Fedha zinazotumwa nchini na diaspora zaongezeka hadi Sh2.11 trilioni

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema fedha zinazotumwa nchini na Watanzania waishio nje ya nchi zimeongezeka huku uwekezaji wao hapa nchini pia ukiongezeka.

Balozi Kombo amebainisha hayo leo Juni 15, 2025 wakati akizungumza na jumuiya ya Watanzania wanaoishi Jimbo la Guangdong katika Jamhuri ya Watu wa China ambako amefanya ziara ya kimkakati.

Amesema takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2024, fedha zilizotumwa na Watanzania waishio nje ya nchi kuja nchini ni Sh2.116 trilioni, ukilinganisha na Sh2.045 trilioni kwa mwaka 2023.

“Kiasi hicho kina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya familia zenu nyumbani, kusaidia uwekezaji na kuchangia ukuaji wa sekta ya fedha nchini,” amesema Kombo huku akisisitiza kwamba Serikali imeendelea kupigania masilahi ya Watanzania wanaoishi nje.

Balozi Kombo amesema Watanzania wanaoishi nje ya nchi, pia, wamekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo katika miradi ya maendeleo. Amesema hadi kufikia Februari 2024, uwekezaji wa Watanzania wanaoishi nje katika Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT-Amis) umefikia Sh7.5 bilioni ukilinganisha na Sh6.4 bilioni, mwaka 2023.

“Ninafahamu kuwa mwaka jana UTT-Amis waliwatembelea hapa Guangzhou kwa lengo la kuwahamasisha muwekeze huko.

“Ninatumaini mliambiwa faida zake na sasa mnaendelea kuwekeza huko kwa kasi kwa kuzingatia kuwa kuna fursa nyingi sana za biashara na uwekezaji katika hii nchi mnayoishi ambazo zinawapatieni vipato. Hatua hiyo, inachangia ukuaji wa sekta ya fedha na uwekezaji wa ndani,” amesema.

Vilevile, amesema Watanzania wengi waishio nje wamenunua nyumba na viwanja kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na sekta binafsi hivyo kuchangia maendeleo ya sekta ya milki na kuchangia upatikanaji wa makazi bora.

“Uwekezaji huo umeongezeka kutoka Sh7.569 bilioni mwaka 2023 hadi kufikia Sh9.28 bilioni, mwaka 2024,” amesema Balozi Kombo.

Balozi Kombo amesema kwa kutambua mchango huo mkubwa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuhakikisha Watanzania waishio nje wanashirikishwa kikamilifu katika ujenzi wa Taifa. Amesema moja ya hatua hizo ni uzinduzi wa toleo jipya la sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001.

“Sera hii pia imeweka mikakati ya kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa Watanzania waishio nje, ili kuhakikisha kuwa mnakuwa na fursa sawa na za haki katika kushiriki kwenye uwekezaji na biashara nchini,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali imeanzisha Kitengo Maalumu cha Diaspora chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Amesema kitengo hicho kimepewa jukumu la kuratibu masuala yote yanayohusu Watanzania waishio nje na kuhakikisha kuwa wanawashirikisha kikamilifu.

“Kwa kupitia kitengo hiki, tumeweza kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kanzidata, ambao unawezesha Watanzania waishio nje kama nyinyi, kujisajili na kutoa taarifa zao za msingi. Kanzidata hii ni muhimu sana katika kuratibu mchango wenu na kurahisisha mawasiliano kati yenu na Serikali,” amesema.

Mbali na hayo, Balozi Kombo amesema Serikali, pia, imechukua hatua za kuhakikisha kuwa raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania wanahusishwa kikamilifu katika maendeleo ya taifa lao.

Amesema kwa kutambua mchango wao na uhusiano wao wa karibu na Tanzania, mchakato wa hadhi maalum utakapokamilika bungeni, wanatarajia kuwapatia kadi maalum inayowapatia hadhi maalumu na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi nchini.

“Kadi hii itatoa fursa maalumu za kisheria na kiuchumi kwa Watanzania waliopoteza uraia wao lakini wanapenda kuendelea kushiriki katika masuala ya kijamii na kiuchumi nchini.

“Hii ni hatua kubwa na muhimu katika kuhakikisha kuwa tunatumia rasilimali zetu za watu kwa ufanisi zaidi, na pia ni njia ya kurahisisha ushirikiano wetu na Watanzania wenzetu waishio nje, ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu,” amesema.

Related Posts