Unguja. Siku moja baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwasilisha bajeti kuu kwa mwaka wa fedha 2025/2026, wataalamu na wananchi wametoa maoni tofauti kuhusu mpango huo wa kifedha.
Baadhi wameipongeza bajeti hiyo wakieleza kuwa imegusa sekta mbalimbali muhimu kama elimu, afya, miundombinu na kilimo, jambo linaloashiria dhamira ya Serikali kuimarisha ustawi wa wananchi na kukuza uchumi wa Zanzibar.
Hata hivyo, kuna kundi jingine la wachambuzi na wananchi walioonyesha wasiwasi kuhusu baadhi ya maeneo ya bajeti hiyo, wakibainisha kuwa yapo mapungufu hasa katika eneo la kodi na ushuru ambayo yanaweza kuongeza gharama za maisha.
Wanaonya kuwa ongezeko la kodi kwenye bidhaa za msingi huenda likaathiri uwezo wa wananchi wa kipato cha chini na kusababisha ugumu wa maisha badala ya kupunguza makali ya hali ya uchumi kama ilivyokusudiwa.
Maoni hayo yametokana na hotuba ya bajeti ya SMZ iliyowasilishwa jana Alhamisi Juni 12, 2025, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha na Mipango), Dk Saada Mkuya Salum, ambapo aliliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha jumla ya Sh6.9 trilioni kwa ajili ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Maombi hayo yamelenga kuongeza mapato ya ndani, kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti matumizi ya shisha na vileo vingine vyenye madhara, kuwalinda vijana dhidi ya athari za ulevi, pamoja na kuimarisha viwanda vya ndani na kukuza ajira kwa wananchi.
Hata hivyo, gazeti hili limezungumza na wataalamu wa maendeleo na wananchi ambapo baadhi yao wameonyesha uimara wa bajeti na wengine wamebainisha mapungufu yaliyomo.
Balozi wa Heshima wa Brazil visiwani Zanzibar, Abdulsamad Abdulrahim amesema kuwa bajeti hiyo imeonyesha mwelekeo mzuri unaoendana na mpango mkakati wa Zanzibar wa kufikia ukuaji endelevu wa uchumi na maendeleo ya kijamii.
Ameongeza kuwa utekelezaji mzuri wa bajeti hiyo, pamoja na kushughulikia kwa ufanisi masuala yaliyoangaziwa, utakuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha malengo yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Bajeti ya ukweli na inasisitiza kuwawezesha vjana, wanawake na watu wenye mahitaji maalumu pamoja uhifadhi wa mazingira na juhudi za kupunguza mabadiliko ya tabianchi ambayo ni nzuri sana katika nafasi ya sasa ya ulimwengu,” amesema.
Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya jamii na siasa, Ali Makame, ametofautiana na maoni ya Abdulrahim kwa kusisitiza kuwa tatizo halipo kwenye kupandishwa kwa ushuru wa bidhaa, bali ni katika utekelezaji.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa iko kwa baadhi ya watendaji wa Serikali ambao wanashindwa kusimamia kwa ufanisi ukusanyaji wa mapato, jambo linalokwamisha utekelezaji wa bajeti kwa ufanisi unaotarajiwa.
Kwa mtazamo wake, zaidi ya asilimia 70 ya kodi inapotea kutokana na kukosekana kwa mfumo madhubuti wa ukusanyaji wa mapato, hali inayochochea mianya ya upotevu wa fedha kupitia mikono ya watu wasio waaminifu.
“Kila mwaka kuna vitu vinapandishwa bei, lakini hiyo sio suluhu kwa sababu unapopandisha kodi kwenye bidhaa anayeumia sio mfanyabiashara bali anaumia mwananchi wa hali ya chini,” amesema na kuongeza;
“Kwa mfano mtu anaongeza kodi ya maji ya kunywa wakati huohuo mnapambana na unywaji maji safi na salama ili kuepusha magonjwa sasa kama hakuna hayo maji mwananchi atakunywa nini au ndio mnawaambia wanywe yoyote yale halafu wakaugue,” amesema Makame.
Hoja ya Makame kuhusu maji imeibuka kufuatia pendekezo la Serikali kutoza kodi ya miundombinu kwa kiwango cha Sh50 kwa kila lita moja ya maji safi na salama yanayoingizwa Zanzibar.
Lengo la hatua hiyo ni kuchangia katika Mfuko wa Maji, ili kusaidia kuboresha na kuimarisha huduma za upatikanaji wa maji visiwani humo.
“Unazuia peremende, biskuti, vitu ambavyo vinapendwa na watoto; je, mnataka wafurahie nini?” Hiyo ilikuwa hoja nyingine ya Makame, akiikosoa SMZ kufuatia pendekezo lake la kutoza ushuru wa Sh1,000 kwa kila kilo ya peremende, biskuti na chokleti zinazoingizwa visiwani.
Hoja ya Serikali imelenga kupunguza matumizi ya bidhaa hizo kutokana na athari zake kiafya, hasa kwa watoto wadogo.
Hata hivyo, Makame ameonyesha wasiwasi kuwa hatua hiyo inaweza kuwa kikwazo kwa furaha ya watoto na kwamba suluhisho bora lingeweza kupatikana kupitia elimu ya lishe badala ya ushuru mkubwa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Zanzibar, Biubwa Omar Khamis amesema kuwa licha ya mapendekezo ya bajeti kuonyesha nia ya kuzingatia usawa wa kijinsia, bado kuna maeneo muhimu hasa katika sekta ya biashara ambayo yamepuuzwa.
Mwenyekiti huyo amesema ingawa bajeti inaonyesha dhamira ya kuinua uchumi wa wananchi kupitia mikopo, mfumo wa sasa wa mikopo ya vikundi haunufaishi wengi.
Ameeleza kuwa ndani ya kikundi cha watu watano, si wote huwa na malengo yanayofanana, jambo linalokwamisha mafanikio ya pamoja.
Mwenyekiti huyo amesema baadhi ya wafanyabiashara wanakumbana na masharti magumu ya kupata mikopo, ikiwemo kutakiwa kuwa na dhamana wakati bado wanaanzisha biashara.
Pia, ameikosoa bajeti kwa kutoweka mkazo wa moja kwa moja katika kuwasaidia wafanyabiashara kwenye masoko na sekta ya utalii, hasa wale wanaotaka kushiriki maonyesho ya kimataifa.
Amebainisha kuwa baadhi ya kampuni zaidi ya 400 zinazotoa huduma za utalii hazijasajiliwa rasmi na hazina ofisi zinazoeleweka, hali inayoathiri mapato ya Serikali.
Mwenyekiti huyo ameitaka Serikali kuboresha usimamizi wa mifumo ya kodi na kuhakikisha usawa katika uendeshaji wa biashara.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Dk Salama Yussuf ameonyesha umuhimu wa kodi kwamba ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya taifa kwani zinachangia katika uboreshaji wa miundombinu kama barabara, maji na huduma za afya, mradi tu zitatungwa na kutekelezwa kwa njia rafiki kwa wananchi na wawekezaji.
Amesema kwamba hali hiyo imeanza kuonekana wazi kupitia jitihada za Serikali zilizopo sasa.
Dk Yussuf ameeleza kuwa iwapo mazingira ya kodi yatavutia wawekezaji na biashara kukua, ajira kwa wananchi zitaongezeka, kipato kitaimarika katika kaya, na hivyo kupunguza kiwango cha umasikini kwa sababu mzunguko wa uchumi utaongezeka.
“Kodi zikilipwa ipasavyo, Serikali itaweza kujitegemea na kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Mfano mzuri ni jinsi barabara zimeboreshwa—leo hii ukitaka kwenda sehemu yoyote ni rahisi, na yote hayo yanatokana na mapato ya kodi,” amesema Dk Salama.
Kwa upande wake mfanyabiashara Karama Juma amesema kuwa hatua ya SMZ kushirikisha sekta binafsi katika mipango ya maendeleo ni ya kupongezwa, kwani Serikali pekee haiwezi kuendesha uchumi bila ushirikiano na sekta hiyo.
“Duniani kote hakuna Serikali inayoweza kuendesha uchumi wake bila kushirikiana na sekta binafsi. Nchi zilizofanikiwa kiuchumi zimewekeza katika mazingira rafiki kwa sekta binafsi. Kwa upande wetu, kupitia bajeti hii, tumeona ishara njema ya kuwahusisha wadau wa sekta binafsi,” amesema Karama.
Ameongeza kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuisaidia Serikali kuinua uchumi wa nchi kupitia uwekezaji, ajira na teknolojia.
“Kuna sera za uwekezaji ambazo zinaonekana zitaimarika na kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuja nchini,” ameongeza.
Kwa upande wake, mdau wa sekta ya usafirishaji, Hussein Haji Abdulla, ameeleza wasiwasi wake kuhusu pendekezo la kupandisha bei ya mafuta ya petroli na dizeli, akisema hatua hiyo italeta mzigo kwa wananchi, hasa kupitia ongezeko la nauli za usafiri wa umma.
Hoja ya Abdulla inatokana na pendekezo la SMZ la kufanya marekebisho ya viwango vya tozo ya leseni ya barabara na tozo la kuendeleza barabara kwa kuongeza tozo ya leseni ya barabara kutoka Sh38 hadi Sh100 kwa uingizaji wa lita moja ya mafuta ya dizeli na petroli.
Pia, SMZ imeongeza tozo ya kuendeleza barabara kutoka Sh100 hadi Sh200 kwa uingizaji wa lita moja ya mafuta ya dizeli na petroli. Hatua hizi zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh35.75 bilioni fedha zake zitatumika katika kuboresha miundombinu ya barabara.