Miili ya wanandoa yakabidhiwa familia, utaratibu watolewa

Dar es Salaam. Familia ya wanandoa waliokutwa wameuawa chumbani kwao eneo la Tabata Bonyokwa Gk, wilayani Ilala jijini Dar es Salaam wamekabidhiwa miili kwa ajili ya kuendelea na taratibu zingine za mazishi.

Wanandoa hao, Antoni Ngaboli (46) na Anna Amiri (39) walikutwa wakiwa wamefariki dunia chumbani mwao usiku wa kuamkia Juni 12, 2025.

Awali, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akizungumzia tukio hilo alisema walikutwa wamefariki dunia huku miili yao ikiwa na majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.

Kamanda Muliro alisema uchunguzi ulikuwa ukiendelea na miili ilipelekwa hospitalini asubuhi ya Juni 12, 2025 kwa uchunguzi zaidi na ndugu walijuzwa wasubiri kwanza.

Leo Jumatatu, Juni 16, 2025, msemaji wa familia hiyo, Nuhu Msangi amesema tayari wamekabidhiwa miili hiyo na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuendelea na taratibu za mazishi ya wapendwa wao.

Msangi amesema wanatarajia miili hiyo itawasili yalipokuwa makazi yao na taratibu nyingine kuendelea.

“Tayari tumeshakabidhiwa miili na tunatarajia miili ya marehemu hao itawasili katika nyumba yao Bonyokwa saa 11 jioni na kisha itafanyika ibada fupi na miili hiyo itakuwa hapo hadi kesho taratibu za kuwaaga zitakapoanza,” amesema.

“Kesho tunatarajia ratiba ya kuwaaga marehemu hao itaanza saa tatu asubuhi kisha baaaye kuelekea Kanisa Katoliki Bonyokwa kwa ajili ya ibada na kuwaaga wapendwa wetu kisha tutasafiri kuelekea Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi,” amesema Msangi ambaye pia ni baba mdogo, Antoni.

Awali, Msangi amesema wanatarajia kuipumzisha miili ya wanandoa hao katika makazi yao ya milele kwenye Kijiji cha Ngulu, wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro Jumatano Juni 18, 2025.

Amesema marehemu hao watazikwa eneo moja kwa kuwa walikuwa wanandoa.

“Kwa mujibu wa mila zetu mwanamke akiolewa anakuwa wa kwetu, hivyo Ally na mkewe watazikwa katika eneo moja,” ameeleza.

Ally alikuwa Muislamu kabla ya kubadili dini na kuwa Mkristo.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia, marehemu hao wameacha watoto watano.

Juni 13, 2025, Joseph Masoud, kaka wa Antoni, alipozungumza na Mwananchi alisimulia tukio hilo akisema alipokea taarifa kutoka kwa dada yake akiambiwa nyumbani kwa mdogo wake (Antoni) kuna tukio limetokea hivyo, yeye na mkewe wameuawa.

“Nilipigwa butwaa lakini nilivaa ujasiri kama mwanamume nilitaka kuthibitisha nilichoambiwa, nilipanda pikipiki hadi nyumbani kwa marehemu ambako nilishuhudia umati wa watu,” alisimulia.

“Awali sikuruhusiwa kuingia lakini muda mchache baada ya polisi kufika nilijitambulisha kuwa mimi ni kaka wa marehemu waliniruhusu. Nilishuhudia miili ya kaka na shemeji ina majeraha, huku ikivuja damu ndani ya chumba cha kulala.

“Nilishuhudia mwili wa kaka ukiwa na jeraha kubwa upande wa moyo, huku shemeji akiwa na majeraha na amefungwa kitambaa maeneo ya usoni. Funguo za dukani na simu vilikuwa sakafuni, pia kuna kiasi cha fedha kilikuwamo ndani,” alisema.

Akisimulia namna alivyobaini kutokea kwa tukio hilo, msaidizi wa kazi za ndani wa familia hiyo, Mariam Said alisema waligundua kutokea kwa tukio hilo baada ya mtoto wa marehemu kugonga kwa muda mrefu chumba cha wazazi wake asubuhi akihitaji nauli ya kwenda ‘tuisheni’ (kwenye masomo ya ziada) bila ya mafanikio.

Alisema baadaye akiwa anafanya usafi nje ya dirisha la wanandoa hao aliona hali iliyomtia shaka baada ya kuona dirisha la wanandoa hao limevunjwa kidogo huku pazia likiwa na madoa mithili ya damu.

“Nilikimbia kumueleza mtoto wao mkubwa ambaye alikimbia kwa haraka kuingia chumbani kwao na kukuta miili yao ikiwa imejeruhiwa,” alisema Mariam.

Alisema baada ya kuwapigia baadhi ya ndugu waliwashauri kutoa taarifa kwa majirani waliowasaidia kutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa.

Mariam alisema awali kabla ya tukio hilo kutokea majira ya saa mbili usiku (jana) wanandoa hao walirudi nyumbani na baada ya kula chakula usiku waliingia ndani kupumzika.

“Baada ya hapo hatukusikia makelele wala kiashiria chochote kibaya hadi asubuhi tulipoiona miili ya dada na kaka ikiwa imejeruhiwa,” amesema Mariam huku akibubujikwa na machozi.

Related Posts