Rais Samia aeleza sababu kuifungua Dodoma

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ametaja umuhimu wa kujengwa kwa miundombinu ya kisasa katika Jiji la Dodoma, akiwahimiza wananchi kuitumia miundombinu hiyo kuboresha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Ametoa kauli hiyo leo Juni 14, 2025, wakati wa mkutano wa hadhara jijini Dodoma, baada ya kufanya ukaguzi wa barabara ya Mzunguko wa Nje na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, akiwa pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina.


Rais Samia amependekeza barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma iitwe jina la Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dk Akinwumi Adesina, akitambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya miundombinu nchini.

Pendekezo hilo limekubaliwa kwa kauli moja na wananchi waliohudhuria mkutano huo, na kuamuliwa rasmi kwamba barabara hiyo itaitwa Barabara ya Dk Akinwumi Adesina kuanzia leo.

Aidha, Rais Samia amesema uhamisho wa makao makuu ya Serikali Dodoma miaka nane iliyopita, umeleta manufaa makubwa kwa wakazi wa mkoa huo na mingine jirani, na umeibua haja ya kuboresha miundombinu ya mji ili kuendana na ongezeko la idadi ya watu na shughuli za kijamii.


“Msongamo uliopo sasa ni dhahiri ukiachwa utaleta athari katika biashara ndani ya nchi na ukanda mzima, ili kuondoa hilo inahitajika barabara ambayo itawezesha magari makubwa na madogo yasiyokuwa na ulazima wa kuingia katikati ya Dodoma kuendelea na safari zakem hivyo kupunguza muda na gharama za safari,” amesema Samia.

“Kutokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi na utawala, wakazi wa Dodoma wanahitaji usafiri rahisi wa kurahisisha maisha yao, hivyo Serikali ilianzisha mradi wa barabara ya mzunguko wa nje ya jiji,” amesema.


Rais Samia amesema usafiri wa anga umeongezeka, na licha ya maboresho madogo uwanja wa ndege wa Dodoma ulikuwa mdogo na haukuweza kupanuliwa kupokea ndege kubwa zaidi.

Amesema Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unajengwa ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Kuhusu barabara ya mzunguko ya Dodoma, amesema AfDB imetoa mkopo nafuu wa Sh489.892 bilioni wakati Serikali imechangia Sh90 bilioni.


Kwa upande wake, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amesema ilikuwa ni ndoto ya tangu Rais wa awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere na wengine waliomfuata, akiwemo yeye (Kikwete), lakini haikutimia badala yake ipo chini ya Rais Samia na sasa uwanja huo unakuwa na hadhi ya kupokea ndege kubwa kuliko zote duniani, ukizidi wa Dar es Salaam.

Kikwete amesema kwa wastaafu kama yeye wanatamani kuona nchi ikiwa na utulivu na amani na akaeleza namna vijana wanavyochapa kazi kumsaidia Rais katika majukumu yake.

Rais wa AfDB, Dk Adesina amethibitisha kuendelea kusaidia miradi mikubwa nchini Tanzania, ikiwemo ujenzi wa Reli ya SGR kipande cha Tabora hadi Uvinza kwa mkopo wa Dola 994.3 milioni.

Amesema tangu kuanzishwa kwa AfDB mwaka 1971, Tanzania imepokea jumla ya Dola 9 bilioni, na kipindi cha uongozi wake, Dk Adesina imepokea Dola 4.73 bilioni.


Dk Adesina amesema uwanja wa Msalato utaongeza biashara, utalii na ujumuishaji wa kikanda, huku ukikuza maendeleo ya Dodoma kama kitovu cha kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa. Makame Mbarawa amesema uwanja wa ndege wa Msalato umeshatumia hadi sasa Sh370 bilioni na utakuwa wa daraja la F baada ya kukamilika, kiwango cha juu kabisa kimataifa kwa viwanja vya ndege.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema barabara ya mzunguko ya Dodoma yenye urefu wa kilomita 112.3 inajengwa kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji.


“Mradi huu ni wa ubia kati ya Serikali na AfDB kupitia mkopo nafuu. Aidha, upanuzi wa barabara ya Chamwino Ikulu hadi Kimbinyiko wenye njia sita na urefu wa kilomita 32 upo kwenye mpango,” amesema Ulega.

Related Posts