Migogoro mitatu inayowatesa wananchi wa Dar

Dar es Salaam. Ndoa, mirathi, ardhi na utapeli, ndiyo migogoro inayotajwa kuusumbua zaidi Mkoa wa Dar es Salaam, huku ukatili wa kijinsia na kingono vikiwa baadhi ya vitendo vilivyoshika kasi katika mkoa huo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kukithiri kwa migogoro na vitendo hivyo, kunachochewa na makundi mbalimbali ya watu waliopo ndani ya jiji hilo.

Kutokana na uhalisia huo, Chalamila amesema Serikali kuanzia Juni 16, 2025 inatarajia kuanza kampeni ya msaada wa kisheria ya Samia ndani ya Dar es Salaam, itakayowezesha utatuzi wa migogoro ya wananchi.

Chalamila ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo, Ijumaa Juni 13, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa kampeni hiyo ya msaada wa kisheria inayotarajiwa kuanza Juni 16, mwaka huu.

Katika kampeni hiyo, amesema wataalamu wa masuala mbalimbali ya kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na sekretarieti ya mkoa huo, watatembelea wilaya zote za Dar es Salaam.

Uzinduzi, amesema utafanyika katika viwanja vya Maturubai, Mbagala jijini humo na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

“Kampeni hii itafanyika kwa siku tisa ndani ya Dar es Salaam, Wilaya na Kata mbalimbali zinatarajiwa kufikiwa na wataalamu wa sheria, lengo ni kuhakikisha migogoro na matatizo yote ya wananchi yatatuliwe,” amesema.

Amewataka wananchi kuhakikisha wanajitokeza wakiwa na ama ushahidi au nyaraka za changamoto zinazowakabili ili kuwezesha kupata msaada wa kisheria haraka.

“Dar es Salaam ni moja ya mikoa yenye takwimu kubwa za matukio ya ukatili wa kijinsia na matarajio yetu ni kwamba wananchi wote wenye matatizo watasikilizwa,” amesema.

Kwa mujibu wa Chalamila, elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria itatolewa katika kampeni hiyo, kadhalika utatuzi wa migogoro ikiwemo ya ndoa, ardhi na mirathi.

“Dar es Salaam Huwa na migogoro mingi hasa ndoa, baba na mama familia ya upande mmoja au vinginevyo na inaibua misuguano na hatimaye ugomvi. Wakati mwingine watu hadi wanauwana,” amesema.

Vitendo vingine alivyovitaja ni utapeli akitolea mfano watu kuuziwa magari yenye kilomita nyingi au chache lakini kiuhalisia haiko hivyo, lakini wapo wanaouziwa magari yaliyoibwa, hivyo kampeni hiyo itasaidia hilo pia.

Amesema ushauri wa kisheria na nasihi utatolewa kuhusu waathirika wa ukatili wa kijinsia hasa ukizingatia Dar es Salaam ina baadhi ya watu wenye tabia za kulawiti na kunyanyasa wanawake au wanaume.

“Wananchi mjitokeze kwa wingi katika huduma hii ya uzinduzi wa kampeni ya kisheria ili kuhakikisha huduma hizi zinawafikia na zitakwenda katika halmashauri zote, wilaya na Kata,” amesema.

Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria wa Wizara ya Katiba na Sheria, Esther Msambazi amesema kampeni ya msaada wa kisheria ya Samia, imeanza mwaka 2023 kwa upande wa Bara na Zanzibar.

Amesema kwa Tanzania Bara mikoa 25 imefikiwa na Zanzibar ni mikoa mitano, huku wananchi zaidi ya milioni mbili wakifikiwa ana kwa ana.

Kwa mujibu wa Esther, migogoro zaidi ya 5,000 imetatuliwa papo hapo kati ya 20,000 iliyowasilishwa kupitia kampeni hiyo.

Related Posts