Mapya yaibuka vifo vya wanandoa

Dar es Salaam. Simulizi ya kaka wa Antoni Ngaboli (46) ambaye pamoja na mkewe Anna Amiri (39) walibainika kuuawa wakiwa chumbani, nyumbani kwao Bonyokwa GK wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam imeibua mambo mapya.

Ngaboli na Anna inadaiwa waliuawa usiku wa kuamkia Juni 12, 2025.

“Ilikuwa saa moja asubuhi nilipopokea taarifa kutoka kwa dada yangu akiniambia nyumbani kwa mdogo wangu (Antoni) kuna tukio limetokea na yeye na mkewe wameuawa.

“Nilipigwa butwaa lakini nilivaa ujasiri kama mwanamume nilitaka kuthibitisha nilichoambiwa, nilipanda pikipiki hadi nyumbani kwa marehemu ambako nilishuhudia umati wa watu,” anasimulia Joseph Masoud, kaka wa Antoni alipozungumza na Mwananchi leo Juni 13, 2025 nyumbani kwa marehemu.

Amesema: “Awali sikuruhusiwa kuingia lakini muda mchache baada ya polisi kufika nilijitambulisha kuwa mimi ni kaka wa marehemu waliniruhusu. Nilishuhudia miili ya kaka na shemeji ina majeraha, huku ikivuja damu ndani ya chumba cha kulala.

“Nilishuhudia mwili wa kaka ukiwa na jeraha kubwa upande wa moyo, huku shemeji akiwa na majeraha na amefungwa kitambaa maeneo ya usoni. Funguo za dukani na simu vilikuwa sakafuni, pia kuna kiasi cha fedha kilikuwamo ndani,” amesema.

Amesimulia kuwa polisi waliendelea na uchunguzi, wakifanya mahojiano na watu waliokuwa wakiishi katika nyumba hiyo.

Masoud ameeleza kitendo hicho ni cha kinyama akitaka sheria kuchukua mkondo wake.

Marehemu Antoni Ngaboli na mkewe Anna Amiri enzi za uhai wao



“Serikali ina mkono mrefu natumai haki itapatikana. Kaka na shemeji wamekufa kinyama, wameacha watoto wakiwa wadogo,” amesema huku akibubujikwa machozi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro jana Juni 12, alieleza miili ya wanandoa hao ilikutwa ndani ya chumba chao cha kulala ikiwa na majeraha. Alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendeleaje kujua chanzo cha vifo hivyo.

Katika hatua nyingine, Msemaji wa familia hiyo Nuhu Msangi, ambaye ni baba mdogo wa Antoni amesema wanatarajia maziko yatafanyika Jumatano Juni 18, 2025 wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

“Ibada ya kuwaaga marehemu hawa inatarajiwa kufanyika hapa nyumbani siku ya Jumanne (Juni 17) na kisha kuanza safari ya kwenda Kilimanjaro,” amesema.

Dirisha la chumba cha wanandoa waliokutwa wamefariki wakiwa chumbani kwao katika eneo la Bonyokwa jijini Dar es Salaam.



Amesema wanatarajia kuwazika katika Kijiji cha Ngulu wilaya Mwanga.

Msangi amesema marehemu watazikwa eneo moja kwa kuwa walikuwa wanandoa.

“Kwa mujibu wa mila zetu mwanamke akiolewa anakuwa wa kwetu, hivyo Ally (Antoni) na mkewe watazikwa katika eneo moja,” amesema.

Nyumbani kwa marehemu wamekuwapo waombolezaji na asubuhi walifika askari polisi wanaoendelea na uchunguzi.

Related Posts