Wabunge walia na utajiri kwa wageni, umasikini kwa wazawa

Dodoma. Wakati pato halisi la Taifa lilifikia Sh156.6 trilioni mwaka 2024 kutoka Sh148.5 trilioni mwaka uliotangulia, wabunge wameonyesha hofu juu ya hali ya kukua kwa uchumi wa Tanzania huku ukuaji huo ukiwa hauakisi moja kwa moja pato la Mtanzania mmoja.

Katika mdahalo wa uchambuzi wa bajeti kwa wabunge uliowakutanisha wabunge na wataalam wa mipango leo Ijumaa Juni 13, 2025, baadhi ya wabunge wamesema licha ya kuelezwa kuwa uchumi unakuwa, lakini hauko katika uhalisia wa pato la mtu mmoja mmoja.

Tatizo lingine linalotajwa ni riba kubwa zinazokopeshwa na mabenki kwamba hazisaidii watu kukua kiuchumi na hivyo Tanzania kushindwa kuzalisha mabilionea.

Mawasilisho ya mjadala huo yalitolewa na Wizara ya Fedha, pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo iliwakilishwa na Lusajo Mwaikemwa na mtaalamu kutoka Tume ya Mipango Dk Fred Msemwa.

Mbunge wa kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya amehoji hilo pato la Taifa lipo wapi ikiwa wananchi wanaendelea kuwa masikini na huku fedha zao zikiendelea kwenda nje ya nchi.

“Ni lazima tutafsiri hilo pato la Taifa lipo kwa nani, tunapoongea kuhusu pato hilo ni muhimu tukawaangalia Watanzania ni wangapi wanamiliki hilo pato,” amehoji Profesa Manya.

Mbunge huyo amesema kuwa katika miradi mingi ambayo inajengwa na kuonyesa kuwa pato limekuwa ikiwemo miradi aliyoita inafanya kazi ya maji, bado wakandarasi wanaochukua fedha nyingi ni wageni kutoka nje ya nchi hivyo fedha zinapelekwa kwa wageni.

Profesa Manya ametolea mfano mwingine wa maduka ya Super Market ambayo nayo bidhaa zinazouzwa ndani ni za kutoka mataifa ya ng’ambo hivyo nako fedha zinapelekwa kwa wageni wakati kuna bidhaa za Watanzania zinazidi kuozea ndani.

Mbunge wa Kahama, Jumanne Kishimba amesema utajiri unaotengenezwa wote unapelekwa nje lakini akaeleza mashaka kuhusu masuala ya utafiti kwa kuwa kuna vitu vinafanyika bila utaratibu kutokana na kutokuwepo kwa utafiti mzuri.

Hoja yake ya utafiti imeungwa mkono na Mbunge wa kuteuliwa, Dk Bashiru Ally ambaye amesema kinacholikosesha Taifa kuwafikisha wananchi kwenye malengo ni kutokuwa na bajeti ya utafiti wa masuala muhimu.

Dk Bashiru amesema uwekezaji katika utafiti umekuwa ni mdogo kwani asilimia moja inayotengwa kwa ajili ya utafiti haitoshi hivyo mambo mengi yaendelea kufanyika bila kuwa na uhalisia kwa kutofanyiwa utafiti kabla.

Mbunge huyo ameshauri wakati mwingine inapofanyika mijadala kama hiyo, lazima wawepo wataalamu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na watu wa Wizara ya Fedha ili wawaeleze wabunge kuhusu vipaumbele.

Mbunge mwingine wa Kuteuliwa Shamsi Vuai Nahodha ametaja riba kubwa za ukopeshaji kutoka kwa mabenki ndiyo kikwazo kwani wanakopesha kwa gharama kubwa hivyo wanaozalisha bidhaa wanaweka bei za juu ambazo haziendani na uchumi huku wageni wakipata mikopo ya riba nafuu katika mataifa yao ndiyo maana bidhaa zao zinauzwa kwa bei ya chini.

Waziri Kiongozi huyo mstaafu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pia amehoji kuna ugumu gani wa kuzalisha bidhaa katika kiwanda cha viwatilifu cha Kibaha ambacho hata kwenye bajeti ya Waziri wa fedha hakukitaja.

Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei akisisitiza vipaumbele katika bajeti za Elimu, Maji na Afya kwa kuwa zinagusa maisha ya watu wa chini huku Mbunge wa viti Maalumu, Benadetha Mushashu akitaja sababu ya kutokua uchumi ni mikopo ya riba kubwa ambayo inatolewa na mabenki.

Akijibu hoja za Nahodha, Waziri wa Mipango Profesa Kitila Mkumbo amejibu kuhusu kiwanda cha viwatilifu Kibaha akisema kwa sasa kiwanda hicho kinamilikiwa moja kwa moja na Watanzania baada ya Serikali ya Cuba kujiondoa.

Profesa Mkumbo ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maagizo na tayari Wizara ya Tamisemi imetenga katika bajeti yake fedha za kununua madawa kutoka katika kiwanda hicho kwa ajili ya kuua mazalia ya mbu ili kutokomeza ugonjwa wa maralia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza amesema kinachowakimbiza wawekezaji hata kuwafanya wasiwe wengi licha ya fursa zilizopo ni utitiri wa kodi ambao pia unapelekea bidhaa zinazozalishwa kuuzwa kwa bei ya juu.

Njeza amesema kama kodi itapungua kwenye uwekezaji, bidhaa zitauzwa kwa bei ya chini lakini wawekezaji watakuwa wengi wa kutosha.

Related Posts