Msalala: Maambukizi ya Malaria yapungua, sababu zatajwa

Shinyanga. Upuliziaji dawa za kuua mazalia ya mbu umechangia kushuka kwa maambukizi  ya Malaria,  Halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, kutoka asilimia 34 mwaka 2021 hadi asilimia 15.9 mwaka 2024, ikipungua kwa asilimia 18.1 ndani ya kipindi hicho.

Mratibu wa Malaria wa Halmashauri ya Msalala, Dk Martine Mazigwa ametoa takwimu hizo leo Juni 14, 2025, wakati akizungumza na gazeti la Mwananchi baada ya kumalizika kwa tathmini ya kampeni ya unyunyiziaji dawa za kuua mbu majumbani (IRS) katika halmashauri hiyo.

Amesema kampeni hiyo ya kitaifa inayolenga kutokomeza mazalia ya mbu waenezao Malaria, imeleta mafanikio katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo, kufuatia utoaji wa elimu kwa wananchi pamoja na unyunyiziaji wa dawa kwenye kuta za nyumba na maeneo ya mazalia ya mbu.

“Tulianza  kwa kutoa elimu  katika jamii na kufuatiwa na unyunyiziaji katika mazalia yote ya mbu. Dawa hii haina madhara kwa binadamu, mimea na mifugo pia, kwani yenyewe inaua viluilui wa mbu tu katika hatua ya lava.

“Mwaka 2021 wakati tunaanza shughuli hii kiwango cha maambukizi ya Malaria kilikuwa asilimia 34, mwaka 2022 asilimia 25.1, mwaka 2023 ilikuwa ni asilimia 19.5 na mwaka 2024 asilimia 15.9. Matarajio yetu ni kufikia kauli mbiu ya zero Malaria ifikapo 2030,” amesema.

Amesema katika Kata ya Bulyanhulu, kaya 24,902 zimepuliziwa dawa hizo za ukoko; na wataalamu wa upuliziaji wanaendelea ili kuvifikia vijiji vinne vyenye kaya 14,902 vilivyosalia, katika kata hiyo.

Amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wakati wote wa shughuli hiyo ili kutokomeza Malaria pamoja na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Sambamba na hilo Dk Mazigwa amewataka wananchi kusafisha maeneo yao, ikiwa ni pamoja na kufukia mabwawa ya maji  hatarishi yanayotajwa kuwa chanzo cha mazalia ya mbu waenezao Malaria, hususani yale yaliyokuwa yanatumiwa na wachimba madini ya ujenzi.

Kijana Ramadhani Nyanda akipulizia dawa ya ukoko kwenye kuta za nyumba ya mmoja wa wakazi wa kata ya Bulyanhulu Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga. Picha na Amina Mbwambo



“Tumeshapokea dawa zote kutoka serikalini awamu ya kwanza tumepuliza katika Kata ya Bugarama na sasa tumehamia Kata ya Bulyanhulu. Tunatarajia kukamilisha ifikapo Juni 28 2025, na tunataka kutokomeza mbu na mazalia yake.

“Desemba 2024 tulipokea lita 3,655 ya dawa za kuangamiza mazalia ya mbu, kutoka Wizara ya Afya,  kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu 354 yaliyobainika   katika Halmashauri ya Msalala,” amesema.

Mtekelezaji wa upuliziaji dawa za ukoko katika Halmashauri ya Msalala, Gerald Kubanda amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalamu wanaofika katika maeneo yao kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.

“Tuna vijana zaidi ya 400 wanaotekeleza zoezi hili kwa bidii kubwa, tayari tumeanza kuona matokeo chanya. Vita yetu ni dhidi ya mbu waenezao Malaria, na tumejidhatiti kuhakikisha tunatokomeza ugonjwa huu katika Halmashauri ya Msalala,” amesema Kubanda.

Elizabeth Bundala, mkazi wa Kijiji cha Bulyanhulu ameeleza mafanikio ya zoezi hilo, akisema tangu nyumba yake ipuliziwe dawa, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa.

“Awali, kila mwezi watoto wangu walikuwa wanaugua Malaria, lakini tangu kupuliziwa dawa za ukoko, hatujaona mbu na hakuna aliyeugua tena. Tunapongeza Serikali kwa hatua hii,” amesema.

Benard Ruhinda, mkazi mwingine wa kata hiyo, ameishukuru Serikali kwa jitihada hizo na kuomba zoezi hilo liwe endelevu ili kuhakikisha Malaria inatokomezwa kabisa.

Kwa mujibu wa taarifa, zoezi hilo limekamilika kwa awamu ya kwanza katika kata za Bugarama na Bulyanhulu, zaidi ya kaya 50,000 zimefikiwa.

Lengo kuu ni kutokomeza mazalia ya mbu waenezao Malaria kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kufikia Malaria sifuri ifikapo 2030.

Related Posts