Dar es Salaam. Serikali imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi katika kesi ya jinai inayowakabili wanafunzi watatu wa vyuo vikuu, likiwemo la kusababisha madhara ya kimwili, bado unaendelea.
Wanafunzi hao ni Mary Matogolo (22) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ryner Mkwawili wa Chuo Kikuu Ardhi, na Asha Juma wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA).
Wote wanakabiliwa na jumla ya mashtaka manane, yakiwemo ya kula njama kutenda kosa, kusambaza taarifa za uongo, kusababisha madhara makubwa, kuharibu mali na kutishia kumuua mwanafunzi mwenzao.

Mshtakiwa Ryner Ponci Mkwawili, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi Dar es Salaam na Asha Suleiman Juma, wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu, Dar es Salaam (TIA), wakiwa wameficha nyuso zao, wakati wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi yao ya kumdhalilisha mwanafunzi mwenzao kuahirishwa. Picha na Hadija Jumanne
Wakili wa Serikali, Erick Kamala, aliieleza mahakama jana Ijumaa, Juni 13, 2025, kuwa kesi hiyo ilikuwa imepangwa kwa ajili ya kutajwa, lakini uchunguzi wake bado haujakamilika. Hivyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 14, 2025 itakapotajwa tena.
Katika tukio lisilo la kawaida, mara baada ya kesi yao kuitwa na kuingia mahakamani, washtakiwa hao walionekana kutojua taratibu za mahakama na kwa pamoja waliwaamkia watu waliokuwa ndani ya ukumbi kwa kusema “shikamoo”.
Tukio hilo lilizua mshangao miongoni mwa waliokuwepo mahakamani, kwani ni kinyume na utaratibu wa kimahakama kutoa salamu au kuzungumza bila ruhusa ya hakimu.
Hata hivyo, salamu hiyo haikuitikiwa, ilionyesha washtakiwa hao ni wageni katika mazingira ya mahakama.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote watatu wanadaiwa kuwa Machi 16, 2025 katika eneo la Sinza, Wilaya ya Ubungo, walikula njama ya kuchapisha taarifa za uongo kwa lengo la kuharibu heshima ya mtu mwingine.
Shtaka la pili linawahusu Mary na Asha, ambapo wanadaiwa kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa WhatsApp, zenye ujumbe: “Toa sauti umefanya mapenzi na Mwijaku lini na wapi.”
Shtaka la tatu linamkabili Ryner pekee kwa kusambaza taarifa hizo hizo kupitia mtandao huohuo.
Shtaka la nne linamkabili Mary pekee kwa madai ya kumshambulia Magnificati Kimario kwa kumpiga kichwani kwa chuma na kumsababishia maumivu makali.
Katika shtaka la tano, washtakiwa wote wanadaiwa kumvuta nywele binti huyo na kumsababishia madhara ya kimwili.
Shtaka la sita na la saba linamhusu Mary pekee, ambapo anadaiwa kuharibu laini ya simu na simu ya mkononi aina ya Samsung yenye thamani ya Sh700,000, mali ya Magnificati.
Shtaka la nane linawahusu washtakiwa wote, wakidaiwa kumtishia kumuua Magnificati kwa kutumia kisu katika tukio hilo hilo la Machi 16, 2025.