivory Coast na Tunisia zinamalizia orodha ya mataifa 10 bora, zikiwa na bajeti za dola bilioni 25.22 na dola bilioni 25.16 mtawalia, zote zikilenga kukuza utulivu wa kiuchumi na maendeleo.

Bajeti hizi za kitaifa za 2025 zinasisitiza dhamira ya Afrika katika ukuaji wa uchumi, upanuzi wa miundombinu, na maendeleo ya kijamii.

Nchi hizo zinakabiliana na changamoto kama vile mfumuko wa bei, usimamizi wa deni, na kuyumba kwa kisiasa, ugawaji huu wa bajeti utakuwa muhimu katika kuunda mandhari ya kiuchumi ya baadaye ya bara hili.

Related Posts