Ahmedabad, India. Familia ya watu watatu kutoka Gloucester, waliopoteza maisha katika ajali ya ndege ya Air India, wametajwa kuwa watu waliopendwa na kuheshimiwa, kwa mujibu wa taarifa ya jamaa zao iliyotolewa kupitia kwa Imamu wao.
Waliofariki ni baba Akeel Nanabawa, mkewe Hannaa Vorajee, na binti yao wa miaka minne, Sara Nanabawa.
Inafahamika kuwa Nanabawa, ambaye alikuliwa Newport nchini Uingereza, alikuwa akirejea nyumbani kwake Gloucestershire akiwa na familia yake baada ya safari nchini India.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi aliyosoma Sara, Abdullah Samad, amesema kwamba mtoto huyo alikuwa “mwanga wa tumaini” darasani ambaye “ameangaza kila kona ya darasa kwa furaha yake.”
Wazazi wake walifahamika sana katika jamii kutokana na moyo wao wa kujitolea na matendo ya hisani.
“Waligusa maisha ya watu wengi, na wengi watawahisi sana,” amesema Samad katika mahojiano na BBC.
“Walishiriki katika harambee za kuchangisha fedha kwa ajili ya misaada ya kibinadamu Gaza, pamoja na kugharamia matibabu kwa watu wasiojiweza nchini India. Haya yalikuwa sehemu ya huduma yao kwa jamii.”
Wanandoa hao waliendesha biashara ya huduma za nje ya kampuni, ‘Iceberg’, yenye ofisi zake mjini Gloucester na Ahmedabad.
Vorajee pia alikuwa Mkurugenzi wa shirika la ‘Peace Inclusion’, taasisi ya kijamii inayojihusisha na kujenga maelewano baina ya jamii mbalimbali na kukuza uelewa wa dini ya Kiislamu kupitia elimu.
Kiongozi mmoja wa jamii ambaye amekuwa karibu na familia hiyo alisema: “Katika kipindi hiki cha huzuni isiyoelezeka, mioyo yetu ipo pamoja na wale wote waliobaki.
“Hakuna maneno yanayoweza kufuta uchungu wa pigo hili kubwa, lakini tunaomba familia ipate faraja kutokana na wingi wa upendo, mshikamano, na huruma kutoka kwa jamii mbalimbali duniani kote.”
“Kumbukumbu zao za upendo na huduma kwa wengine ziwe faraja kwa waliobaki. Na roho zao zipumzike kwa amani ya milele.”