Ahmedabad, India. Dada wawili waliokuwa wakisafiri kwenda kumtembelea bibi yao kwa ajili ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika ajali ya ndege ya Air India.
Dhir na Heer Baxi, wote wakiwa katika umri wa miaka ishirini na kitu, walitoka majumbani kwao London, Uingereza, na kuelekea Ahmedabad kwa ziara ya ghafla ambayo hawakuipanga hapo awali.
Walikuwa wakirejea nyumbani na ndipo ndege waliyoipanda ilidondoka na kulipuka kwa moto sekunde chache baada ya kupaa chini ya dakika moja tangu kuondoka ardhini.
Familia na marafiki wa marehemu hao wamesema maisha yao yamebadilika, wakieleza kwa majonzi kuwa “kila kitu kimefutika” baada ya vifo vya vipaji hivi vichanga vilivyokuwa vikiibuka.
Dhir, mbunifu wa mavazi, alihitimu mwaka 2024 kutoka shule ya sanaa na ubunifu ya ‘Parsons Paris’ kwa Shahada ya Sanaa ya Ubunifu wa Mavazi (Bachelor of Fine Arts in Fashion Design).
Heer, dada yake, alihitimu kutoka Chuo cha Barnard taasisi ya elimu huria inayohusiana na Chuo Kikuu cha Columbia ambako alisomea uchumi pamoja na lugha na tamaduni za Asia ya Mashariki, na baadaye akaanza kufanya kazi mjini London.
Heer alikuwa kiongozi wa miradi katika sekta ya uwekezaji na nishati mbadala, na pia alihudumu kama kiongozi wa tawi la London la ‘Columbia Venture Community’.
Kabla ya kurejea Ulaya, alifanya kazi katika miji ya Hong Kong na Singapore ambako inaaminika kuwa ndipo walikulia.
Katika maonyesho yake ya mwisho ya ubunifu chuoni, Dhir alitengeneza mkusanyiko wa mavazi ya kufikirika ya wanawake wa mafia, yaliyochochewa na simulizi halisi zilizomo kwenye kitabu ‘Mafia Queens of Mumbai – Stories of Women From the Ganglands’.
Wasifu wake wa Instagram uliandikwa “Paris and London”, ukiwa umejaa picha za mavazi aliyobuni, zilizopigwa kwa ushirikiano na wabunifu na wapiga picha mbalimbali.
Familia yake imesema kuwa alikuwa akigawanya muda wake kati ya Paris na London, na alikuwa karibu kurejea tena Paris kwa ajili ya onyesho la mavazi mapya.
Kaka yao mkubwa, Ishan Baxi, aliliambia gazeti la The Telegraph la Uingereza: “Siwezi kueleza kile ambacho familia yetu nzima inapitia kwa sasa tupo katika hali ya kustuka, hatujakubaliana wala kuelewa kilichotokea. Hilo ndilo naweza kusema kwa sasa.”
Aliendelea kwa kusema: “Wote wawili walikuwa na hulka ya kusaidia kwa moyo wa dhati, na walizingatia sana maadili ya kifamilia.
Walikuwa na ndoto za kufanikisha maisha yao hadi kufikia hatua ya kuweza kuzunguka duniani kwa uhuru bila mashaka. Wakiwa pamoja na wazazi wetu, walikuwa na mtazamo wa kupokea maendeleo ya kisasa bila kuachana na mizizi yao ya kitamaduni.
“Dada zangu walikuwa watu wa maadili thabiti; walijua kipi ni sahihi na kipi siyo. Ndiyo maana kila walichokifanya iwe katika taaluma au kwenye ubunifu walikifanya kwa mafanikio na kwa amani, bila mivutano wala migongano na wenzao au wakubwa wao.”
Katika chapisho la mwisho la Heer kwenye Instagram, lililowekwa Novemba 2024, mtu mmoja aliandika maoni Alhamisi jioni: “Pumzika kwa amani, kipaji kichanga,” sambamba na picha ya mwanamitindo aliyekuwa amevalia mojawapo ya mavazi ya Dhir, akiwa amepambwa na ‘gajra’ shada la maua la kitamaduni – kichwani mwake.