Lori lililoanguka lazua foleni Mikumi usiku kucha

Mikumi. Abiria wa mabasi na watumiaji wengine wa vyombo vya moto wamekwama katikati ya Mbuga ya Mikumi, Barabara ya Morogoro – Iringa kwa zaidi ya saa saba kutokana na lori kuanguka barabarani.

Foleni ilianza saa saba usiku wa kuamkia leo Juni 14, 2025 hadi alfajiri, kukiwa na magari zaidi ya 100 yaliyokwama, abiria na madereva wakiwa ndani wakihofia usalama wao kutokana na eneo hilo kuwa na wanayamapori.

Polisi wa kituo cha ukaguzi Mikumi walitoa tahadhari kwa madereva na abiria kutoshuka kwenye magari.

Dereva wa gari linalosafirishwa kwenda nje ya nchi (IT), Jackson Mwakyembe amesema anakwenda Zambia lakini kutokana na foleni ana hofu ya kwenda kutozwa faini kwa kuchelewa kulifikisha kwa mhusika.

“Hii foleni imetuumiza, tumekaa hapa tangu jana (Juni 13) mpaka asubuhi hii hatujasogea. Mahali hapa ni hatari anaweza kutokea simba au tembo, sisi wenye magari madogo ndiyo tuko kwenye hatari zaidi,” amesema.

Hassan Juma, dereva wa gari linalofanya safari kati ya Mikumi na Kidatu aliyekwama eneo hilo, amesema leo Juni 14, 2025  alfajiri amekutana na foleni hiyo.




“Wakati natoka Kidatu nilipigiwa simu na madereva wenzangu wakaniambia kuna foleni kubwa Mikumi, hata hivyo niliendelea na safari hadi kufika hapa nimekwama sijui foleni hii inasababushwa na nini maana imeanzia mbali siwezi kuona,” amesema.

Nestory Kiungo, abiria aliyekuwa akisafiri kwenda Iringa kwa ajili ya maziko ya ndugu yake yanayofanyika leo Juni 14 amesema hana tumaini la kuwahi.

“Taarifa ya msiba nimeipata jana (Juni 13) na hawa watoto wa marehemu wanatakiwa kufika kwa wakati lakini hali tuliyokutana nayo hapa Mikumi imetuvunja moyo, hatuoni kama tunaweza kufika mapema leo na kuwahi mazishi,” amesema.

Baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakielekea Dar es Salaam kufuata au kupeleka bidhaa wamesema hawajawahi kukubiliana na foleni ya aina hiyo.

“Nimebeba vitunguu na ndizi napeleka Dar es Salaam kutokana na na foleni hii kama hatutapata msaada naweza kupata hasara kubwa bidhaa zitaharibika,” amesema Yusuph Matiku.

Akizungumzia foleni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka amesema foleni imesababishwa na ajali ya lori ambalo lilianguka katikati ya barabara na kuzuia magari kupita.

Shaka amesema ametoa maelekezo kwa mkuu wa kikosi cha usalama barabarani wilayani humo kuhakikisha lori hilo linaondolewa haraka kuwezesha barabara kupitika.

“Foleni hii imeanza usiku na mpaka asubuhi ya leo bado barabara ilikuwa haijafunguka. Kwa muda huu (saa tano mchana) tayari askari polisi wapo eneo la tukio wanajitahidi kupitisha magari upande mmoja wa barabara, naamini mpaka kufikia mchana barabara itakuwa inapitika na lori litakuwa limeshasogezwa,” amesema.


Shaka amewapa pole watumiaji wa barabara hiyo kwa changamoto hiyo inayoendelea kutatuliwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema licha ya lori kuanguka na kuzuia barabara pia kumekuwa na ukaguzi na ufuatiliaji wa mwenendo wa madereva ambao umesababisha foleni.

Related Posts