Kibano kwa waagizaji mbolea zisizozingatia afya ya udongo chaja

Dodoma. Serikali imesema baada ya kukamilika kazi ya upimaji wa afya ya udongo nchini, itapiga marufuku uagizaji wa mbolea zisizozingatia mahitaji ya udongo husika, kwa lengo la kulinda afya ya ardhi na kuongeza tija katika kilimo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Juni 15, 2025 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alipozungumzia uzinduzi wa Kiwanda cha Mbolea cha Intracom, kinachotarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Juni 28, 2025.

Bashe amesema tayari ramani ya afya ya udongo imekamilika katika mikoa mingi na kwamba, hatua inayofuata ni kuhakikisha matumizi ya mbolea yanayozingatia taarifa hizo.

“Tutakwenda hatua inayofuata ya kupiga marufuku uagizaji wa mbolea za aina ya generic. Haiwezekani kuanzia Dar es Salaam hadi Kataramke wote tunatumia mbolea ya DAP kupandia, hali hiyo ilisababishwa na kukosekana kwa taarifa sahihi za udongo,” amesema Bashe.

Pia, amesema kiwanda hicho kimenunua tani 100,000 za samadi kutoka kwa wafugaji wa ndani zenye thamani ya Sh15 bilioni, hatua inayolenga kuwasaidia wafugaji kupata soko la uhakika la bidhaa hiyo.

Aidha, amebainisha kuwa, kiwanda hicho pia kinazalisha chokaa kwa ajili ya kurekebisha tindikali kwenye udongo ulioathirika ili kuboresha afya ya udongo katika maeneo husika.

“Ili kulinda viwanda vya ndani, Serikali imepanga kununua tani 200,000 za mbolea na tani 50 za chokaa kwa ajili ya kilimo mwaka huu,” amesema.

Takwimu za Wizara ya Kilimo za mwaka 2024 zinaonesha mahitaji ya mbolea nchini yalifikia tani 848,884, huku tani 114,223 pekee zikizalishwa nchini na tani 614,651 zikiagizwa kutoka nje.

Bashe amesema licha ya mfumo wa ruzuku kuendelea, Serikali itanunua mbolea hiyo na kuisambaza katika maeneo yenye matumizi duni, ikiwa ni mkakati wa kuongeza matumizi ya mbolea zinazozalishwa nchini.

Amefafanua kuwa, lengo la muda mrefu ni kuhakikisha asilimia 80 ya mbolea inatokana na uzalishaji wa ndani huku asilimia 20 pekee ikiagizwa kutoka nje ya nchi.

Kuhusu kuongeza uzalishaji wa ndani, Waziri Bashe amesema Serikali ipo kwenye mazungumzo na wawekezaji wawili watakaowekeza kwenye viwanda vya kutengeneza mbolea ya Urea kwa kutumia makaa ya mawe.

Kwa upande wa uzinduzi wa Kiwanda cha Intracom, amesema Rais wa Burundi, Meja Jenerali Mstaafu Évariste Ndayishimiye amethibitisha kushiriki katika hafla hiyo.

Pia, mawaziri wa kilimo kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wamealikwa, lengo ni kutaka kukuza soko la mbolea hiyo kikanda.

Mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho, Nduwimana Nazaire amesema uzinduzi huo unafanyika baada ya miaka mitatu na nusu tangu ujenzi wa kiwanda uanze.

“Tumeweza kuzalisha fomula 14 za mbolea kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za utafiti. Tuna uwezo wa kutengeneza mbolea kulingana na eneo, zao na mahitaji ya mkulima,” amesema Nazaire.

Kiwanda cha Intracom kimegharimu uwekezaji wa Dola180 milioni za Marekani na kimetoa ajira za moja kwa moja kwa watu 1,805 huku ajira zisizo za moja kwa moja zikikadiriwa kufikia 5,000.

Related Posts