Rais Samia, Profesa Juma wampa mzigo Jaji Mkuu mpya

Dar es Salaam. Profesa Ibrahim Juma amehitimisha safari ya miaka takribani saba ya kuiongoza Mahakama akiwa Jaji Mkuu wa Tanzania huku akimtaka mrithi wake, George Masaju kuendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan.

Jaji Mkuu, Masaju amesema amepokea kijiti hicho akiahidi kuendelea alipoishia Profesa Juma kwa kuhakikisha wanatenda haki kwa watu wote bila kujali hali ya mtu kiuchumi na kijamii.

Wakati huohuo,Rais Samia Suluhu Hassan amempa hongera na pole, Jaji Mkuu, Masaju akimweleza jukumu lililopo mbele yake ni kubwa: “Mungu akupe hekima na busara uweze kuifanya vyema kazi hiyo.”


Viongozi hao wamesema hayo leo Jumapili, Juni 15, 2025 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma baada ya Rais Samia kumaliza kumwapisha Masaju kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania akimrithi Profesa Juma.

Masaju aliteuliwa Juni 13, 2025 kushika wadhifa huo.

Awali, alikuwa mshauri wa Rais masuala ya sheria. Awamewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mshauri wa masuala ya sheria wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Baada ya kuhitimisha safari ya miaka saba na miezi tisa,  leo Jumapili, saa 4:10 asubuhi, Profesa Juma aliyeuliwa Septemba 10, 2017 na Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Magufuli amemshukuru Mungu kwa kumwezesha kuimaliza kazi hiyo salama.  

Profesa Juma amemtaka Jaji Mkuu, Masaju kuhakikisha Mahakama inaimarisha ushirikiano na mihimili mengine na kuachana na dhana potofu kuwa ushirikiano huo unaifanya Mahakama kushindwa kutenda haki. 


Profesa Juma amesema ili Mahakama iweze kutimiza jukumu lake la kusimamia haki ni lazima ishirikiane na mihimili mingine, hivyo ndivyo alivyofanya katika kipindi cha uongozi wake. 

Amesema kuna upotoshaji wa ushirikiano unaotafsiriwa kama kuingilia uhuru, ukweli ni kwamba ushirikiano unatusaidia kupata rasilimali kwa sababu uchumi na maendeleo ya nchi unahitaji kuwa na Mahakama bora.

“Ni lazima tuwe na ushirikiano ingawa ukisikiliza sana mitandao ya kijamii wana tafsiri hasi ya uhuru wa Mahakama. Wengi wanaamini ushirikiano na mihimili mingine ni kuingilia uhuru wa mahakama,” amesema Profesa Juma.

Profesa Juma aliyezaliwa Juni 15, 1958, wilayani Musoma, Mkoa wa Mara ametolea mfano hata akiwa na Rais Samia, Waziri Mkuu na au Spika katika mazungumzo yao, hawajawahi kuzungumzia masuala ya kesi bali huwa wanaongelea mambo yenye masilahi makubwa.

Ameweka wazi ushirikiano mkubwa aliopata kutoka kwa Rais Samia kipindi cha uongozi wake ulimuwezesha kufanya mageuzi makubwa katika mhimili wa Mahakama. 

“Pamoja na kunipa mazingira mazuri ya kufanya kazi, ulinipa uwezeshaji mkubwa ulioleta utulivu wa hali ya kipekee katika Mahakama,” amesema.

New Content Item (1)


New Content Item (1)

Katika hilo, Profesa Juma akamweleza mrithi wake: “Ushauri wangu kwako Jaji Mkuu, siku zote jicho lako likamate jicho la Rais, muangalie anafanya nini na hicho anachokifanya kitasaidiaje Mahakama.”

“Huyu ni mdau muhimu, bila uwekezaji wake hakuna chochote kinaweza kufanyika. Siku zote fuatilia hotuba za Rais, mule ndani kuna ahadi anazitoa hizo unaweza kuzitumia kama silaha.”

Aidha, Profesa Juma amemtaka Masaju kusimamia ukamilishaji ujenzi wa Mahakama za Mwanzo na Wilaya maeneo mbalimbali nchini kwani fedha zilikwishatoka serikalini na kwa wadau wa maendeleo ambao muda ukipita zitapaswa kurudshwa.

Profesa Juma ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani zake kwa Rais Samia kwa kumuamini katika kipindi chote alichohudumu kama Jaji Mkuu na kumpongeza kwa kumpata Jaji Mkuu mpya. 

“Leo ni siku ya shukrani kwa Mungu kwa kukuongoza Rais kuweza kumtafuta, kumpata, kumteua na kumuapisha Jaji Mkuu wa tisa. Ni rahisi kuorodhesha Watanzania wengi wenye sifa ya kuwa Jaji Mkuu lakini sio rahisi kumpata mtu mwenye vigezo vya sifa za kumpata Jaji Mkuu kulingana na wakati uliopo,” amesema Profesa Juma.

Alichokisema Spika Tulia 

Suala la mihimili mingine kutokuwa na uhusiano wa kuingiliwa na uhuru wa Mahakama, limezungumziwa pia na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.


Katika salamu zake, Dk Tulia amesisitiza umuhimu wa Watanzania kutambua tofauti ya mihimili hiyo na kumuweka Rais katika mahali anapostahili kila anapotekeleza majukumu yake chini ya mhimili husika. 

“Ni muhimu wa Tanzania wakafahamu kwamba, Rais ana nafasi nyingi Kikatiba na zote zimewekewa majukumu yake. Anaposhirikiana na Mahakama anayo majukumu Kikatiba kama mkuu wa nchi, hii haihusishi nafasi yake kama mkuu wa Serikali,” amesema.

Mkuu huyo wa muhimili wa Bunge amesema:“Yako mazingira ambayo pengine yanawafanya Watanzania kumtazama Rais kama mkuu wa Serikali wakati wote. Kuna wakati anatoa maelekezo kama mkuu wa nchi na wakati mwingine mkuu wa Serikali haya ni majukumu tofauti watu wanapaswa kujifunza kuyafahmu vyema.” 

Rais Samia amemtaja Profesa Juma kama Jaji aliyeandika historia na kuacha alama kubwa na kufanikisha kuongeza imani ya Watanzania katika mhimili wa Mahakama. 

Amesema katika kipindi cha uongozi wake amekuza ushirikiano na mihimili mingine ya dola na kufanya mageuzi makubwa kwenye mhimili huo. 

“Nikushukuru kwa kazi kubwa uliyofanya ndani ya mhimili wa Mahakama. Pamoja na kushikwa mkono na Serikali, uongozi wako ndani ya Mahakama ndiyo umeweza kuleta mageuzi yale, kimuundombinu, kimfumo na kiutendaji.

“Hongera kwa kukamilisha kazi hii bila makando kando. Wakati unazungumza nilikuwa nakuangalia usoni, sijawahi kukuona ukiwa na furaha na kuchangamka kama leo. Nikuombee ukapumzike kwa furaha, Mungu akuongoze katika shughuli ulizopanga kufanya baada ya kustaafu, hata hivyo Serikali haitasita kukutumia pale itakapokuhitaji,” amesema.

Kuhusu Jaji Mkuu mpya, Rais Samia amesema matarajio ya Watanzania ni kuona Mahakama ikiendelea kusimamia haki ndani ya nchi na haki zetu nje ya nchi, hivyo ni muhimu kwake kuhakikisha hayo yanatimia. 


“Jaji mkuu mpya nikupongeze na nikupe pole kwa kwa mzigo huu sio mdogo, kuna kazi kubwa ya kufanya. Mungu akupe hekima na busara uweze kuifanya vyema kazi hiyo,” amesema.

Akirejea kauli aliyowahi kuitoa huko nyuma juu ya utoaji haki Rais Samia amesema: “Majaji kazi yenu ni kusimamia haki, kazi ya kutoa haki ni ya Mungu.” 

“Kwa Mungu kumezidi mambo mawili kudra na jahara lakini majaji kazi yao ni kusimamia haki kwa misingi iliyopo. Eneo lingine ambalo ningependa ukaliangalie ni utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya haki jinai, kuna yale yaliyotekelezwa mengine bado.”

Jaji Masaju aliyezaliwa Aprili 7, 1965, Kijiji cha Bwai Wilaya ya Musoma mkoani Mara amesema ataendeleza kazi iliyofanywa na mtangulizi wake huku akiahidi kusimamia utoaji haki ambalo ndilo jukumu mahususi la Mahakama. 

Miongoni mwa maeneo ambayo ameahidi kuyafanyia kazi ni kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi ili kuharakisha utoaji na upatikanaji wa haki.

“Nashukuru Rais kwa kuniona nafaa katika kazi hii, nitaifanya kikamilifu. Katika kutoa haki tumepewa kanuni zinazotuongoza, mojawapo ya kanuni ni kutenda haki kwa watu wote bila kujali hali ya mtu kiuchumi na kijamii,” amesema.

Masaju ambaye sasa ana miaka 60 amesema ataendelea kushauriana na wenzake namna gani ya kusogeza huduma za kimahakama kwa wananchi. 

Masaju aliyewahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali ikiwamo mwanasheria mkuu wa Serikali ameahidi kuendeleza ushirikiano na waandishi wa habari na kubaki kuwa mtumishi wa umma.

Related Posts