Mwanza. Katika ulimwengu wa sasa uliotawaliwa na teknolojia na mitandao ya kijamii, uaminifu katika uhusiano unapitia majaribu mapya.
Ingawa usaliti wa kimapenzi si jambo geni, kuibuka kwa njia mpya za mawasiliano kama WhatsApp, Instagram, Facebook, Snapchat, na hata programu za kutafuta wachumba kumebadilisha sura ya usaliti.
Siku hizi, si lazima mtu ahusike kimwili na mtu mwingine ili aitwe msaliti. Mazungumzo ya siri, kutumiana picha au ujumbe wa kimahaba mtandaoni, vinachukuliwa kama usaliti wa kihisia kwa wenza.
Tofauti na usaliti wa kimwili ambapo mhusika hujihusisha kimapenzi na mtu mwingine, usaliti wa kihisia mtandaoni hutokea pale mtu anapojenga uhusiano wa karibu wa kihisia na mtu mwingine nje ya uhusiano wake wa sasa kupitia majukwaa ya kidijitali.
Hilo hufanyika kwa kutumiana ujumbe wa kimahaba, mazungumzo ya mara kwa mara yasiyo rasmi, au hata kushiriki mambo ya faragha na mtu ambaye si mpenzi wake halali.
Kinachofanya usaliti huu kuwa tata ni kuwa hauonekani wazi kama ule wa kimwili. Wengi hujaribu kuhalalisha kwa kusema, “Hatukukutana uso kwa uso,” au “Ni maongezi tu ya kawaida.”
Mitandao ya kijamii imerahisisha mawasiliano lakini pia imefungua milango ya majaribu. Kwa mfano, mtu anaweza kuanza kuwasiliana na mpenzi wa zamani (ex), au mtu anayemvutia, kupitia mtandao bila mwenza wake kujua.
Mazungumzo haya yanaweza kuanza kama utani tu au mazungumzo ya kirafiki, lakini baadaye yakageuka kuwa ya siri, ya kina na ya kihisia.
Programu kama Snapchat hufuta ujumbe moja kwa moja baada ya kutazamwa, hali inayowafanya watumiaji kuwa na uhuru wa kusema au kutuma chochote bila hofu ya ushahidi kubaki. Vilevile, baadhi ya watu hutumia majina bandia.
Maoni kuhusu usaliti wa kihisia yanatofautiana. Wapo wanaochukulia jambo hilo kama kosa kubwa linalopaswa kumaliza uhusiano, huku wengine wakiliona kama kosa linalosameheka endapo halijafikia hatua ya kimwili.
Hata hivyo, tafiti nyingi zinaonesha kuwa watu wengi huumia zaidi wanapogundua wenza wao walikuwa na uhusiano wa kihisia na watu wengine.
Mariam Msangi mshauri wa uhusiano jijini Dar es Salaam, anasema: “Kusaliti kihisia huonesha kuwa tayari kuna pengo la kihisia katika uhusiano. Watu hawaanzi tu kuzungumza na wengine bila sababu. Mara nyingi ni matokeo ya kutotimizwa kihisia au kutokuwa na mawasiliano ya wazi na mwenza.”
Kusaliti kihisia kwa njia ya mtandao kunaweza kuathiri uhusiano kwa kuvunjika kwa uaminifu. Mwenza anapogundua kuwa mpenzi wake alikuwa na mazungumzo ya siri, mara nyingi uhusiano hupoteza uaminifu wa msingi.
Migogoro hutokea mara kwa mara inayoweza kusababishwa hata kwa mambo madogomadogo.
Athari nyingine ni kujitenga kihisia. Mwenza anayeendelea na usaliti wa mtandaoni, huanza kujitenga kwa mwenza wake wa halali, jambo linalodhoofisha ukaribu wao.
Pia afya ya akili huwa mashakani. Usaliti unaweza kusababisha msongo wa mawazo, huzuni, au hata kushuka kwa hali ya kujithamini kwa mwenza aliyeumizwa.
Ingawa mitandao ya kijamii na programu za mawasiliano hutoa changamoto mpya kwa uaminifu, si sahihi kusema kuwa teknolojia ndiyo chanzo cha matatizo haya. Teknolojia ni chombo, ni namna tunavyokitumia ndiyo huleta matokeo. Uhusiano mwingi pia umeimarika kwa kutumia mitandao ya kijamii kama njia ya mawasiliano, hasa kwa wapenzi waliotengana kwa umbali.
Njia za kukabiliana na usaliti wa mtandaoni
Mosi, uwazi katika Mawasiliano. Wapenzi wanapaswa kuzungumza wazi kuhusu mipaka ya kile kinachokubalika na kisichokubalika katika mawasiliano ya mtandaoni.
Pili, kujenga uaminifu. Ikiwa kuna tatizo katika uhusiano, ni vyema kulizungumza badala ya kutafuta faraja kwa mtu mwingine.
Tatu, kuepuka vichocheo. Ikiwa mtu anajua kuwa mazungumzo na mtu fulani yanazidi mipaka, ni busara kukatisha mawasiliano hayo kabla hayajaharibu uhusiano halali.
Nne, kuomba msaada wa ushauri. Wakati mwingine, msaada wa kitaalamu kutoka kwa mshauri wa uhusiano unaweza kusaidia kurejesha maelewano na kuepuka usaliti.
Usaliti wa kihisia kwa njia ya mtandao unazidi kuongezeka na kuumiza wengi kimya kimya. Wakati mwingine, maumivu ya usaliti wa maneno yanaweza kuwa makali kuliko ya mwili.
Ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha anaheshimu mipaka, anakumbuka maadili ya uhusiano, na kutumia teknolojia kwa njia chanya. Uaminifu bado una nafasi hata katika enzi ya kidijitali.