Mwanza. ‘Bila mafuta, gari haliwezi kuendeshwa, vivyo hivyo bila damu, mwili hauwezi kufanya kazi’ ndivyo unavyoweza kuelezea umuhimu wa damu katika mwili na maisha ya mwanadamu.
Watalaamu wa afya wanasema bila damu hakuna usafirishaji wa hewa ya oksijeni na virutubisho mwilini wala kuratibu wa mfumo wa kinga mwilini, ili kupambana na maambukizi mbalimbali ya magonjwa pamoja na kudhibiti joto.
Hapa nchini matumizi ya damu yanatajwa kuwa makubwa hasa kwa kundi la wajawazito wanaopoteza damu wakati wa kujifungua, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, waathirika wa ajali za barabarani na wagonjwa wa saratani.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kukusanywa idadi ya chupa za damu ambazo ni sawa na asilimia moja ya idadi ya wananchi waliopo kwenye nchi au eneo husika, hivyo mahitaji ya damu nchini yanakadiriwa kuwa chupa 610,000, kwani Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inaonyesha kuna Watanzania zaidi ya milioni 61.
Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha asilimia 87ya wachangia damu ni wanaume na asilimia 54 ni vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 29, huku chupa moja ya damu inayochangiwa ikiwa inaweza kugusa na kuokoa maisha ya watu hadi watatu, kwa kutengeneza mazao ya damu aina tatu ambayo ni chembe nyekundu, chembe sahani na plasma (sehemu ya majimaji ya damu).
Kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, mwanamke anaweza kuchangia damu kila baada ya miezi minne na mwanamume anaweza kuchangia kila baada ya miezi mitatu.
Hata hivyo ili watu hawa wachangie, wanalazimika kuwa na umri usiopungua miaka 18 na usiozidi miaka 65, uzito usiopungua kilo 50
Aidha, mwanamke asiwe mjamzito au anaenyonyesha, asiwe na maradhi ya muda mrefu kama shinikizo la damu, kisukari, kifafa, pumu na mengineyo.
Vigezo vingine mchangiaji awe mzima wa afya njema na asiwe na homa, asiwe na mienendo hatarishi ya kupata maambukizi ya magonjwa kama homa ya ini pamoja na Ukimwi.
Wizara ya Afya nchini inasema damu inaweza kuokoa maisha ya kina mama kwa zaidi ya asilimia 28.2, hutumika kwenye idara ya upasuaji kwa zaidi ya asilimia 23.2 na idara ya watoto kwa asilimia 19.2, hivyo upatikanaji wa damu unatajwa kuwa nguzo muhimu katika kupunguza vifo vya kina mama vinavyotokana na magonjwa, uzazi na kujifungua.
“Faida za kuchangia damu zipo sana kwenye kusaidia wagonjwa na hiyo ndiyo faida kubwa sababu unapochangia damu, unamwangalia mgonjwa ambaye ndiye mhitaji mkubwa wa damu wakiwemo wajawazito na watoto wenye selimundu ambao mara kwa mara wanapungukiwa damu, majeruhi wa ajali wakiwemo bodaboda,,,’’ anasema mtaalamu wa maabara kitengo cha damu salama katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora-Kitete, Mwasara Abubakari.
Kwa mhusika mwenyewe anayechangia damu mara kwa mara, anapata manufaa ya kupata uchunguzi wa afya yake bila malipo, kwani mchangiaji hulazimika kupima mapigo ya moyo, shinikizo la damu, kiwango cha damu, Ukimwi, kaswende, homa ya ini na kundi la lake la damu
“Jamii mara nyingi haijaipa check ups (upimaji afya) kipaumbele, kwahiyo unapochangia damu kuna uwezekano mkubwa wa kutambua afya yako japo sio lengo la uchangiaji,”anasema Mwasara.
Aidha, anasema baada ya kuchangia damu, mwili huanza kuzalisha damu mpya kwa haraka, jambo ambalo huimarisha mfumo wa damu na kufanya mwili kuwa na damu safi na yenye afya.
Boresha afya yako kwa kuchangia
Uchangiaji damu unatajwa kuwa na manufaa kedekede kwa mhusika ikiwamo kupunguza kiwango cha chuma mwilini. Mwili unapokuwa na kiwango kikubwa cha madini ya chuma, kuna hatari ya kupata matatizo ya moyo na ini.
Kuchangia damu mara kwa mara husaidia kupunguza kiwango hiki, hivyo kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa yanayohusiana na ziada ya chuma mwilini.
Kuchangamsha uzalishaji wa seli mpya za damu: Baada ya kuchangia damu, mwili huanza mchakato wa kutengeneza seli mpya ili kuchukua nafasi ya damu iliyopotea. Mchakato huu huufanya mfumo wa damu kuwa mpya na wenye afya, na huongeza ufanisi wa kusafirisha oksijeni mwilini.
Utafiti unaonyesha kuwa watu wanaochangia damu mara kwa mara wana uwezekano mdogo wa kupatwa na magonjwa ya moyo. Hii inatokana na kupungua kwa msongamano wa damu na viwango vya chuma, ambavyo vinaweza kusababisha mshtuko wa moyo au kiharusi.
Aidha, uchangiaji damu huambatana na hisia za furaha na kuridhika kwa kuwa unajua umeokoa maisha ya mtu mwingine. Kitendo hiki cha huruma husaidia kupunguza msongo wa mawazo na huongeza hali ya kiakili na kihisia.
Wapo wanaodhani uchangiaji wa damu ni jambo lisilofaa kwa kuwa lina madhara. Wapo wanaokimbia kuchangia wakihisi wakipimwa watagundulika kuwa na magonjwa mbalimbali.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Zabron Masatu anasema hakuna madhara yoyote kwa mtu anayechangia damu kama ambavyo baadhi ya watu wanavyoamini.
“Hakuna madhara na ndio maana kuna vigezo ukionekana umetimiza vigezo hivyo basi unakuwa huru kuchangia damu na unapofanya hivyo hakuna madhara yoyote. Wapo watu wanadai kuwa ukichangia utakuwa unaishiwa damu hii sio kweli kwani damu ina tabia ya kujiongeza,” anaeleza.
Kwa upande wake, Mwasira anasema kuna baadhi ya watu wanaaminisha wenzao mitaani kuwa mtu akichangia damu, mwili unatengeneza damu nyingi kitu ambacho siyo kweli, akieleza kiutaratibu mwili hurudisha damu kwa kiwango kile kile kilichotolewa.
‘’Tukisema ana damu nyingi..mwili unatengeneza damu nyingi ina maana hapo kuna tatizo lazima amuone daktari siyo kwamba tatizo limechangiwa na uchangiaji damu. Hapana amuone daktari labda mfumo wake wa utengenezaji damu una shida,’’ anasema.
Kwa mujibu wa Mwongozo wa Tathmini na Uteuzi wa Wachangia Damu, mtu anayechangia damu kwa malipo ya pesa au zawadi nyingine, hubeba hatari kubwa ya maambukizi yanayoweza kuambukizwa kupitia uhamishaji damu, uchangiaji ambao haukubaliki kimaadili na haupendekezwi nchini.
Hata hivyo, mwongozo huo umeruhusi mtu kuchangia damu yake mwenyewe, ili ihifadhiwe kwa ajili ya kuitumia katika upasuaji wake.
Mkazi wa jijini Mwanza, Saleh Mrisho anasema licha ya kusikia tetesi mbalimbali ikiwemo kutakiwa kutoa damu mara kwa mara endapo atachangia, aliamua kuchangia damu kwa mara ya kwanza kwenye kampeni ya damu salama katika Hospitali ya Bugando bila kupata athari yoyote.
“Nilielezwa faida ya kuchangia damu hasa katika kuokoa maisha ya watu, nikachangia lakini sikupata madhara yoyote. Hadi leo nimeshachangia damu mara nne haijajaa wala siumwi kichwa, nipo kawaida kama nilivyokuwa,”anasema Mrisho.
Kuchangia damu si tu tendo la huruma bali pia lina manufaa ya moja kwa moja kwa afya ya mchangiaji. Ni njia rahisi, salama, na ya haraka ya kusaidia jamii huku ukiboresha afya yako binafsi.
Inashauriwa watu wenye afya nzuri wachangie damu mara kwa mara, ili kuendelea kuokoa maisha na kujinufaisha kiafya.
Uchangiaji damu na saratani
Kwa mujibu wa utafiti, watu wanaochangia damu mara kwa mara, wanajiweka katika nafasi nzuri ya kutoshambuliwa na saratani ya damu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochaposhwa na tovuti ya BBC Swahili, watu wanaochangia damu mara nyingi wana uwezekano mkubwa wa kuwa na mabadiliko ya vinasaba katika damu yao, hali ambayo watafiti wanasema inaweza ma
kupunguza hatari ya kupata ugonjwa huo tishio.
Taarifa inaeleza watafiti kutoka Taasisi ya Francis Crick, walilinganisha damu ya makundi mawili ya wanaume wenye afya njema walio katika miaka yao ya 60, huku kundi la kwanza likiwa ni la wale waliochangia damu mara tatu kwa mwaka kwa miaka 40, kundi jingine ni wale waliochangia damu mara tano katika maisha yao.
Watafiti walisema watu wanapochangia damu, seli zilizopo kwenye uboho yaani ndani ya mifupa, hutengeneza seli mpya za damu ili kuziba pengo la damu iliyopotea, mchakato huo unaweza kusababisha mabadiliko ya maumbile ya vinasaba katika uboho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watafiti waligundua kiwango cha mabadiliko ya vinasaba katika damu ya kundi la watu 217, waliochangia damu mara kwa mara na kundi la pili la watu 212 waliochangia damu mara tano tu katika maisha yao.
Iligundulika mabadiliko hayo katika seli za uboho yalikuwa tofauti. Asilimia 50 ilikuwa kwa waliochangia damu mara kwa mara na 30 kwa waliochangia damu mara chache.
“Ni aina ya mabadiliko ambayo hupunguza hatari ya kupata saratani ya damu,” anasema mtafiti, Dk Hector Huerga Encabo,kama alivyonukuliwa na tovuti hiyo.