Vigogo wa Chadema Dodoma wapandishwa kizimbani

Dodoma. Viongozi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Dodoma Mjini wamefikishwa mahakamani leo na kusomewa shtaka moja la kutishia kufanya fujo.

Washtakiwa hao ambao wanawakilishwa na wakili wa kujitegemea, Fred Kalonga ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Stephen Karashan, Katibu wa Chadema Wilaya ya Dodoma mjini, Azizi Abbas na Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Wiliam Keiya.

Wote watatu wamesomewa shtaka hilo la kutishia kufanya fujo na kuhamasisha maandamano yasiyo na kibali baada ya kukamilikankwa mkutano wa hadhara wa chama hicho Juni 8, 2025 mbele ya hakimu Mkazi wa mahakama ya hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule.

Hata hivyo, washtakiwa wote watatu walikana mashtaka hayo ambapo walitakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini mali yenye thamani ya Sh5 milioni kila mmoja na wanatakiwa kuwa wakazi wa Dodoma.

Washtakiwa wote watatu walikamilisha masharti ya dhamana na waliachiwa huru kwa dhamana ambapo hakimu Mpangule aliwataka wadhamini hao kuhakikisha washtakiwa wanafika mahakamani kila siku ya kesi yao bila kukosa hadi itakapokwisha.

“Mkishindwa kuwasimmia washtakiwa kufika mahakamani kila siku ya kesi yao mali zenu mlizoandika kama dhamana zitauzwa na kama hazitakuwa na thamani ya Sh 5 milioni au zitaharibika mtafungwa kifungo cha miezi sita,” amesema Mpangule.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 27, 2025 itakapokuja kusikilizwa hoja za awali.

Related Posts