Chumi apokea hati za utambulisho za Mwakilishi Mkazi wa AKDN nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mwakilishi Mkazi mpya wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) nchini Tanzania, Amin Mawji.

Hafla hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam jana, Juni 13, 2025 ambapo Chumi alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Akizungumza baada ya kupokea hati hizo, Chumi amempongeza Mawji kwa uteuzi na kumhakikishia ushirikiano kutoka kwa Serikali ya Tanzania wakati wa kutekeleza majukumu yake mapya.

Aidha, ameipongeza AKDN kwa mchango wake nchini katika maeneo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

“AKDN imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo nchini. Tumeshuhudia kazi zenu katika kupunguza umaskini, kuimarisha elimu, kutoa huduma bora za afya na kuhifadhi urithi wa kitamaduni Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema Chumi.


Kwa upande wake, Mawji ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa uhusiano mzuri na utekelezaji wa mafanikio ya miradi ya AKDN.

Ameahidi kuendeleza ushirikiano huo, hasa katika maeneo ya mapambano dhidi ya saratani katika ukanda wa Afrika Mashariki, utafiti wa mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya mazingira, kwa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu ndani na nje ya nchi, zikiwemo za Canada na Ujerumani.

Mawji anachukua nafasi ya Amin Kurji, ambaye anamaliza muda wake wa kuhudumu kama nchini Tanzania.

AKDN ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali linalojishughulisha na miradi ya maendeleo endelevu kwa lengo la kuboresha maisha ya watu, bila kujali dini, rangi au jinsia, hasa barani Asia na Afrika.

Tangu kuanza shughuli zake nchini Tanzania mwaka 1991, AKDN imekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya, elimu, maendeleo ya jamii na utamaduni.

Related Posts