Dk Mwinyi aridhishwa na kazi inayofanywa na makandarasi wazawa

Unguja. Ili kufikia lengo lililokusudiwa la kuanzishwa Taasisi ya Wahandisi, Wasanifu na Wakadiriaji majenzi Zanzibar (IAESZ), Serikali imetoa wito kwa wahandisi kujisajili katika taasisi hiyo ili kuunganisha nguvu za pamoja na kufikiwa na fursa zinapojitokeza.

Serikali imesema kuwa tasisi hiyo itawasaidia wazawa na Watanzania katika masuala ya usanifu na ukadiriaji wa miundombinu inayotekelezwa nchini.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Juni 14, 2025 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla wakati akifungua mkutano wa pili wa IASEZ uliofanyika Mjini Unguja.

Dk Mwinyi amesema Serikali zote mbili zinathamini mchango unaotolewa na taasisi hizo ili kutekeleza miradi mikubwa ya kimaendeleo kwa kuwapa nafasi makandarasi wazawa.

Amesema Serikali ina mipango mingi ya kimaendeleo inayohitaji ujuzi wa miundombinu mbalimbali ikiwamo ujenzi wa majengo ya kisasa, barabara, maji na umeme na vyote vinahitaji ujuzi.

“Serikali inahitaji makandarasi wazawa kutumia ujuzi wao katika kutekeleza miradi  hiyo kwa kushirikiana ikiwa na lengo la kuwajaengea uwezo wataalamu wetu kujiajiri na kuwajengea imani kutumika na wawekezaji wanaokuja kuwekeza nchini,” amesema Dk Mwinyi. 

Pia, Dk Mwinyi amewasihi makandarasi hao kutumia taratibu zinazowekwa ili kuepusha majanga yanayoweza kujitokeza na Serikali itaendelea kuthamini michango ya tasisi hizi na kuahidi kutoa nafasi kwa wazawa kuliko wageni.

“Katika miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kati ya miradi hiyo mingi imetekelezwa na wazawa kwa viwango vivyoridhisha na hiyo ni ishara ya kuthibitisha uwezo wao,” amesema Dk Mwinyi. 

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohammed amesema shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo ni uhai, kwani ikitokea wamekosea wanaweza kusababisha maafa makubwa.

Ameseme taasisi hiyo ni muhimu kwa uhai wa watu na wamefanya kazi katika kusimamia viwango na maadili kwa uadilifu, kukadiria gharama za miundombinu na kutoa mafunzo.

“Nchi yetu inapiga hatua hasa katika sekta ya ujenzi, mchango wa maendeleo hayo yanatokana na  wahandishi ambao wazawa,” amesema Dk Khalid.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla akishuhudia utiaji wa saini hati ya makubaliano ya kufanya kazi kwa kushirikiana kati ya Taasisi ya wasanifu, wahandisi na wakadiriaji majenzi Zanzibar na Taasisi ya Warka Water 
kwenye Mkutano wa Pili wa Taasisi ya (IAESZ).



Kwa upande wa Rais wa  IAESZ, Abdul Samad  Mattar amesema katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, imefanikiwa kuwa na ushirikiano kutoka taasisi mbalimbali na kutoa misaada ili kuendeleza taasisi hiyo.

Pia, amesema taasisi hiyo inalenga kusajili wananchama 500 kutoka kisiwani hapa, hivyo ametoa wito kwa wadau.

Related Posts