Tarehe kuvunjwa mabaraza ya madiwani hadharani, Mchengerwa atoa maelekezo

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ametangaza kuwa mabaraza yote ya madiwani nchini yatavunjwa rasmi ifikapo Juni 20, 2025.

Tangazo hilo amelitoa leo Jumapili, Juni 15, 2025, alipokuwa akitoa tamko rasmi kuhusu tarehe ya kuvunjwa kwa mabaraza hayo pamoja na mikutano ya kamati za kudumu za halmashauri.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, mamlaka hayo yametolewa chini ya Sheria ya Serikali za Mitaa na Mamlaka za Wilaya, Sura ya 287, kifungu cha 178, ambacho kinamruhusu Waziri mwenye dhamana, kuvunja mabaraza hayo siku saba kabla ya Bunge kuvunjwa kuelekea uchaguzi mkuu.

Amesema tayari imefahamika kuwa Bunge litavunjwa rasmi Juni 27, 2025.

Akizingatia masharti hayo ya kisheria, Mchengerwa amesema amesaini notisi mbili za kuvunjwa kwa mabaraza ya madiwani katika mamlaka za wilaya na mamlaka za miji, ambazo zinatarajiwa kuchapishwa katika Gazeti la Serikali hivi karibuni.

Notisi hizo zinaelekeza kuwa vikao vya halmashauri na kamati zake vinapaswa kuwa vimekoma ifikapo Juni 20, 2025.

Ameonya kuwa kufanyika kwa kikao chochote cha halmashauri au kamati yake baada ya tarehe hiyo, itakuwa ni uvunjaji wa notisi hizo na mkurugenzi wa halmashauri husika atawajibika kwa mujibu wa sheria.

“Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kulivunja Bunge Juni 27 na mabaraza ya madiwani yanapaswa kufikia kikomo rasmi Juni 20,” amesema Mchengerwa.

Uendeshaji baada ya kuvunjwa

Mchengerwa ameeleza kuanzia Juni 20, 2025, shughuli zote za kamati za halmashauri zitasitishwa hadi uchaguzi mpya wa madiwani utakapofanyika.

Katika kipindi cha mpito, amesema majukumu yote ya halmashauri yatasimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, ambaye atakuwa mwenyekiti wa halmashauri, akisaidiwa na wakuu wa idara kama wajumbe wa kamati.

Pia, ameeleza kuwa mkurugenzi hataruhusiwa kuanzisha miradi au uwekezaji mpya, wala kufanya mabadiliko katika uamuzi au miradi iliyopitishwa kabla ya kuvunjwa kwa baraza. Aidha, mkurugenzi atatakiwa kuwasilisha taarifa ya mwenendo wa vikao vya menejimenti vilivyofanyika katika kipindi cha mpito kwenye kikao cha kwanza cha Baraza jipya la Madiwani.

Waziri huyo amesisitiza kuwa matumizi mabaya ya mamlaka au kutotekeleza ipasavyo majukumu ya kiutawala katika kipindi hicho, kutasababisha mkurugenzi kuwajibika binafsi kwa mujibu wa sheria.

Waziri huyo ametoa wito kwa wananchi, viongozi wa Serikali na watendaji wote wa halmashauri kushiriki kikamilifu katika kipindi hiki kwa kuzingatia utawala bora, maadili ya utumishi wa umma, pamoja na kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Wiki iliyopita, Juni 11, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo pia aliwataka wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri za mkoa huo, kusimamia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hata baada ya mabaraza ya madiwani kuvunjwa.

Chongolo alitoa wito huo wakati wa kikao cha baraza la madiwani katika halmashauri ya Ileje lililofanyika kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).

Aliwataka wataalamu wanaobakia kutekeleza majukumu ya kitaalamu kutotumia mwanya wa kuvunjwa kwa mabaraza ya madiwani kufanya mambo kiholela.

“Hakikisheni fedha zinalindwa zaidi, kila mkuu wa idara anatakiwa ajibadilishe kuwa diwani kulinda fedha za Serikali na kuziba mianya ya ufujaji wa fedha hizi,” alisema Chongolo.

Mkuu huyo wa mkoa alivitaka pia vyombo vinavyosimamia utendaji wa halmashauri navyo vijibadili kuwa kama wajumbe wa baraza la madiwani sambamba na kuwa jicho la kuangalia kila taratibu zinazofanyika kwenye halmashauri zao.

Alisema vyombo vyote vya usalama vimeunganishwa na vina jukumu la kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha za Serikali huku akivitaja kuwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkuu wa Wilaya ambaye ni msimamizi mkuu wa shughuli zote za Serikali ngazi ya wilaya, pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ambaye pia ni mjumbe wa baraza la madiwani na vikao vya Wakuu wa Idara (CMT) wa halmashauri.

“Macho yote yanapaswa kuelekezwa kwenye vikao vya halmashauri ili kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa,” alisema Chongolo.

Aidha, aliwataka maofisa tarafa nao kuwajibika kwa nafasi zao kwa kuwa ni wawakilishi wa Serikali Kuu katika ngazi ya serikali za mitaa.

Related Posts