Netanyahu azindua operesheni ya ‘Simba anayeamka’ dhidi ya Iran

Mashariki ya Kati. Ni vita vya wazi. Ndivyo hali inavyoonekana baada ya Iran, usiku wa jana, kurusha makombora ya masafa marefu kuelekea Tel Aviv, Israel na kusababisha vifo vya watu watatu huku wengine saba wakijeruhiwa.

Mashambulizi hayo yametajwa kuwa hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya shambulio la ghafla lililofanywa na Israel mjini Tehran, ambapo watu 78 waliuawa, wakiwamo makamanda waandamizi wa Jeshi la Iran na zaidi ya watu 320 kujeruhiwa.

Pia, katika mashambulizi hayo ya Israel, viongozi wakuu wa kijeshi wa Iran waliuawa na maeneo zaidi ya 100 ya kimkakati yalilengwa, ikiwa ni pamoja na vituo vya uboreshaji wa urani na maghala ya makombora.

Hali hiyo imezidi kupandisha joto la mvutano kati ya mataifa hayo mawili, huku hatari ya kuibuka kwa vita kamili ikionekana kuwa karibu zaidi kuliko wakati wowote ule.

Taarifa kutoka Tel Aviv zinaeleza kuwa, Hospitali ya Beilinson imethibitisha kuwa mwanamke mmoja amefariki dunia kufuatia shambulio la kombora la Iran na hivyo kufanya jumla ya waliopoteza maisha kufikia watatu.

Hospitali hiyo pia iliwahudumia watu saba walioumia katika shambulio hilo lililotokea alfajiri ya Jumamosi.

Kwa mujibu wa huduma za zimamoto na uokoaji za Israel, kombora hilo lilianguka na kugonga jengo moja katika jiji hilo.

Huduma ya uokoaji ya Israel, Magen David Adom, imeripoti kuwa kombora la Iran lilianguka karibu na makazi ya watu katikati mwa Israel Jumamosi na kusababisha vifo vya watu wawili pamoja na kuwajeruhi wengine 19. Nyumba nne ziliharibiwa.

Iran usiku wa Jumamosi ilirusha mfululizo wa makombora ya masafa marefu kuelekea Israel kulipiza kisasi kwa mashambulizi dhidi ya maeneo yake ya nyuklia huku Benjamin Netanyahu akionya kwa msimamo mkali kuwa “mengine yanakuja.”

Kwa mujibu wa ‘The Guardian’, makombora ya Iran yalipiga maeneo ya makazi katika pwani ya kati ya Israel na kuua watu watatu, wakiwamo mwanamke wa miaka 60 na mwanamume wa miaka 45.

Takribani watu wengine 34 wamejeruhiwa usiku wa kuamkia leo, wengi wao wakiwa na majeraha madogo, huku watu wawili zaidi wakiuawa leo asubuhi katika shambulio la moja kwa moja katikati ya Israel.

Katika Mji wa Tel Aviv, mlio wa ving’ora ulisikika usiku mzima huku wakazi wakikimbilia kwenye hifadhi za dharura.

 Saa 3 usiku, makombora ya ‘Arrow’ ya ulinzi wa anga yalifyatuliwa, yakizua milipuko angani na kutawanya vipande vya chuma vilivyodondoka kwenye majengo ya ghorofa, mojawapo likipiga jengo la makazi na kusababisha uharibifu mkubwa.

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Khamenei, alitoa tishio la kutisha kwa raia wa Tel Aviv, akiapa “kuleta mapigo mazito” na kuihusisha Israel moja kwa moja na kuanzisha vita.

Marejeo ya video za kushtua yanaonesha mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel, ‘Iron Dome’, ukizuia baadhi ya makombora juu ya anga ya jiji hilo, lakini mengine yalifanikiwa kupenya, likiwamo kombora moja lililolipua upande wa jengo, huku taarifa zikieleza kuwa watu walikuwa wamekwama ndani.

Huduma za dharura za Israel zimeripoti kuwa angalau watu 34 katika eneo la Gush Dan, yaani maeneo ya Jiji la Tel Aviv na vitongoji vyake, walijeruhiwa katika mashambulizi ya usiku wa jana, wakiwamo mwanamke mmoja aliyejeruhiwa vibaya sana na mwanamume mmoja aliye katika hali mahututi.

Iran ilidai kuwa, ilirusha mamia ya makombora, lakini Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisisitiza kuwa makombora yaliyovurumishwa yalikuwa chini ya 100, mengi yalinaswa angani au yalianguka kabla ya kufika walikokusudiwa.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliahidi kuwa mashambulizi zaidi yanakuja, na kuongeza kuwa utawala huo haujui kilichowapiga, wala kitakachowapiga.

Makombora yalipokuwa yakianguka kwa saa kadhaa juu ya Tel Aviv, Netanyahu aliwahimiza raia wa Iran kuinuka na kuuondoa ‘utawala mwovu na wa kimabavu’ wa Tehran, huku mvutano katika Mashariki ya Kati ukiendelea kupamba moto.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa alitangaza kuwa watu 78 wameuawa na 320 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel.

Baada ya Netanyahu kutoa onyo la mashambulizi zaidi, shirika la habari la Tasnim la Iran (ambalo ni la Serikali) lilichapisha video inayoonesha moto mkubwa ukiteketeza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mehrabad, mjini Tehran. Video hiyo inaonesha moshi mzito ukipaa angani usiku.

Awamu ya pili ya mashambulizi ya makombora kutoka Iran ililenga Mji wa Yerusalemu Jumamosi asubuhi, kwa mujibu wa jeshi la Israel  na mashuhuda waliripoti milipuko juu ya mji huo wa kale.

Tehran ilikuwa tayari imeahidi kisasi cha maumivu makali kufuatia shambulio la usiku wa kuamkia leo la Israel ambalo halijawahi kushuhudiwa, na ambalo limeiweka kanda yote katika hatari kubwa ya kuingia vitani kwa mapana.

Waizraeli walikimbilia kwenye maeneo ya kujihifadhi huku ving’ora vya tahadhari vikilia usiku kucha na Jeshi la Israel likithibitisha kuwa mifumo yao ya ulinzi ilikuwa ikifanya kazi kuzuia tishio hilo.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer na Rais wa Marekani Donald Trump wamezungumza jioni hii (jana) kuhusu umuhimu wa diplomasia na mazungumzo katika kutatua mgogoro huo, kwa mujibu wa taarifa kutoka Downing Street.

Inasemekana Marekani ilisaidia Israel jioni hii (jana) katika kuzuia makombora hayo, huku Pentagon ikihamisha majeshi ya wanamaji karibu na pwani ya Israel katika siku za karibuni.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel, Avichay Adraee, alisema: “Utawala wa Iran ulirusha chini ya makombora 100 kwa awamu mbili kuelekea Israel.

“Makombora mengi yalizuiwa angani au yalianguka kabla ya kufika. Majengo machache yaliharibiwa, mengine kutokana na vipande vya makombora yaliyolipuliwa angani.”

Watu wawili wanaripotiwa kuwa katika hali mahututi, huku wagonjwa 18 wakipokea matibabu katika hospitali ya Ichilov, mjini Tel Aviv.

Wengine 15 wanahudumiwa katika hospitali ya Sheba, mjini Ramat Gan, wakiwamo mgonjwa mmoja aliye katika hali mbaya sana.

Wagonjwa wengine saba wanatibiwa katika Hospitali ya Beilinson, huko Petah Tikva, pamoja na mgonjwa mwingine aliyekuwa mahututi.

Shambulio la usiku wa jana lilikuwa kilele cha miaka ya utafiti na mipango ya jeshi la Israel pamoja na shirika la ujasusi la Mossad, likiwa na lengo la kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia.

Israel ilitumia ndege za kivita na kituo cha siri cha droni kilicho karibu na Tehran kushambulia vikali maeneo ya nyuklia, vituo vya kurushia makombora, na kuwalenga makamanda wa juu wa kijeshi  katika operesheni ambayo Waziri Mkuu Netanyahu ameipa jina la ‘Operesheni ya Simba Anayeamka’ (Operation Rising Lion).

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, aliandika kwenye mtandao wa X jioni hii kwamba utawala wa Kizayuni (Israel) hautabaki salama kutokana na matokeo ya uhalifu wake.

Related Posts