Moshi. Aliyekuwa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Godfrey Malisa ameibukia kwenye mkutano wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) huku akisema hawezi kubaki nyuma katika kupigania mdororo wa demokrasia nchini.
Dk Malisa alivuliwa uanachama wa CCM, Februari 10,2025 na kugeuka gumzo kwa tuhuma za kukiuka katiba na maadili ya chama hicho taarifa iliyotolewa na katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Mercy Mollel.
Hatua ya kufukuzwa Malisa ilitokana na kauli zake ambazo amekuwa akizitoa, kupinga maamuzi ya mkutano mkuu wa chama hicho Taifa uliofanyika Januari 19, 2025 akidai uamuzi wa kupitisha mgombea urais wa chama hicho ulikiuka katiba ya chama hicho.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kumalizika mkutano wa C4C, uliofanyika Juni 13, 2025 Moshi Mjini, Dk Malisa amesema suala la mdororo wa demokrasia nchini ni janga ndani ya CCM na nje ya chama hicho, kulimaliza hilo jamii haipaswi kuwa na woga katika kukabiliana nalo.
“Tatizo kubwa tulilonalo Tanzania ni ukosefu wa demokrasia na shida hiyo si ya CCM pake yake hata huku nje kwa vyama vya upinzani hakuna demokrasia na hao waliopasuka kutoka Chadema kuja Chaumma ni mivurugano ya demokrasia ndani ya chama.
“Kelele yangu kubwa ni kudai haki na demokrasia ya kweli na hata hapa ningesimama ningesema jambo hilohilo hatuwezi kwenda kokote bila kupigania demokrasia,” amesema.
Dk Malisa aliyekuwa amekaa jukwaa kuu la viongozi wa Chaumma, amesema: “Nchi hii haiwezi kubadilika kama tunaogopa kutekwa, nimepiga kelele muda wote huu wananishangaa kuniona…” amesema.
Alipoulizwa anataka kujiunga na Chaumma kiasi cha kupanda kwenye jukwaa la chama hicho amesema: “Mimi bado ni kada wa CCM nitaendelea kubaki hiyo wala sijafukuzwa na hii hainizuii kuja kuzungumzia madai ya demokrasia ya kweli huku Chaumma.”