Habari. Nimeolewa na nina watoto watatu. Ninataka kufanya biashara ila sijui nifanye biashara gani. Naomba ushauri wako nitoke vipi.
Hongera kwa kuwa mke bora anayefikiria kujiingizia kipato licha ya kuwa ameolewa. Maana wapo wanaowategemea wame zao kwa kila kitu.
Kwa sababu hujasema una mtaji kiasi gani nitakushauri biashara kadhaa za kufanya kulingana na maisha yako ya sasa kwa maana ya kuwa mke na mama wa watoto watatu.
Pia nitakushauri kwa kukadiria mtaji mdogo tu wa mama wa nyumbani, kwa maana ya kukutajia au kukushauri biashara za mjasiriamali mdogo anayeanza. Na kutokana na majukumu ya familia ya watoto watatu kama ulivyosema biashara inayokufaa ni ambayo hautakuwa nje ya nyumbani kwa muda mrefu.
Kwanza kabla ya kuanza ujipe ujasiri na kutokana tamaa, kwani kila kitu kina changamoto ikiwamo biashara.
Moja ya biashara ambazo ningekushauri uanze nayo ni ya vyakula au vitafunwa. Hii ni biashara ambayo haipotezi soko, kwani kila mtu anahitaji kula. Ikiwa unapika vizuri au unapenda kupika, unaweza kuanza kwa kupika maandazi, vitumbua, chapati, au hata chakula cha mchana ambacho utakisambaza kwenye maeneo jirani mfano sokoni au maofisini, siyo lazima ofisi za mbali hata kwenye saluni, madukani ukiwalenga wauzaji, shuleni.
Unaweza kuanza kwa kupika vitu vichache nyumbani kisha unasambaza kwenye maeneo niliyokwisha kuyataja.
Hapa si pa rahisi kwama unavyodhani kwani siku hizi wajasiriamali ni wengi hivyo utakuta kuna wenzako waliokutangulia, hivyo jitofautishe. Unaweza kuamua wewe unapika vitu vya asili tu, kama maboga, kisamvu, nyama ya kukaushwa, dagaa wa kuokoa n.k. Pia unavyoviandaa, siku hizi kuna vifungashio vya kila aina unaweza kuvitumia pia kujitofautisha na wanaoweka kwenye masahani.
Baada ya muda, jina lako litajulikana na biashara itakua polepole bila kuteseka sana na hutokwenda mbali na familia yako kwa muda mrefu.
Biashara nyingine nzuri ni ya kuuza bidhaa za matumizi ya kila siku kama sabuni, mafuta ya kupikia, chumvi, unga, maziwa, na sukari. Unaweza kuanza na kibanda kidogo nje ya nyumba yako au sehemu iliyo karibu. Uzuri wa biashara hii ni kwamba haihitaji ujuzi wa kipekee na bidhaa zake huwa zinajiuza zenyewe kwa kuwa ni mahitaji ya kila siku. Pia, ukiwa na muda, unaweza kuongeza bidhaa kama gesi ndogo ndogo au vyakula vya watoto, ambavyo ni mahitaji muhimu kwa familia nyingi.
Kwa kuwa wewe ni mama na una uzoefu wa kulea watoto, unaweza pia kuangalia uwezekano wa kuanzisha biashara ya kuangalia watoto (daycare) ikiwa una nafasi nyumbani. Wazazi wengi siku hizi wanatafuta sehemu salama za kuwaacha watoto wao wakiwa kazini. Kama unapenda watoto na una mazingira ya kutosha, hii inaweza kuwa biashara ya muda mrefu, yenye malipo mazuri na inayokufanya ukae karibu na familia yako huku ukipata kipato.
Biashara nyingine ni kuuza bidhaa za mtandaoni. Unaweza kuuza mitumba, vipodozi, viungo vya chakula kupitia mitandao kama WhatsApp, Facebook, au Instagram. Mtandao ni soko kubwa sana ambalo linakupa uwezo wa kufikia wateja wengi bila kulazimika kuwa na duka, hapa utaokoa muda na gharama za kukodisha fremu kwa ajili ya duka ilihali bado unajitafuta. Zingatia huu ni mwanzo wa kukupatia uzoefu, ila siku zote fikiria mawazo makubwa.