Helikopta ya mahujaji yaanguka, yaua saba India

Kedarnath, India. Katika tukio la kusikitisha lililotokea India, helikopta iliyokuwa ikiwabeba mahujaji wa dini ya Kihindu imeanguka dakika chache baada ya kupaa, na kuua watu wote saba waliokuwa ndani.

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, ajali hiyo ilitokea asubuhi na mapema, saa 11:30 kwa saa za huko (saa 3:00 kwa saa za Tanzania), ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kuanza safari ya dakika kumi kuelekea kituo cha hija cha Guptkashi kilichopo katika safu ya milima ya Himalaya, jimbo la kaskazini la Uttarakhand.

Helikopta hiyo ilikuwa imeondoka kutoka mji wa Kedarnath, eneo linaloheshimiwa sana na waumini wa dini ya Kihindu, ambapo msongamano wa mahujaji huzidi kila msimu wa kiangazi. Kutokana na mazingira magumu ya milima, huduma za helikopta hutumika kwa wingi kusafirisha mahujaji.

Maafisa wamesema kuwa helikopta hiyo, iliyokuwa inamilikiwa na kampuni binafsi ya Aryan Aviation, ilianguka ndani ya eneo la msitu, mbali kidogo na njia kuu ya mahujaji. Sababu ya ajali hiyo inaelezwa kuwa ni hali mbaya ya hewa, ambayo mara kwa mara hubadilika ghafla katika maeneo hayo ya juu.

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni rubani pamoja na mahujaji waliotoka majimbo jirani ya Uttar Pradesh, Maharashtra na Gujarat. Miili yao iliteketea vibaya kutokana na moto uliozuka baada ya ajali hiyo, taarifa ya maafisa wa uokoaji imesema.

Tukio hili linajiri siku tatu tu baada ya ajali nyingine kubwa ya ndege kutokea nchini humo, ambapo ndege ya Shirika la Ndege la India (Air India) ilianguka chini ya dakika moja baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Ahmedabad, na kuua takribani watu 270.

Tayari mamlaka zimeanzisha operesheni ya uokoaji na uchunguzi, huku ikielezwa kuwa taratibu za usalama na uendeshaji wa safari za anga katika eneo hilo zitapitiwa upya.

Ajali za helikopta si jambo geni katika eneo hilo la Himalaya, kwani hali ya hewa hubadilika bila kutabirika na hewa nyembamba ya maeneo ya juu huongeza hatari ya ajali.

Katika tukio jingine mapema mwezi huu, helikopta nyingine iliyokuwa ikihudumu katika Bonde la Kedarnath ililazimika kutua kwa dharura barabarani muda mfupi baada ya kupaa, kutokana na hitilafu ya kiufundi. Rubani alijeruhiwa, lakini abiria watano waliokuwa ndani waliokolewa wakiwa salama.

Mei mwaka huu, helikopta nyingine ilianguka katika wilaya ya Uttarkashi, na kusababisha vifo vya watu sita wakiwemo rubani, huku mtu mmoja pekee akinusurika.

Tukio hili la hivi karibuni limezidisha simanzi miongoni mwa familia za waathirika, waumini na jamii kwa ujumla, huku sauti zikiendelea kuitaka serikali kuimarisha hatua za kiusalama kwa huduma za anga katika maeneo yenye hija muhimu.

Related Posts