Othman ataka machungu ya historia ya Zanzibar yaandikwe

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ameeleza wajibu na umuhimu wa kuandika historia ya kweli ya Zanzibar, hata ikiwa ina matamu na machungu.

Amesema historia ya nchi haipaswi kuandikwa kwa ‘kalamu ya kisiasa’, bali inapaswa kuandikwa kwa kuzingatia misingi ya haki na ukweli, kwa maslahi ya vizazi vyote vya sasa na vijavyo.

Othman ameeleza hayo leo Juni 13, 2025, aliposhiriki hafla ya maadhimisho ya kumbukumbu ya kusitishwa kwa biashara ya utumwa, iliyoandaliwa na Kanisa la Anglikana Mkunazini, Mji Mkongwe Mkoa wa Mjini- Magharibi, Unguja akimwakilisha Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud akisalimiana na Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania, Fabian Mndolwa wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya kusitishwa kwa biashara ya utumwa katika kanisa la Anglikana Mkunazini Zanzibar



Tukio hilo ni mwendelezo wa Ibada Maalumu ya kuadhimisha miaka 152 tangu tamko la kukomesha biashara ya utumwa Zanzibar na duniani kote.

Kwa Zanzibar tamko hilo lilitangazwa rasmi Juni 6, 1873, katika eneo mashuhuri lilipo sasa Kanisa la Anglikana, ambalo limo katika urithi wa kudunia chini ya Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco).

“Historia ni mapito ya matukio ya kweli, hivyo ni vyema kuiandika kwa kuzingatia yote, matamu na machungu, ili kusaidia kuleta mazingatio na mabadiliko, kwa vizazi vya sasa na baadaye,” amesema.

Amesema maazimio haya yana lengo la kuwakumbusha binadamu madhila na madhara ya utumwa na biashara ya utumwa ulioendeshwa katika karne kadhaa kabla ya kuanza kupigwa marufuku kuanzia karne ya 19.

“Maadhimisho ya kukomeshwa na kukumbukwa kwa biashara ya utumwa duniani, hayapo hapa Zanzibar pekee, bali ni katika nchi mbalimbali ulimwenguni. Miongoni mwa nchi hizo ni Ghana na Senegal na nyingine nyingi barani Afrika,” amesema

Tangu Juni 6 mwaka jana, Serikali imeanza kuweka kumbukumbu za sekta ya utalii na mambo ya kale kuhusu tukio hili, ambapo mwaka huu imeendelea kuiadhimisha siku hii kwa pamoja.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud akizungumza aliposhiriki hafla ya maadhimisho ya kumbukumbu ya kusitishwa kwa biashara ya utumwa, iliyoandaliwa na Kanisa la Anglikana Mkunazini, Mji Mkongwe Mkoa wa Mjini- Magharibi, Unguja.



“Moja ya mafanikio muhimu ya ushirikiano baina ya Serikali na Kanisa la Anglikana ni uhifadhi na uendelezaji wa makumbusho yetu na hasa katika historia ya biashara ya utumwa ambapo hatua hii imeongeza wigo wa nafasi ya nchi katika midahalo ya kitaifa na kimataifa na hususan juu ya historia yetu hii katika Afrika Mashariki,” amesema.

Amesema kupitia hatua hiyo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla imekuwa mnufaika kimataifa, ambapo hivi karibuni Tanzania imekuwa ikishirikiana zaidi na wadau mbalimbali wa maendeleo, pamoja na kupata fursa ya kushiriki katika michakato ya kimataifa ya urejeshaji wa malikale.

“Hatua hii pia imewezesha kuongezeka kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za utafiti wa kiakiolojia, kijiolojia na kihistoria katika shughuli za binadamu wa awali hapa Zanzibar, walioishi karne nyingi zilizopita,” amesema.

Faida nyingine ni kufanya ukarabati wa majengo ya kihistoria, kuimarisha nafasi ya Zanzibar katika orodha ya miji ya urithi wa kihistoria na kuendeleza sekta hii kwa kushirikiana na sekta binafsi katika uhifadhi na uendelezaji wa makumbusho.

Ameeleza kuwa Serikali kupitia Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale imeanza jitihada ya kuweka kwenye kumbukumbu sehemu walizopita watumwa kuwa ni sehemu maalumu za kihistoria Unguja na Pemba.

Vilevile, kwa msaada wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, kimetungwa kitabu cha kumbukumbu ya historia ya utumwa Zanzibar kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

“Serikali ya Oman imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi na ukarabati wa makumbusho ya Kihistoria, ikiwemo makaburi ya watawala wa zamani Zanzibar na jengo la Beit-al -Ajaib, ‘People’s Palace’ na Kibweni Palace.

Amesema maadhimisho haya yanatoa fursa za midahalo, taaluma, tafiti na maelewano, na kuchukua hatua za pamoja za kuhakikisha maeneo muhimu ya historia ya nchi yanatunzwa, kuendelezwa na kuwa sehemu ya vivutio vya utalii na urithi.

Waziri wa Utalii na Mambo Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga amepongeza hatua ya kuichagua Zanzibar kuwa mahala pa maadhimisho ya siku ya kutokomeza biashara ya utumwa duniani.

Waziri Soraga amesema maadhimisho hayo yamelenga pia kutumia fursa ya kuutangaza utalii wa nchi pamoja na kuweka mkazo kwamba madhila yaliyopatikana katika historia ya biashara hiyo, yasitokee tena.

Naye, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Fabian Mndolwa amesema Kanisa na Taasisi nyingine zikiwemo za Serikali ya Zanzibar, wanaadhimisha siku hii ikiwa ni sehemu ya kuiombea nchi na pia biashara ya mateso waliyokuwa wakiyapata binadamu, kwamba yasijirejee tena.

Kiongozi huyo ambaye ameeleza hatua ya Kanisa lake kuzitaka mamlaka ambazo ni pamoja na za Kimisheni na Serikali ya Uingereza kuomba radhi kutokana na hila na madhila waliyotenda dhidi ya binadamu, kupitia biashara ya utumwa.

Ametoa wito wa kukomesha aina zote za dhulma ikiwa ni pamoja na biashara ya utumikishaji wa binadamu kwa kivuli cha ahadi za ajira nje ya nchi, ukoloni wa lugha unaoendeleza ung’ang’anizi wa kufundishia lugha ya kikoloni ya Kiingereza.

“Jambo lingine ni huu utumwa wa kiimani; tutambue kwamba utumwa wowote ni dhambi; na dhambi ni uasi,” amesema Askofu.

Mawaziri wa Fedha wa Afrika Mashariki wamewasilisha bajeti kuu za Serikali zao kwa mwaka wa fedha 2025/26, huku wakikabiliwa na mazingira magumu ya kiuchumi pamoja na mizozo ya kisiasa duniani na katika kanda.

Nchi zilizowasilisha bajeti zao Juni 12, 2025 ni Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda zinazonesha tofauti katika vipaumbele huku zikiweka mkazo kwenye vyanzo vipya vya mapato.

Mwenendo wa bajeti hizo unaonesha kuongezeka mwaka hadi mwaka, huku Kenya ikiwa na bajeti kubwa kuliko nchi nyingine za Afrika Mashariki, ikifuatiwa na Tanzania, Uganda na Rwanda.

Related Posts