Mtaalamu wa Video Tabora United asepa

UONGOZI wa Tabora United umeachana rasmi na aliyekuwa mtaalamu wa utathimini wa viwango vya wachezaji na mchambuzi wa video ‘Video Analyst’, Brian David Aswani raia wa Kenya kwa kile kilichoelezwa kuamua kuondoka mwenyewe kikosini humo.

Licha ya uongozi wa Tabora kutotaka kuweka wazi juu ya suala hilo, ila Mwanaspoti linatambua mtaalamu huyo ameondoka kwa kile kinachodaiwa kutolipwa fedha anazodai, ingawa haijawekwa wazi anaidai timu hiyo kiasi gani hadi alipoamua kuondoka.

Mtu wa karibu na mtaalamu huyo aliliambia Mwanaspoti, Brian aliondoka kutokana na kutoliwa mshahara kwa takribani miezi minne na kikosi hicho, hivyo akaamua kujiweka pembeni huku akishinikiza alipwe stahiki zake ili aweze kurudi kwao Kenya.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Charles Obiny ambaye pia ni raia wa Kenya, alipoulizwa kuhusu suala hilo la mtaalamu huyo kuondoka, hakutaka kuzungumza chochote, japo Mwanaspoti linatambua wamefikia makubaliano ya kuachana naye.

Brian aliyejiunga na Tabora United kuanzia Agosti 2024, hadi alipoamua kujiweka kando Mei 31, 2025, amewahi kufanya kazi sehemu mbalimbali za kwao Kenya ikiwemo, Kariobangi Sharks FC akiwa benchi la ufundi na kocha wa timu ya vijana (U-20).

Brian alianza kufanya kazi na Wakenya wenzake, makocha, Francis Kimanzi na msaidizi wake, Yusuf Chippo waliojiunga rasmi na timu hiyo, Julai 31, 2024, kisha kuondoka Oktoba 21, 2024, kutokana na kilichoelezwa mwenendo mbaya wa Ligi Kuu Bara.

Related Posts