Dar/Arusha. Wakati baadhi ya watu wakifurahia usingizi nyakati za mvua, kwa wengine hali hiyo ni chanzo cha hofu, huzuni na maafa.
Wanapolala, hawana uhakika iwapo wataamka salama au watapata tena makazi.
Hali hii ni uhalisia wa maisha ya wakazi wa pembezoni mwa mito Gide mkoani Dar es Salaam na Ngarenaro, Arusha, ambako mvua badala ya kuwa baraka kwao, huwa tishio la usalama wa maisha.
Maafa yanayowakumba wakazi hao ni kielelezo cha athari za mabadiliko ya tabianchi katika miji.
Mito iliyokuwa mifereji midogo zamani, sasa imepanuka na kusomba makazi kutokana na mvua kubwa, hali inayochangiwa na ongezeko la joto duniani.
Ripoti ya jopo la kimataifa la wataalamu kuhusu mabadiliko ya tabianchi (IPCC) ya mwaka 2023 inaeleza miji mingi barani Afrika inakabiliwa na hatari ya mafuriko kutokana na ongezeko la mvua na ukosefu wa mipango miji iliyo thabiti.

Kukua kwa miji bila mpangilio, changamoto katika mifumo ya mifereji na ukosefu wa makazi mbadala vinawaacha wakazi wa maeneo ya mabondeni katika hatari ya kupoteza maisha na mali zao.
Takribani kaya 50 zimepoteza makazi eneo la Mabibo Mgundini mkoani Dar es Salaam, pembezoni mwa Mto Gide, huku zaidi ya kaya 1,590 zikiwa hatarini kukumbwa na mkasa huo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hadi 2024.
Ingawa uharibifu huu umehusishwa na ujenzi holela kinyume cha sheria, baadhi ya wakazi wanasema walipojenga, maeneo hayo hayakuwa mito bali mifereji midogo ya maji ya mvua.
“Mto huu umetufuata. Nimejenga hapa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Ulikuwa mfereji mdogo ulio mbali kutoka nyumba yangu. Sasa umefika hadi ukaibeba nyumba,” anasema Mwajuma Mellol, mkazi wa Dar es Salaam.
Kauli ya Mwajuma inaonesha si wote waliokiuka kifungu cha 55 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kinachozuia shughuli ndani ya mita 60 kutoka kingo za mito, bahari au maziwa. Kwa baadhi, mto uliwafuata kadri mazingira yalivyobadilika.
Kwa sasa, Mwajuma anaishi kwa jirani aliyemsaidia baada ya nyumba aliyorithi kutoka kwa marehemu mume wake kusombwa na maji ya Mto Gide.
Kwa upande wake, Othman Orotu mkazi wa Arusha, mbali ya nyumba yake kusombwa na maji ya Mto Ngarenaro, aliachwa na mwenza wake wa zaidi ya miaka 10.
“Aliniambia tuhame tukapange, sikuwa na fedha. Alinitahadharisha mapema kwamba ipo siku nyumba yetu itaingiliwa na maji. Ilipotokea aliondoka akisema mimi ni mzembe,” anasimulia Orotu.
Anasema alipojenga eneo hilo, halikuwa na mto wala mfereji hali inayoashiria uwapo wa mabadiliko ya tabianchi.
“Wengine wanasema tulijenga karibu na mto, lakini hawakuwapo kipindi tunajenga. Nilijenga hapa miaka mingi iliyopita hakukuwa na chochote, leo kuna mto unaobeba hadi nyumba,” anaeleza.
Baada ya kuachwa na mwenza aliyeondoka na watoto, Orotu sasa anasema anaishi kwa kaka yake eneo la Njiro, Arusha.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mgundini uliopo Mabibo, Dar es Salaam, Said Kitogo anasema nyumba zaidi ya 1,000 ziko hatarini kusombwa na maji ya Mto Gide.
“Takriban miaka 20 iliyopita mto huu ulianza kupanuka na kufuata makazi ya watu. Pamoja na juhudi za kuusafisha mara kwa mara kwa kushirikiana na madiwani, bado hali si shwari,” anasema.
Anaeleza uchafu na taka zinazoziba njia ya mto zimechangia kupanuka kwake, hivyo Serikali inapaswa kuingilia kati kwa kuondoa uchafu na kuurejesha kwenye mkondo wake wa awali.
Mkoani Arusha, Mwenyekiti wa Mtaa wa Darajani, Kata ya Ngarenaro, Hemedi Ally anasema nyumba zilizopo eneo hilo zilijengwa miaka mingi iliyopita.
“Hizi nyumba zipo tangu tulipozaliwa. Wamiliki wake wanathibitisha kuwa wakati wanajenga huu mto ulikuwa mfereji mdogo na mbali kabisa na makazi yao,” anasema.
Anasema kadri miaka ilivyosonga, mto ulipanuka na kuanza kusomba baadhi ya nyumba huku nyingine zikiwa hatarini.
Kama hatua za awali, mawe yamewekwa kwenye kingo za mto ili kuzuia shughuli za kibinadamu.
“Tumeendelea kutoa elimu kuhusu masharti ya ujenzi na sheria zinazohusika. Hata hivyo, ukweli ni kwamba hakuna kikao rasmi kilichowahi kuitishwa kwa ajili ya kuwaondoa wananchi maeneo hayo,” anasema.
Katika mtaa huo, baadhi ya nyumba zinaning’inia juu ya mto na ziko kwenye hatari ya kuanguka wakati wowote, huku wamiliki wakiendelea kuishi ndani kutokana na ukosefu wa maeneo mbadala ya kuhamia.
“Wengine wamesogeza nyumba, lakini wengi wameshindwa kwa sababu hawana pa kwenda. Na ukweli ni kwamba, mto ndiyo uliowafuata,” anasema.
Matumaini ya kupatikana suluhu ya changamoto hiyo kwa upande wa Dar es Salaam huenda yakaanza mwaka 2027, baada ya Serikali kukamilisha utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) unaohusisha ujenzi wa Daraja la Juu la Jangwani, kama inavyoelezwa na Diwani wa Mabibo, Thomas Klerru.

Anasema Serikali ina nia ya kutekeleza ujenzi wa kingo za Mto Gide na utaingizwa kuwa sehemu ya mradi wa DMDP, lakini itafanyika hivyo baada ya kukamilika shughuli zinazofanyika sasa.
“Ni mradi mkubwa unaohitaji fedha nyingi na hatuwezi kutegemea bajeti yetu ya Serikali ya kawaida, ndiyo maana tumepanga kuiweka kwenye DMDP,” anasema.
Klerru anasema mpango wa ujenzi wa kingo za mto huo, unatarajiwa kuhusisha mto wote, kuanzia Mbezi na maeneo yote yaliyoathirika ambayo ni Saranga, Kimara, Ubungo, Mabibo hadi Kigogo.
“Tumesema angalau kwa mwaka 2027 shughuli nyingine kama daraja la juu la Jangwani litakuwa limekamilika na angalau tunafikiria mwaka 2027 mto huo unaweza kuingia kwenye programu,” anasema.
Anasema kuna gharama kubwa za ujenzi wa kingo hizo, akibainisha mita moja ya ujazo inagharimu Dola 500 za Marekani (zaidi ya Sh1.3 milioni).
“Sasa angalia kuanzia Mbezi, Ubungo, Mabibo, Kigogo hadi Mkwajuni tutatumia kiasi gani cha fedha. Ni mradi mkubwa na wananchi wanaweza kufikiria Serikali haina huruma lakini unafanyaje kwenye hali ya namna hiyo,” anasema.
Klerru anasema changamoto hiyo imekuwa ikisababisha wakati mwingine wananchi wasiwaelewe, lakini hawana namna zaidi ya kushughulikia kwa kadri ya uwezo wao.
“Hapa tunapoongea (Aprili 5, 2025) sisi Mabibo tumepata Sh12.6 milioni, tumefanikiwa kusafisha kuanzia Daraja la Kigogo, Mtaa wa Matokeo, Mabibo Farasi na nimebakiza Mtaa wa Mabibo na Shungashunga,” anasema.
Diwani wa Ngarenaro, Isaya Doita anasema kwa mwaka huu pekee nyumba nne zimesombwa na maji pembezoni mwa mto.
Idadi hiyo anasema ni tofauti na nyumba nyingi zilizosombwa wakati wa mvua za El-Nino (Oktoba 2023 hadi Aprili 2024) na zote zilikuwa karibu na mto huo.
“Kwenye mvua ya mwaka jana, nyumba nyingi zilisombwa na maji na kuna moja binti alikuwa ndani zikafanyika juhudi za kumuokoa,” anasema.
Anasema hadi sasa kuna nyumba maji yameingia kwa chini, zenyewe zinaelea juu na muda wowote zinaanguka, lakini bado wananchi wanaishi ndani.
“Niseme ukweli kuna shida hata kwa viongozi tumekuwa wanasiasa katika jambo hili. Tukipanga kuondoa wananchi, wapo baadhi wanataka wabaki,” anasema.
Kwa nafasi yake ya udiwani anasema anakosa namna kwa kuwa hana nguvu ya kuamua zaidi, kwa kuwa hana mamlaka ya kusimamia sheria.
“Hata juzi (Machi 23, 2025) chumba kimoja karibu na mto kimedondoka na hadi sasa mwenye nyumba ametaka kukirudishia lakini tumemkatalia,” anasema.
Meneja wa Tarura Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga anasema licha ya madai ya wananchi kuwa walijenga kabla ya kuwapo mito hiyo, uhalisia ni kuwa wengi wamejenga kinyume cha sheria.
“Ukitazama mtu yupo ndani ya mita 60 wengi wapo kwenye mto wenyewe na wanapunguza umbali wa mito wakihifadhi viwanja,” anasema.
Suala la uboreshaji wa mito, anasema wanalifanya kwa ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali, ikiwamo mamlaka ya Serikali za mitaa.
Anasema Mto Gide ni miongoni mwa iliyoingizwa kwenye mpango wa kuboreshwa kupitia mradi wa DMDP, isipokuwa kipaumbele kiliwekwa kwa barabara kwa sababu ndiyo ilikuwa hitaji kubwa.
“Kwanza tuliweka vipaumbele, ikabidi tuanze na barabara kwa sababu ya umuhimu wake. Nyingi tumezijenga zile ambazo hazijajengwa ni kwa sababu ya changamoto mbalimbali lakini zote zitajengwa,” amesema.
Baada ya barabara, anasema kinachofuata ni Tarura kuandaa vigezo na masharti ya wasanifu watakaohitajika kisha itangazwe zabuni ili wapatikane watakaofanya tathmini ya mto huo na kupendekeza maboresho ikiwamo ujenzi wa kingo kwa kadiri watakavyoeleza.
Katika mradi wa DMDP, anasema walianza na mingine na sasa wataingia kwenye maboresho ya mito, ujenzi wa dampo, vituo na masoko.
Kuhusu kuwafidia waathirika, anasema atakayelipwa ni atakayethibitika kuwa katika eneo sahihi lakini si wale waliojenga kinyume cha sheria.
“Sasa unamlipa nani kwa mtu ambaye yeye mwenyewe hakufuata sheria. Baada ya kutathmini kile tutakachokikuta kwenye mradi wakati huo ndipo mtu atakayetakiwa kulipwa atalipwa. Lakini kama umevunja sheria hatutakulipa,” anasema.
Habari hii imeandaliwa kwa udhamini wa Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765 864 917.