Zanzibar kushirikiana na Serikali ya Uingereza kujenga miradi ya maendeleo

Unguja. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,  Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum amesema Zanzibar inatambua umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Uingereza, kwa lengo la kuchambua na kutambua maeneo mapya ya ushirikiano ya kiuchumi,  yatakayochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuimarisha maendeleo endelevu.

Ameeleza hayo leo Juni 14, 2025 baada ya mazungumzo na ujumbe wa Serikali ya Uingereza, ukiongozwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania,  Marianne Young na  Mjumbe wa Biashara wa Serikali ya Uingereza Afrika Mashariki, Kate Osamor.

Dk Saada amesema awali walishirikiana na Serikali hiyo katika miradi ya maendeleo nchini ikiwamo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba unaojengwa kwa fedha za mkopo kutoka United Kingdom Export Finance (UKEF) kwa gharama za Euro 170 millioni (Sh516.75 billioni).

Miradi mengine ni ujenzi wa barabara kutoka Mkoani hadi Chake Chake Pemba yenye urefu wa kilomita 43, Tunguu hadi Makunduchi yenye urefu wa kilomita 48 na Fumba hadi Kisauni yenye urefu wa kilomita 12 ambazo kwa pamoja zinajengwa kwa gharama ya Euro 230 millioni (Sh607.24 billioni).

Ameeleza kuwa, huo ni mwendelezo wa ushirikiano wao kwa kuwa, kipindi cha nyuma walisaidiana kutatua changamoto za kijamii ikiwamo ujenzi wa miradi ya maendeleo, kutatua changamoto zinazowakumba vijana wanaotumia dawa za kulevya na usimamizi wa fedha.

“Kwa sasa wameonesha nia ya kushirikiana katika miradi mikubwa ikiwamo umeme, majisafi na salama na miundombinu ya eneo la kibiashara katika Bandari Kuu ya Mangapwani na wamefurahishwa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema Dk Saada

Naye, Balozi Marianne amesema wapo tayari kuendeleza ushirikiano huo wa muda mrefu kwa kutafuta namna bora ya kukuza uchumi nchini.

Mbali na miradi mengine, amesema Serikali hiyo ipo tayari kuwekeza katika sekta ya kilimo na utalii endelevu kama inavyosema sera ya utalii nchini hapa.

Hivi karibuni ujumbe huo umekutana na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi na ameeleza nia ya kukifungua Kisiwa cha Pemba kiuchumi.

Kwenye mazungumzo hayo, Dk Mwinyi, amesema kuwa licha ya ongezeko la uzalishaji wa zao la mwani kisiwani hapa bado bei ya hairidhishi kulingana na juhudi zinazofanywa na wazalishaji, hivyo ametoa rai kwa ujumbe huo kuangalia njia bora ya kuwawezesha wazalishaji na kuongeza thamani ya zao hilo.

Vilevile, Dk Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji wawekezaji zaidi kutoka sekta binafsi ili kufikia dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050, hivyo amekaribisha wawekezaji kuwekeza Zanzibar.

Related Posts