Mahakama yaidhinisha majeshi ya Trump California

San Francisco. Mahakama ya Rufaa ya Marekani imempa Rais Donald Trump ruhusa ya muda ya kuendelea kuwaweka wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Taifa (National Guard) katika jiji la Los Angeles.

Uamuzi huo unazuia kwa sasa utekelezaji wa agizo la awali la jaji wa Serikali, ambaye alitaka kikosi hicho kirejeshwe chini ya usimamizi wa Gavana wa California, Gavin Newsom.

Hatua hii inakuja wakati mvutano kuhusu mamlaka ya udhibiti wa vikosi hivyo ukiendelea kati ya Serikali ya shirikisho na Serikali ya jimbo.

Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani, Charles R. Breyer, alikuwa ametangaza kuwa Rais Trump alikiuka sheria kwa kupeleka majeshi hayo bila idhini ya Serikali ya jimbo.

Katika hukumu yake, aliandika kuwa Trump “alivuka mipaka ya mamlaka yake kisheria na pia alikiuka Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Marekani,” na akaamuru mamlaka ya kikosi hicho irejeshwe kwa Gavana Newsom.

Ingawa Breyer alisitisha utekelezaji wa agizo hilo hadi saa sita mchana Ijumaa, Serikali ya Trump ilikata rufaa mara moja katika Mahakama ya Rufaa ya Kanda ya Tisa, ambayo ilikubali ombi la serikali na kuahirisha utekelezaji wa hukumu hiyo. Kesi hiyo sasa itasikilizwa Jumanne.

Ofisi ya Gavana Newsom ilipoulizwa kutoa maoni kuhusu uamuzi huo wa mahakama ya rufaa, ilielekeza waandishi kwenye kauli za awali za gavana aliyesema “ana imani na utawala wa sheria.”

Mvutano huu wa kisheria umeibuka kufuatia kesi iliyofunguliwa wiki hii na serikali ya jimbo la California dhidi ya Rais Trump, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth, ikitaka kuweka mipaka kuhusu majukumu ya Walinzi wa Taifa na Majaribio ya Majini (Marines) walioko Los Angeles wakitaka waruhusiwe kulinda tu majengo ya serikali kuu na wafanyakazi wake.

Serikali ya jimbo iliiomba mahakama kuweka zuio la muda kwa shughuli za wanajeshi hao, na kupinga hatua ya Rais kuwatuma bila kushirikisha wala kupata idhini ya Gavana.

Serikali ya Trump iliwaamuru wanajeshi 4,100 wa Walinzi wa Taifa na Majini kuingia Los Angeles kukabiliana na maandamano.

Kati yao, wanajeshi 2,100 wapo katika jiji hilo. Wote ni sehemu ya Task Force 51, ambayo imepewa jukumu la kulinda taasisi na miundombinu ya serikali kuu, kwa mujibu wa taarifa ya Kamandi ya Kaskazini ya Jeshi la Marekani.

Gavana Gavin Newsom, ambaye ni Mdemocrat na mara kwa mara amekuwa kwenye mvutano wa wazi na Rais Trump, amesema kwamba hapingi jukumu la Serikali kuu kulinda mali zake.

Hata hivyo, ameeleza kuwa anapinga matumizi ya vikosi vya kijeshi  kama Marines na Walinzi wa Taifa  kuendesha operesheni za kutekeleza sheria za uhamiaji na sheria nyingine za kiraia mitaani.

Amesisitiza kuwa anachotafuta ni “msaada wa muda ulio makini na unaozingatia athari zisizorekebishika kwa jamii zetu na kwa utawala wa sheria,” iwapo Serikali ya shirikisho itaendelea na mpango huo.

Serikali ya Trump ilijibu ombi la zuio la muda la Gavana Newsom kwa kusema kuwa “halina msingi wowote wa kisheria,” na kwamba utekelezaji wake “utahatarisha usalama wa wafanyakazi wa Idara ya Usalama wa Ndani (DHS) na kuingilia uwezo wa serikali ya shirikisho kufanya kazi zake ipasavyo.”

Katika rufaa yake, Serikali ya Trump iliita agizo la jaji kuwa ni “uvamizi wa kipekee dhidi ya mamlaka ya Rais,” likieleza kwamba linaingilia haki ya kikatiba ya Rais kuhamasisha Walinzi wa Taifa kutoka majimbo mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na ghasia dhidi ya serikali kuu.

“Agizo hili linaweka maofisa wa Serikali kuu katika hatari kubwa kwa kila dakika linapobaki kutumika,” timu ya Trump iliongeza.

Wakati huo huo, viongozi wa Serikali za mitaa wamepinga vikali kauli kutoka mrengo wa kulia wa kisiasa zinazodai kuwa kuna mgogoro mkubwa au vurugu zinazoendelea katika jiji la Los Angeles.

Mwendesha Mashtaka wa Kaunti ya Los Angeles, Nathan Hochman, aliwaambia waandishi wa habari wiki hii kuwa “asilimia 99.99 ya wakazi wa jiji hili hawajafanya kosa lolote kinyume cha sheria kuhusiana na maandamano haya.”

Hukumu ya Jaji Breyer yenye kurasa 36 inakosoa hatua za serikali ya Trump, ambapo aliandika kuwa “kuendelea kuwepo kwa majeshi katika mazingira ya kutozingatia sheria ndani ya Los Angeles kunachochea mvutano zaidi na waandamanaji, hali inayoweza kusababisha machafuko makubwa na hata kupotea kwa maisha ya watu.”

Related Posts