WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inawathamini Watu wenye Ulemavu wakiwemo wenye ualbino na wakati wote itahakikisha inawalinda na kuwapatia fursa stahiki katika ujenzi wa Taifa.
Amesema katika kuendelea kutekeleza mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kutumia mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, hadi kufikia Machi, 2025 tayari shilingi bilioni 5.48 zimetolewa kwa vikundi 891 vya Watu Wenye Ulemavu nchini.
Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa (Juni 13, 2025) wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uelewa kuhusu Ualbino yaliyofanyika katika uwanja wa Mwanga Centre, mkoani Kigoma.
Ameongeza kuwa katika mwaka 2024/2025 kiasi cha ruzuku inayotolewa kwa Vyama vya Watu wenye Ulemavu kimeongezeka hadi kufikia shilingi milioni 230 ikilinganishwa na shilingi milioni 200 zilizotolewa kwa mwaka 2023/2024.

“Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ilitenga shilingi bilioni 8.743 kwa ajili ya huduma za ustawi wa Jamii na shilingi 182. 8 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta kinga ya saratani ya ngozi kwa watu wenye Ualbino.”
Aidha, Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa wahakikishe wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi kwa Watu wenye Ualbino, Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi na Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Taarifa za Watu wenye Ulemavu (PD-MIS) katika ngazi ya Halmashauri.

Amesema kuwa mfumo huo utarahisisha, utaharakisha na utahakikisha usahihi katika usajili wa watu wenye ualbino na ulemavu nchini Tanzania, hususan walioko maeneo ya pembezoni.
“Mfumo huu utapunguza gharama za usafiri na usafirishaji wa vifaa kwa ajili ya usajili, na pia kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi zinazosaidia Serikali kupanga na kutekeleza sera kwa ufanisi,” alisema.

“Pia, Serikali imetoa agizo kwa halmashauri kutoa fedha kwa ajili ya kununua mafuta kinga ambayo imesaidia kupunguza uhaba wa mafuta kinga”
Pia, Godson amewataka watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 2025 “Jitokezeni kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu, mkifanya hivyo mtakuwa mmetimiza haki yenu ya kikatiba ya kuchagua au kuchaguliwa”
Katika Maadhisho hayo Mheshimiwa Majaliwa alizundua Programu janja ya usajili ya wenye ualbino ‘Albino Mobile App’. itakayowezesha kuwasajili na kuwatambua wenye ualbino.