Imani potofu zinavyosumbua wagonjwa wa kisukari

Dar es Salaam. Kisukari ni ugonjwa sugu unaohitaji uelewa wa kina na usimamizi wa kila siku ili kumwezesha mgonjwa kuishi maisha ya kawaida.

Hata hivyo, katika jamii nyingi, hususan vijijini na maeneo yenye uelewa mdogo wa kiafya, kuna imani potofu zinazozuia wagonjwa kupata matibabu sahihi au kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.

Imani hizi zimekuwa chanzo kikuu cha madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na ulemavu, kifo na kuenea kwa msongo wa mawazo miongoni mwa wagonjwa wa kisukari.

Mojawapo ya imani potofu ni kuwa kisukari husababishwa na kurogwa. Wapo wazazi au ndugu wanaoamini mtoto au kijana aliyegunduliwa na kisukari ameandamwa na nguvu za giza, na hivyo badala ya kumpeleka hospitali, wanampeleka kwa mganga wa kienyeji au kutumia tiba za mitishamba.

Wakati huo huo, kiwango cha sukari huendelea kupanda au kushuka bila kudhibitiwa, hali ambayo husababisha matatizo ya kiafya kama upofu, ugonjwa wa figo, vidonda vya miguu, au hata kupoteza fahamu.

Imani nyingine potofu ni kuwa kisukari huweza kupona kwa kunywa juisi za asili au kufunga kula kabisa kwa siku nyingi.

Ingawa lishe bora ni sehemu muhimu ya usimamizi wa kisukari, uamuzi wa kujitibu bila ushauri wa daktari, unaweza kusababisha hali ya hatari kama vile kuongezeka kwa sukari. Wagonjwa wengi wamejikuta wakipoteza fahamu, wakilazwa hospitali au hata kupoteza maisha kwa sababu ya kuamini kuwa dawa za hospitali hazifai.

Pia kuna dhana potofu kuwa mtu akitumia sindano ya insulini mara moja itamletea ulemavu wa daima, Imani hii huwafanya wagonjwa, hasa watoto na vijana, kukataa kuanza matibabu sahihi, na wengine kuacha kutumia insulin ghafla bila kuruhusiwa na daktari. Matokeo yake ni kuharibika kwa viungo vya mwili hatua kwa hatua.

Imani hizi huambatana na unyanyapaa na wengine huamini kisukari ni laana au adhabu. Wagonjwa hujificha, hukosa kujiamini, na huogopa kueleza hali yao hata kwa waajiri au walimu. Hili husababisha kupungua kwa ufanisi kazini au shuleni, na wakati mwingine mgonjwa hufikia hatua ya kukata tamaa kabisa.

Suluhisho la changamoto hizi ni elimu. Tunahitaji kampeni za mara kwa mara zinazolenga kuondoa imani potofu kuhusu kisukari kwa kutumia lugha rahisi, vielelezo vya maisha halisi, na ushirikishwaji wa viongozi wa dini, waganga wa jadi wanaokubali mabadiliko, pamoja na watoa huduma za afya.

Kadhalika, elimu hii inapaswa kuanzia shuleni hadi kwenye jamii, ikilenga si tu wagonjwa bali hata wale wanaowazunguka, familia, marafiki na jamii kwa ujumla.

Kisukari si laana, wala si ugonjwa unaotokana na ushirikina,  bali ni hali ya kiafya inayodhibitika kwa matibabu na mabadiliko ya mtindo wa maisha.

Related Posts